Sunday, February 5, 2017

HADITHI, ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU SEHEMU YA 27

HADITHI
 
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 27
 
ILIPOISHIA
 
“Kwanini akutaje wewe?”
 
“Alinitaja kwa kudhani nilikuwa na kisasi na Kweka na hivyo polisi walihisi kwamba mimi ndiye niliyemuua”
 
“Sasa walikupata wapi?”
 
“Walitumia mbinu. Walimwambia Vicky anipigie simu kutaka nikutane naye New Africa Hotel. Nilipofika New Africa nikakamatwa”
 
“Na huyo Vicky ulikutana naye hapo?”
 
“Ndiyo nilikutana naye. Wakati tunazungumza ndio polisi wakatokea na kunikamata”
 
“Mlipofika kituo cha polisi ikawaje?”
 
“Mimi nilikanusha kumuua Kweka na pia nilikanusha kufika katika hoteli ya Suzy. Niliwekwa ndani tangu asubuhi. Hii saa tisa ndio wakaniachia”
 
SASA ENDELEA
 
James akashusha pumzi.
 
“Usikae hapa mjini Simon, polisi wameshakujua”
 
Simon akakenua mdomo kutabasamu.
 
“Unaogopa nini James? Misukosuko ya kipolisi ni sehemu ya maisha yangu. Ninachojua mimi ni kwamba nitakimbizana na polisi mpaka nitaingia kaburini”
 
“Sikuwezi. Wewe umeshakubuhu”
 
“Sana”
 
“Unanidai kiasi gani tumalizane?”
 
Simon alimtajia kiasi ambacho aliahidi kumpa baada ya kumuua Kweka. James akaingia chumbani kwake na kutoa pesa hizo akampa.
 
“Asante sana”
 
Simon alizipokea na kunyanyuka.
 
“Twenzetu”
 
Walitoka tena nje.
 
“Nadhani mkataba wetu umeisha” Jamea alimwabia Simon huku akifungua mlangowa gari yake.
 
“Usijali” Simon alimjibu. Alikuwa akielekea alipoliegesha gari. James ndiye aliyetangulia kuondoka. Simon aliondoka nyuma yake.
 
Alikwenda kibaha alikokuwa amekodisha bastola, akairudisha bastola aliyokuwa ameikodi.
 
“Nipunguzie, sikutumia risasi hata moja dili yangu iliharibika” Simon alimwambia mtu aliyekuwa amemkodi bastola hiyo.
 
Mtu huyo aliipindisha bastola hiyo na kuangalia risasi zilizokuwa ndani.
 
“Kama hukuzitumia ni juu yako, hapa kwangu zimeshatoka. Nipe pesa yangu”
 
“Samson usinibabaishe, mimi sikuanza kufanya kazi na wewe jana au juzi. Kulibaki laki yako moja, sasa nitakupa nusu yake. Tena nakupa tu sikuifanyia kazi yoyote”
 
Simon akanyanyuka na kutoa shilingi elfu hamsini akampa. Samson alizipokea bila kusema chochote.
 
Simon alipotoka Kibaha alilirudisha gari alilokuwa amelikodi.
 
                                     *****************
 
Tkriban miaka arobaini na mitano iliyokuwa imepita, mtu mmoja aliyekuwa ametoka Zaire, hivi sasa Congo DRC, aliwasili katika mji wa Kigoma akiwa na mke wake. Waliweka masikani katika mji huo wakijishughulisha na shughuli za kilimo.
 
Baada ya miaka miwili yule mtu alifariki dunia kwa ajali ya gari. Aliyemgonga alikuwa anaitwa Stifano Kweka. Polisi wa usalama barabarani baada ya kuipima ajali iliyotokea waliona maraehemu ndiye aliyekuwa na makosa.
 
Lakini Stifano Kweka kutokana na utu wake aligharamikia mazishi ya marehemu na kumtunza mjane aliyekuwa ameachwa kwa kipindi cha karibu mwaka mmoja.
 
Miaka miwili baadaye Sitifano naye alifiwa na mke wake akaamua kumuoa yule mjane wa kikongo ambaye kwa wakati ule alikuwa akijitegemea mwenyewe..
 
Alihama naye mkoa wa Pwani na kuishi naye maeneo ya Kibaha. Haukupita muda mrefu yule mwanamke akapata ujauzito. Akajakuzaa watoto wawili pacha wa kiume, Alphonce Kweka na Isaac Kweka.
 
Wakati Alphonce na Isaac wanasoma sekondari mama yao akafa, akazikwa pale pale Kibaha. Mzee Kweka naye alifariki dunia siku chache tu baada ya Alphonce na Isaac kuanza elimu ya chuo kikuu wakiwa Dar es Salaam.
 
Alphonce alikuja kuangukia kwenye udaktari, akawa daktari bingwa wa upasuaji. Isaac akawa mchumi, akaanzisha kampuni yake ya biashara.
 
Alphonce alikuwa ameajiriwa katika hospitali ya Muhimbili lakini baada ya kufanya makosa ya kizembe akiwa daktari alihamishiwa wizarani na kupewa kazi nyingine.
 
Katika likizo yake moja Alphonce aliamua kwenda Congo alikotokea mama yao ili kuitafuta asili ya mwanamke huyo. Baada ya kuuliza uliza ukoo wao, aliambiwa kwamba babu yake alitokea Lagos Nigeria na alifika Zaire kabla ya uhuru.
 
Alphonce aliporudi Dar aliazimia siku moja aende Nigeria kuutafuta ukoo wa babu yake. Mwaka uliofuata alipopata likizo nyingine Alphonce akafunga safari ya kuelekea Nigeria.
 
Akiwa lagos alipangisha chumba katika hoteli moja na kuanza kazi ya kuuliza uliza. Jioni moja wakati yuko njiani akirudi pale hoteli kwa miguu alivamiwa na vijana wawili waliokuwa wanataka kumpora saa, simu na pesa alizokuwa nazo.
 
Alphonce katika kujiokoa alimchoma mmoja wa vijana hao kwa kisu kidogo cha kukunja. Alimchoma katika usawa wa moyo na kumuua pale pale. Kijana mwingine akakimbia.
 
Wakati tukio hilo linatokea kulitokea gari iliyosimama kando ya barabara. Msichana mmoja aliyekuwa akiendesha alifungua mlango na kumpungia mkono Alphonce. Alphonce alikwenda mahali liliposimama gari hilo.
 
“Umeshaua, ingia garini nikuondoe mahali hapa” Mwanamke huyo alimwambia Alphonce kwa kingereza.
 
Alphonce kwa kuona kweli alikuwa ameua alijipakia kwenye gari hilo haraka.
 
“Wale vijana walikuwa wanataka kuniibia” Alphonce alimwambia msichana huyo mara tu alipoliondoa gari.
 
“Niliona tangu nilipokuwa ninakuja, ndio maana nilisimamisha gari kukusaidia”
 
“Wamenishitua sana, nilikuwa katika mawazo tofauti, yaani kama nisingetumia kisu wangeniumiza na kuniibia kila kitu”
 
“Hilo ndilo tatizo lilioko katika jiji letu. Kuna vijana wengi wasio na kazi. Sasa wamekuwa ni tishio kwa wageni na wakazi wenyewe”
 
Alphonce akagutuka kidogo. Aligutuka baada ya kuambiwa vijana hao wamekuwa ni tishio kwa wageni…
 
Akajiuliza, msichana huyo amejuaje kama yeye ni mgeni? Na alimuona wapi?
 
Kama vile msichana huyo alisoma mawazo ya Alphonce, akamwambia.
 
“Hatufahamiani. Mimi naitwa Mwana, mwenzangu unitwa nani?”
 
“Naitwa Alphonce”
 
“Nimekuwa nikikuona katika hoteli fulani, sijui ni wewe au nimekufananisha?”
 
“Hoteli gani?”
 
Msichana alimtajia jina la hoteli ambayo amekuwa akimuona Alphonce tangu alipowasili nchini humo.
 
“Ni kweli, nimepanga chumba katika hoteli hiyo”
 
“Mimi ninafika sana pale hoteli, hata mchana wa leo nilikuja kula pale na nilikuona”
 
“Nimefurahi sana kukufahamu”
 
“Na mimi nimefurahi kukufahamu. Karibu sana nchini kwetu”
 
Kweka aligutuka tena.
 
Amejuaje kuwa mimi ni mgeni? Kupangisha chumba hotelini si lazima uwe mgeni.
 
Hata hivyo alimjibu.
 
“Asante sana”
 
“Unatokea Dar es Salaam?”
 ITAENDELEA KESHO USIKOSE

No comments:

Post a Comment