Sunday, May 10, 2015

SOMA MAKUBWA YALIYOJIRI MAGAZETINI LEO, MAY 10 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo pia kinatoa kozi ya Kiingereza na Computer pamoja na huduma ya Hostel. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746

LWOOO
MWANANCHI
Mbio za urais ndani ya CCM sasa zimefikia pabaya baada ya kuibuka hofu ya kuwapo kwa mpango wa kuivuruga Kamati Kuu kabla ya haijakutana kuchuja majina ya makada watakaotakiwa kupigiwa kura na Halmashuri Kuu ili kumpata mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu.
Hadi sasa CCM haijatangaza ratiba yake kwa ajili ya kuongoza wanachama wanaotaka kuwania uongozi wa ngazi mbalimbali kwa tiketi ya chama hicho.
Hata hivyo, Kamati Kuu ya CCM itakutana Mei 20 na kufuatiwa na vikao vya siku mbili vya Halmashauri Kuu Mei 21 na 22 kwa ajili ya kupitisha ratiba, ilani na taratibu nyingine za uchaguzi, ikiwa ni kuashiria kuanza rasmi kwa mchakato wa uchaguzi ndani ya chama hicho kikongwe.
Wakati chama kikitafakari kuanzisha rasmi mchakato wa uchaguzi, tayari kuna habari kuwa moja ya makundi ya makada wanaowania urais limeonyesha kutokuwa na imani na mwenendo wa Kamati Kuu ambayo ina jukumu la kuchuja wanaowania urais na kupeleka majina Halmashauri Kuu kwa ajili ya kupigiwa kura.
Taarifa zinaeleza kuwa kundi hilo linashawishi wanachama ili wakubali kuomba kupiga kura ya kutokuwa na imani na Kamati Kuu kwa madai kuwa inaonekana kupendelea baadhi ya waliojitokeza na kubana wagombea wengine.
“Kuna mkakati wa kuweka CC itakayowasaidia kwa kuwa ukishapita hapo, umeshakuwa Rais wa nchi hii. Uzuri ukishinda ndani ya chama na kutangazwa kuwa mgombea wao, basi makundi yote hurudi kukipigania chama na wengine kujipendekeza ili wapewe nafasi katika serikali ijayo,”.
MWANANCHI
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki ameteua timu ya wahandisi kutoka Wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kufanya tathmini ya uharibifu wa miundombinu kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha pamoja na kujua gharama stahiki kulirudisha jiji katika hali yake.
Sadiki alisema kuwa baada ya kufanya tathmini hiyo, itatoa mwanga ni kiasi gani kinahitajika ili kurudisha miundombinu iliyoharibika katika hali yake ya kawaida.
“Siwezi nikasema leo (jana) kuwa miundombinu iliyoharibikia itafanyiwa matengenezo kwa kiasi hiki au kile, subirini. Nimeitisha wahandisi na wanaendelea na kazi,” Sadiki
“ Hiki kitu siyo cha kukurupuka kina taratibu na sheria zake inabidi zifuatwe, hayo yote yakishakamilika wananchi wa mkoa huu watafahamishwa lini ukarabati unaanza na kwa kiasi gani, kwani hapa hakuna siri,”.
Alisema mvua zimelivuruga jiji na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu.
Aliyataja maeneo yaliyoathirika zaidi kutokana na mvua hizo ni pamoja na Keko, Chang’ombe Maduka Mawili, Yombo Vituka, Vingunguti, Africana, Msasani Bonde la Mpunga, Jangwani, Manzese, Kigogo, Mburahati, Boko na Basihaya.
Licha ya kuathirika na mafuriko yaliyotokana na mvua zilizoonyesha mfululizo kwa siku kadhaa, wakazi wa maeneo yaliyopatwa na adha hiyo wamesisitiza kuwa hawatahama katika makazi yao kwa sababu mafuriko yamewafuata.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili walidai kuwa wameishi maeneo hayo kwa miaka mingi, wakipata huduma zote, ikiwamo maji, umeme lakini hakukuwa na adha hiyo, huku wakiitupia lawama Serikali kwa kushindwa kutafuta jinsi ya kuwasaidia.
