Wednesday, May 13, 2015

WAKO WAPI WANAOMUENZI GWIJI WA FASIHI AFRIKA MASHARIKI NA BARA LA AFRIKA

Vitabu vya Shaaban Robert

Jina la Shaban Robert ni maarufu miongoni mwa wa-Tanzania na wengine wa nchi zingine wanaokijua Kiswahili. Lakini, tujiulize ni wa-Tanzania wangapi  ambao wamesoma angalau vitabu vichache vya Shaaban Robert. Ni wangapi wamesoma au wanasoma mashairi yake, tenzi zake, insha zake, barua zake, na riwaya zake?

Ni wangapi wamesoma vitabu vyake vingine, kama vile Wasifu wa Siti Binti Saad, Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini, na tafsiri yake ya mashairi ya Omar Khayyam? Kama hatuna majibu ya kuridhisha, tuache kujigamba, kujidanganya na kudanganyana kuwa tunamwenzi mwandishi wetu huyu maarufu.

Ingawa kulikuwa na kipindi cha uhaba, leo vitabu vya Shaban Robert vinapatikana kirahisi Tanzania, baada ya kampuni ya uchapishaji ya Mkuki na Nyota kuanza kuvichapisha upya.

Imekuwa ni faraja kwangu kuvisoma, baada ya kuzinduka kutoka katika mazoea ya kusoma zaidi maandishi ya ki-Ingereza. Ninajiona kama vile nimeanza kujikomboa kimawazo. Lugha yako ni utambulisho wako, na kuifahamu na kuitumia vizuri ni ishara ya kuiheshimu lugha hiyo. Ni ishara ya kujiheshimu.

Pamoja na kununua na kusoma vitabu alivyoandika Shaaban Robert, ninajitahidi kupanua akili yangu kwa namna nyngine pia. Ninayo maandishi yanayochambua maandishi ya Shaaban Robert. Mfano ni vitabu vinavyoonekana hapa pichani, kimoja cha A.G. Gibbe, na kingine cha Clement Ndulute. Maandishi mengine yamo katika majarida na vitabu vingine ambavyo baadhi ninavyo pia.

No comments:

Post a Comment