Wednesday, February 8, 2017

AISHI CHINI YA MUEMBE KWA MIAKA 19



Tanga, MHANGA wa mafuriko ya mvua za Elnino Magaoni Tanga, John Mhina mwenye umri zaidi ya 80, ameshangazwa na Serikali kushindwa kumpatia msaada mbali ya kuishi chini ya muembe kwa zaidi ya miaka 19.

Mzee huyo ambaye amejenga nyumba ya  miti na kuizungushia karatasi za plastic amesema toka nyumba yake isombwe na mvua za Elnino 1998  amekuwa akiishi chini ya muembe mvua jua ikiwa ni yake.

Amesema mke wake ambaye alikuwa akiishi nae alifariki mwanzoni mwa mwezi wa kwanza mwaka huu ambapo walikuwa wakiendesha maisha yao kwa kutegemea wasamaria wema.

Amesema mbali ya kuiomba Serikali kumjengea kibanda ambacho angeweza kujisitiri nyakati za mvua na jua amedai kuwa kilio chake hakuna aliekisikiliza hadi sasa.

Akiizungumzia changamoto hiyo, Mjumbe wa Serikali ya Mtaa Mtaa wa Magaoni, Abdalla Mwadege, amesema suala la mzee huyo liko katika ofisi za Halmashauri ya jiji na hawezi kulizungumzia kwa madai kuwa hajui lolote.

Amesema anachojua ni kuwa mzee huyo amefanya makazi yake chini ya muembe kwa miaka mingi na wajibu wake kama kiongozi ni kujua mazingira na usalama wake.
                                         





No comments:

Post a Comment