MWANANCHI
Wakati viongozi wa vyama vya upinzani wakieleza hofu ya Uchaguzi Mkuu kuahirishwa, Tume  ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesitisha mchakato wa kuandikisha wapigakura mkoani Mbeya uliopangwa kufanyika kuanzia Mei 5 hadi itakapotangazwa tena.
Tayari kazi hiyo inaendelea kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Iringa ambako kazi hiyo pia ilianza kwa kusuasua, na NEC ilitarajiwa kuongeza kasi ya uandikishaji kwa kuingia mikoa ya Dodoma, Katavi na Mbeya ambako mpango huo umesitishwa kwa muda usiojulikana.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Dk Lazaro Samweli alisema walipewa taarifa za kusitisha uandikishaji hadi hapo watapotaarifiwa tena licha ya Tume hiyo kupeleka vifaa vya BVR.
Mwezi uliopita, Nec ilitangaza kwamba ingeanza kazi hiyo ya kuboresha Daftari la Wapigakura mkoani hapa Mei 5, jambo ambalo lilisababisha uongozi wa jiji utangaze nafasi za kazi ya kuandikisha kwa wenye ujuzi wa kompyuta.
“Kabla ya Mei 4, ofisa kutoka Tume ya Uchaguzi alikuja akatuambia tusimamishe mchakato wa kuwapata watu wa kusimamia hadi hapo tutakapotaarifiwa, lakini vifaa tulishavipokea, hivyo tunawasubiri wao watakavyotuelekeza taratibu zao kwa mara nyingine tena,”Dk Samweli.
Alisema walipokea mashine 86 za BVR kutoka NEC na kwamba mashine 15 kati ya hizo ni kwa ajili ya mafunzo ya waandikishaji na 71 zinazosalia zitakuwa maalumu kwa kazi yenyewe ya kuandikishia.
Viongozi wa vyama vya upinzani wamekuwa wakituhumu kuwa kusuasua huko kwa kazi ya kuboresha Daftari la Wapigakura ni mpango wa kutaka Serikali ya Awamu ya Nne iongezewa muda kwa kuwa haijajiandaa kukabidhi madaraka.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema hakuwa na taarifa za kusitishwa kwa uandikishaji mkoani Mbeya, lakini akaongeza kuwa wananchi wanatakiwa kuwa wavumilivu kwani uandikishaji utafanyika kama ulilovyopangwa.
Unajua sikuwa na taarifa hizo kwa sababu nilikuwa katika kikao na wenyeviti wenzangu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Kama kweli limesitishwa, itakuwa ni mchakato mdogo wa maandalizi haujakamilika. Ila niwatoe hofu wakazi wa mkoa huo uandikishaji utafanyika kama ulivyopangwa,” Jaji Lubuva.
MWANANCHI
Siku moja baada ya Ikulu kutangaza kuwasafisha mawaziri watano na Katibu Mkuu, Eliackim Maswi, wabunge wamejiweka pembeni na suala hilo wakisema Bunge lilishatimiza wajibu wake.
Juzi, Ikulu iliwasafisha mawaziri wanne walioshinikizwa kuachia ngazi na Bunge kutokana na kuhusishwa na sakata la Operesheni Tokomeza Ujangili na mmoja aliyejiuzulu kutokana na kashfa ya uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow, pamoja na katibu mkuu wa wizara.
Waliotangazwa na Ikulu kuwa safi ni Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Shamsi Vuai Nahodha, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Wawili hao wanatajwa kwenye kinyang’anyiro cha urais kwa tiketi ya CCM ingawa hawajatangaza nia.
Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki na aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, David Mathayo.
Hali kadhalika, Profesa Sopster Muhongo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye alijiuzulu kutokana na kashfa ya escrow, pamoja na katibu mkuu wa wizara hiyo, Eliackim Maswi aliyesimamishwa kutokana na sakata hilo, wametangazwa kuwa safi.
Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa alisema kitendo cha Serikali kutangaza kuwa mawaziri hao hawakuhusika katika kutekeleza makosa yaliyotokana na Operesheni Tokomeza, kinaonyesha nia ya kuendeleza tabia ya viongozi kutopenda matatizo yaliyotokea wakiwa madarakani.
“Kilichofanyika ni kuionyesha dunia kuwa hakuna kuwajibika, unapopewa jukumu lazima uwajibike. Sijui Taifa hili linakwenda wapi? Nakosa hata maneno ya kuzungumza,” Msigwa.
Mbunge wa viti maalumu (CCM), Esther Bulaya alisema kuwa katika taarifa hakuna kipya kwani haina tofauti na ile ya Kamati ya Bunge iliyoundwa kuchunguza suala hilo.
“Jana (juzi) nilimsikiliza kwa makini sana (Katibu Mkuu Kiongozi) Balozi Sefue wakati akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari ila kichwani lilinijia swali moja tu; hivi madai yaliyotolewa na wananchi katika tume iliyoundwa kuchunguza jambo hili ya kweli au si kweli?” Bulaya.
JAMBOLEO
Idadi ya watu waliokufa katika mafuriko yaliyotokea Dar es Salaam Jumatano na Alhamisi wiki iliyopita, baada ya mvua kubwa kunyesha, imeongezeka na kufikia watu 10.
Wakati matukio hayo yakitokea, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA ) imewaasa wakazi wa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam, kutopumbazwa na jua lililotoka jana, kwani mvua hiyo itaendelea kunyesha leo katika maeneo mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik alisema kuwa madaktari kutoka Hospitali ya Amana, Temeke na Mwananyamala wamethibitisha kutokea kwa vifo hivyo, ambavyo vimesababishwa na mafuriko.
“Ni lazima madaktari wathibitishe vifo hivyo kwa sababu wapo watu ambao huenda walinyongwa na kutupwa kwenye maji wakati ule wa mvua, ambapo unaweza kusema wamekufa kwa mafuriko, kumbe sivyo,”.
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa taarifa alizopokea kutoka kwa madaktari hao, mpaka sasa ni watu 10 ambao wamekufa, kutokana na mafuriko hayo.
Pia, alisisitiza kuwa kwa wale wote waliokumbwa na mafuriko hayo, hakuna msaada wowote kutoka serikalini watakaopata kwa kuwa waliambiwa muda mrefu wahame kwa kuwa hayo ni mazingira hatarishi, hawakufanya hivyo.
Mpaka sasa zaidi ya wakazi 300 wa kata ya Jangwani jijini Dar es Salaam, wamekimbia nyumba zao kutokana na nyumba 90 hadi 100 za wakazi hao kufunikwa na maji.
HABARILEO
Mganga mmoja wa kienyeji amekamatwa akifanya ushirikina katika Mahakama ya wilaya ya Bunda mkoani Mara kwa kutumia tunguli ili kuwezesha kushinda kesi.
Mganga huyo ni moja kati ya waganga sita, ambao walikamatwa kwa kosa la kupiga ramli chonganishi na kufunguliwa kesi katika mahakama hiyo ya wilaya.
Mtuhumiwa huyo pamoja na wenzake hao, walikamatwa Machi 11 mwaka huu saa 6:00 mchana katika kijiji cha Kabasa wilayani hapa, wakipiga ramli chonganishi ya kuchonganisha wananchi kinyume cha sheria.
Mtuhumiwa huyo aliyeshikwa juzi akifanya ushirikina huo katika mahakama hiyo ni Riku Wasaga Yahaya, mkazi wa kijiji cha Kabasa wilayani hapa.
Mtuhumiwa huyo pamoja na wenzake hao, walipokamatwa wakipiga ramli chonganishi, walifunguliwa kesi namba 86 ya mwaka huu katika mahakama hiyo.
Mwendesha mashitaka wa Polisi, Athumani Salum, alidai kuwa juzi wakati watuhumiwa hao wakiwa mahakamani hapo, wakisubiri kesi yao kutajwa, mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Said Hamad Kasonso, mtuhumiwa Yahaya alionekana akifanya ushirikina kwa kutumia tunguli.
Ilidaiwa baada ya mtuhumiwa huyo kupekuliwa na polisi, walimkuta akiwa na vibuyu viwili vya tunguli na dawa ya ungaunga na mchanga mfukoni mwake, alivyokuwa anavitumia kufanyia ushirikina katika mahakama hiyo.
Hakimu Kasonso alisema mtuhumiwa huyo na wenzake watano, walikamatwa wakijaribu kufanya ushirikina wa kuroga mahakama hiyo, jambo ambalo ni la ajabu mno, kwani Mahakama ni chombo ambacho kazi yake ni kutoa haki na kutafsiri sheria kikamilifu na kwa kina zaidi ili haki iweze kutendeka.
Hakimu Kasonso alisema kuwa kitendo hicho cha ushirikina ndani ya chombo cha haki, kamwe hakiwezi kuvumiliwa na hivyo mahakama hiyo inawapeleka mahabusu watuhumiwa wote sita kwa muda wa siku 14 hadi Mei 22, mwaka huu, kesi yao itakapotajwa tena mahakamani hapo.
Mahakama ni chombo cha kisheria ambacho kinatoa haki baada ya kuitafsiri sheria kwa kina zaidi na kisha kutoa maamuzi, sasa kitendo cha kuja kufanya ushirikina katika chombo ambacho kazi yake ni kutenda na kutoa haki, kamwe hakiwezi kuvumiliwa, hivyo watuhumiwa wote waende mahabusu siku 14,”.
HABARILEO
Mtu yeyote atakayepatikana akiingiza au kuuza silaha za bandia, atahukumiwa kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini isiyozidi Sh milioni 10.
Adhabu hiyo imetajwa na Muswada wa Usimamizi na Udhibiti wa Silaha na Risasi wa mwaka 2014.
Muswada huo ni moja ya miswada tisa ambayo Rais Jakaya Kikwete amesaini kuwa sheria. Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema Rais Kikwete alisaini sheria hizo tisa Aprili 25, mwaka huu.
Alisema Muswada huo wa Usimamizi na Udhibiti wa Silaha na Risasi wa mwaka 2014, unaweka kikomo cha umri wa kumiliki silaha, pia umepiga marufuku na kudhibiti uingizwaji na uuzwaji wa silaha bandia nchini.
“Sheria hiyo inapiga marufuku kwa silaha za bandia kuingizwa na kuuzwa nchini na mtu yeyote atakayepatikana na silaha hizo za bandia atahukumiwa kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini isiyozidi milioni 10” .
Pia, Rais amesaini Muswada wa Sheria ya Miamala ya Kieletroniki wa mwaka 2015, wenye lengo la kudhibiti uhalifu wa kifedha na udanganyifu wa bidhaa na huduma katika mtandao.
Muswada mwingine uliosainiwa ni wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Tume ya Kudhibiti Ukimwi wa mwaka 2015, ambayo inatoa mwanya wa kuanzisha Mfuko wa Kudhibiti Ukimwi ili kupunguza utegemezi wa fedha za wahisani katika kudhibiti janga hilo.
Alisema sheria nyingine ni ile ya Baraza la Vijana ya mwaka 2015, ambapo baraza hilo litakuwa chombo cha kusaidia Serikali kufikia vijana kwa urahisi na pia litakuwa ni jukwaa rasmi kuzungumzia masuala muhimu, yanayohusu maisha yao na kubaini changamoto zinazowakabili na kubuni mikakati ya kuzitatua.
Miswada mingine ambayo Rais amesaini ni ya Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Risiti Ghalani, Sheria ya Kusimamia Ajira ya Watu Wasio Raia wa Tanzania, Sheria ya Makosa ya kwenye Mtandao na Sheria ya Takwimu.
HABARILEO
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amedai kuwa majangili wote wanaotiwa mbaroni na vikosi vya Askari wa Wanyamapori, wanadaiwa wanatumwa na watu waliopo kwenye ofisi za serikali na wengine nje ya nchi.
Amesema mtandao wao ni mkubwa lakini ameapa kula nao sahani moja.
Nyalandu alisema hayo jana wakati wa ziara yake wilayani Masasi mkoani Mtwara, alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Idara ya Wanyamapori, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakuu wa idara na Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani hapa.
Sambamba na hilo, amewaagiza maofisa wanyamapori na misitu nchini, kumkamata mwananchi yeyote atakayevamia hifadhi za wanyamapori zilizotengwa.
Nyalandu alisema kuwa hatua ya kwanza ambayo serikali imedhamiria kuchukua katika mapambano hayo dhidi ya ujangili ni kuvipatia vyombo vya ulinzi na usalama vitendea kazi vya kiintelejensia ili vyombo hivyo viweze kufanya kazi kwa kupashana habari kati ya Tanzania na nchi jirani.
Alitaka maofisa wanyamapori na misitu nchini, kufanya kazi zao kwa kufuata kanuni na taratibu za nchi na kwamba waache kufanya kazi kwa mazoea.
Alisema ujangili ni tishio kubwa kwa wanyamapori nchini na kwamba kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya sheria na Katiba na Wizara ya Maliasili na Utalii, zimeandaa mpango mkakati wa kukabiliana na tatizo hilo la ujangili, linaloathiri sekta ya utalii nchini.
Alisema vyombo vya ulinzi na usalama ni nguzo muhimu katika kulinda usalama wa nchi, lakini vyombo hivyo vinaweza kushindwa kutekeleza jukumu hilo, kutokana na kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha katika kupashana habari na kupeana taarifa mbalimbali za kiintelejensia.
Nyalandu alisema taifa kila siku linapoteza rasilimali zake muhimu na kwamba jambo hilo linarudisha nyuma uchumi wa taifa, hivyo hatua ya serikali kutaka kuvipatia vyombo vya ulinzi na usalama vitendea kazi vya kisasa, itasaidia kuwabaini watu wanaojihusisha na biashara ya ujangili nchini.
Kwa mujibu wa waziri huyo, serikali inatambua wajibu na umuhimu wa vyombo vya ulinzi na usalama lakini ili vyombo hivyo viweze kufanya kazi kwa ufanisi, ushirikiano wa karibu ni lazima.
Alisema Wizara ya Maliasili kwa kushirikiana na Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpool) na Idara ya Wanyamapori, watahakikisha wanawasaka majangili wote duniani, lengo likiwa ni kukomesha vitendo hivyo.
MTANZANIA
Tume ya ushindani imeteketeza tani moja ya nyembe bandia aina ya Super Max zebye thamabi ya milioni 117.
Uteketezaji wa nyembe hizo ulifanyika jana jijini Dar es salaam katika mtambo wa kuteketeza taka wa Safe Waste Disposal Incinerator uliopo Wilayani Mkuranga,.
Mkurugenzi mkuu wa tume hiyo Fredrick Ringo alisema shehena ya nyembe hizo ilikamatwa katika bandari ya Dar es salaam wakati wa ukaguzi wa kawaida baada ya kukutwa kwenye kontena.
“Huwa tunafanya ukaguzi wa kawaida katika mizigo yote inayoshushwa katika bandari ya Dar, na tulibaini  shehena hili katika kitengo cha makontena cha TRH ikitokea China” Ringo
Usiwe mbali nami, kuwa karibu kila wakati na kukusogezea kila kinachonifikia hapa hapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment