HADITHI
YAMENIKUTA SALMA MIE
ILIPOISHIA
Aliponiambia hivyo nilishituka kidogo kwa sababu nilihisi Ibrahim
akisikia kumeingia ujumbe kwenye simu yangu anaweza kumpa Zacharia amsomee na
hivyo kugundua mipango yangu.Lakini nikasema potelea mbali liwalo na liwe.
Kuondoka ni lazima niondoke na Chinga.
“Siwezi kujilazimisha kuendelea kuishi na mwanaume ambaye simtaki”
nikajiambia kimoyomoyo.
Chinga akaniambia tuingie kwenye basi ambalo lilikuwa karibu na
mahali tulipokuwa tumesimama. Tukajipakia kwenye basi hilo la kampuni ya Rahaleo.Tulitafuta siti
zetu, tulipoziona tuliweka masanduku yetu kwenye kifaa cha kuwekea mizigo.
Tukaketi.
Vile tunaketi tu niliona mtu ambaye sikumtarajia akiingia ndani ya
basi hilo,
mkono mmoja akiwa ameshika bakora yake na mkono mwingine ameshikwa na kijana
ambaye bila shaka ndiye aliyemleta hapo stendi.
Alikuwa Ibrahim!
Moyo wangu ulishituka. Furaha niliyokuwa nayo yote ikanipotea. Nikabaki
kumtazama kuona alikuwa anataka kufanya nini.
Nilishajua kuwa alinifuata mimi baada ya kuugundua ule ujumbe
niliotumiwa na Chinga ambao ulimtambulisha kuwa nilikuwa nimetoroka kwake na
nilikuwa ninasafiri na mwanaume kwenda Dar er salaam kwa basi la Rahaleo.
Mabasi ya Rahaleo yalikuwa yakifanya safari zake Da er salaam na
Tanga.
Hata kama Chinga hakuandika kuwa tunakwenda Dar lakini kwa vile
alitaja basi la Rahaleo, Ibrahim alishajua kuwa tunakwenda Dar. Bila shaka
baada ya Zacharia kumsomea ujumbe huo wa Chinga kwenye simu yangu, Ibrahim
alimwaambia aangalie kwenye kabati ambako waliona nilikuwa nimechukua nguo zangu
zote muhimu na vitu vyangu vyote.
SASA ENDELEA
Hapo ndipo Ibrahim alipotaharuki na kukurupuka akaamua kunifuata
stendi. Sikujua ni kwanini aliletwa na kijana mwingine badala ya Zacharia
lakini nilipata jibu kuwa huenda ni kijana wa bodaboda aliyoikodi.
Chinga hakuwa ameshituka. Kwanza
alikuwa hamjui Ibrahim. Pengine alipomuona alidhani ni miongoni mwa abiria wa
basi hilo, isitoshe
alichokuwa anakijua Chinga ni kuwa nilikuwa nimeshaachana naye na nilikuwa
nimehamia kwa shangazi yangu.
Sasa sijui itakuwaje? Nikawaza. Hata hivyo nilipata moyo kidogo
kwa sababu Ibrahim mwenyewe asingeweza kuniona kwa vile haoni na kijana aliyekuja
naye alikuwa hanijui.
Nikatulia kimya kwenye siti huku nikizungumza na Chinga kama vile huyo mtu aliyeingia nilikuwa simjui.
Ibrahim alipoingia ndani ya basi hilo alisimama kando ya mlango
akauliza.
“Salma, umo ndani ya basi hili?”
Chinga akashituka wakati Ibrahim alipolitaja jina hilo . Mimi nikanyamaza
kimya.
“Anamuuliza nani?” Chinga akaniuliza kwa sauti ya chini.
Nikamjibu “Sijui”.
Ibrahim akauliza tena.
“Jamani namtafuta mke wangu anayeitwa Salma. Kama
yumo ndani ya basi hili naomba anijibu”
Chinga akanitazama. Bila shaka alikwisha gundua kuwa yule ni mume
wangu na Salma anayemtafuta ni mimi.Lakini aliponitazama hakuniambia kitu,
akageuza uso wake kumuangailia Ibrahim.
“Jamani mnaulizwa kuna mtu anayeitwa Salma mke wa huyu bwana?”
abiria mmoja akamsaidia Ibrahim kuuliza baada ya kuona watu wako kimya.
Abiria wakawa wanatazamana. Kila mtu akamtazama mwenzake. Kwa
bahati wanawake tulikuwa wengi humo ndani ya basi, kwa hiyo hakukuwa na
aliyenitilia shaka.
Yule abiria aliyemsaidia Ibrahim kuuliza akamwaambia “Naona hayumo”
“Kwani hili si ndilo basi la Rahaleo au kuna jingine?” Ibrahim
akauliza
“Liko jingine lakini limeshaondoka.Labda alikuwa kwenye basi hilo ” Ibrahim akajibiwa.
Hapo nikaona uso wa Ibrahim ukisambaratika na kuonekana kama aliyetaka kulia.Laiti ningekuwa na moyo wa
kibinaadamu ningemhurumia na pengine ningebadili mawazo ya kumkimbia.
Lakini ibilisi alikuwa amesha nishika sawasawa. Nilimuona Ibrahim
kama shetani aliyekuwa anataka kuzuia mafanikio yangu.
Ibrahim akageuka ili atoke ndani ya basi. Nikaona mistari ya
machozi ikitokeza chini ya miwani aliyokuwa amevaa.
Nilimchungulia Ibrahim kwenye dirisha wakati aliposhuka ndani ya
basi. Kijana aliyekuwa amemshika mkono alikuwa akienda naye mahali alipoiegesha
pikipiki yake.
“Imekuwaje Salma?” Chinga akaniuliza.
“Imekuwaje nini?” nikamuuliza ingawa nilishajua alichokusudia.
“Huwezi kunidanganya, huyu jamaa ndiye mume wako na alikuwa
anakuuliza wewe”
Nilibetua mabega “Aka! Si tumekwisha achana. Atakuwaje mume
wangu?”
“Sasa kama mmeachana mbona anakufuata?”
“Ni usumbufu tu, labda anataka kunibembeleza nirudi lakini mimi
sitarudi tena kwake”
“Na amejuaje kuwa unasafiri?”
Hapo sikuwa na jibu, nikamwaambia.
“Atajua mwenyewe, mimi sijui. Labda ameambiwa na shoga yangu Rita.
Rita naye kwa umbeya hawezekani!”
Wakati namuambia hivyo basi lilipigwa moto na kuanza kuunguruma
kwa sekunde chache kabla ya kuondoka.
Tulifika Dar er salaama saa sita mchana. Tukiwa katika kituo cha
mabasi cha Ubungo, Chinga alikodi taksi iliyotupeleka Sinza.
Nikamuuliza Chinga kwanini tunakwenda Sinza wakati
aliniambia nyumba yake iko Masaki.
“Nina nyumba mbili, moja iko Sinza na moja Masaki” Chinga
akanijibu.
Tulipofika Sinza niliiona nyumba ya Chinga. Ilikuwa nyumba ya
kawaida tu. Chinga akaniambia nyumba yake iliyokuwa Masaki ndiyo ya thamani
zaidi.
“Tutaanzia maisha hapa. Nikikuona una upendo wa dhati
nitakuhamishia kwenye nyumba yangu ya Masaki” Chinga akaniambia.
“Kwani umenionaje?” nikamuuliza.
“Sijaishi na wewe, siwezi kukujua kwa undani”
“Upendo umo ndani ya moyo wangu. Kama
sina upendo na wewe nisingemuacha mume wangu kwa ajili yako”
“Sasa ndiyo uuoneshe na mimi niuthibitishe”
Tulikuwa tumeshaingia ndani ambako tulimkuta kijana ambaye Chinga
aliniambia kuwa ni mkazi wa nyumba ya jirani anaye muachia nyumba anaposafiri.
Sebuleni palikuwa na fanicha za thamani. Chinga alinitembeza
nyumba nzima akanionesha kila kitu. Chumba chake cha kulala kilikuwa chenye
hadhi hasa, siyo kama kile nilichokuwa
ninalala na Ibrahim. Kwa jumla nilifurahia kuanza maisha mapya nikiwa na
mwanaume tofauti. Sikumfikiria tena Ibrahim wala sikumkumbuka.
Niliishi na Chinga kama mke na
mume ingawa hatukulizungumzia tena suala la ndoa. Mimi sikutaka kulizungumza
kwa sababu nilijijua kuwa bado nilikuwa mke wa Ibrahim na Chinga hakulizungumza
labda kwa sababu alitaka tuishi kwanza ili tupimane tabia.
Wiki moja baada ya kuanza maisha Chinga alininunulia simu nyingine
mpya ya bei mbaya. Pia alinifanyia shopping ya karibu nusu milioni. Akaniambia
zile nguo nilizotoka nazo Tanga nisizitumie tena kwa sababu haziendani na Jiji
la Dar. Viwalo alivyoninunulia vilikuwa ni vya fasheni za kisasa za kisichana. Sikumbuki
lile baibui langu nililitupia wapi.
Kila wiki tulikuwa tunatoka mara mbili kwenda kwenye matanuzi. Kumbi
zote za starehe za Dar sasa nilikuwa ninazifahamu. Hakukuwa na mahali ambako
sikupajua. Chinga alinifundisha ulevi nikawa mlevi wa kupindukia. Friji letu
halikukosa kuwa na bia kila siku.
Chinga alinitambulisha kwa marafiki zake mbalimbali waliokuwa
wakifanya biashara pamoja. Niliwazingatia marafiki zake wanne Frenk, Steven,
Jonathan na Mussa. Mara kwa mara watu hao walikuwa wanakuja nyumbani na kufanya
mazungumzo lakini Chinga hakutaka nisikilize mazungumzo yao .
Kuna siku walikuwa wakileta nyumbani vitu vya thamani kama TV na
Friji na vitu vingine ambavyo Chinga aliniambia vilitoka bandarini na baada ya
siku mbili tatu huvipeleka kwa wateja wao.
Kadiri siku zilivyokwenda Chinga alianzisha tabia mabayo sikuwa
nikiipendelea. Kuna siku ambazo hutoka na mimi lakini kuna siku ambazo hutoka
peke yake na kurudi usiku wa manane. Siku nyingine anarudi siku ya pili yake
tena mchana.
Kila ninapomuuliza hutoa sababu mpya. Kuna siku anazoniambia
amelala nje ya Jiji kuitokana na kazi zake za biashara na kuna siku ambazo
huniambia amechelewa kurudi nyumbani kwa sababu alikuwa na mikutano na
wafanyabiashara wenzake.
Pale ninapoonesha kukasirika kwa kumshuku kuwa ana wasichana
wengine, Chinga alikuwa hodari wa kunibembeleza na kujitakasa kwamba hakuwa na
msichana yeyote wa nje. Nikawa sina budi nikubaliane naye.
Ilipita miezi minne. Kuna siku Chinga aliniaga kuwa anakwenda
Tanga kumsalimia baba yake na kuchukua gari lake. Aliniachia pesa za kutosha na
ndani ya nyumba kulikuwa na kila kitu. Nakumbuka aliondoka asubuhi. Ilipofika
jioni wakati nimeketi sebuleni nikiangalia tv nikasikia gari likasimama huko
nje.
Nilipochungulia kwenye dirisha niliona teksi imesimama mbele ya
mlango. Nikaona msichana anashuka. Alionekana kama anatoka safari kwani dereva
alimteremshia masanduku mawili.
Teksi ikaondoka.Yule msichana akaja kubisha mlango. Nikanyanyuka
na kwenda kumfungulia.
“Hujambo?” akaniuliza.
“Sijambo, karibu”
ITAENDELEA kesho nini kitatokea na huyu msichana ni nani tukutane kesho hapahapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment