HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 25
ILIPOISHIA
“Tulikuwa tumetengana
kidogo…”
“Kwa vipi?”
“Niliwahi kupata matatizo
kidogo ya kipolisi nikashitakiwa kwa kuhisiwa kuwa nilifanya mauaji ya msichana mmoja lakini mahakama
ikaona sikuwa na hatia ikaniachia huru. Sasa niliporudi uraiani Vicky akaniambia kuwa alidhani
ningenyongwa hivyo ndoa yetu alishaivunja kwa Padre”
“Unamfahamu mtu anayeitwa
Kweka?”
Simon alishituka alipoulizwa
swali hilo.
Mshituko wake ulionekana waziwazi.
Akajiambia akijibu kuwa
hamfahamu atajiingiza katika matatizo kwani hakujua Vicky aliwaeleza nini
polisi.
“Namfahamu” akajibu baada ya kusita
kidogo.
“Tueleze unavyomfahamu?”
“Ni rafiki yangu”
“Ni kweli kwamba alimuoa mke
wako baada ya wewe kuwekwa ndani kutokana na kesi iliyokuwa inakukabili?’
Simon aligundua kuwa hilo swali lilikuwa la
mtego.
“Vicky aliwahi kunieleza kuwa
aliolewa na mtu mwingine lakini nilimwambia kuwa hakupaswa kuolewa”
“Alikwambia aliolewa na
nani?”
SASA ENDELEA
“Hakuniambia. Labda leo baada
ya kukutana naye ndio angeniambia”
“Baada ya kukwambia kuwa
ameolewa na mtu mwingine ulikasirika sana?”
“Sikukasirika”
“Bila shaka ulitaka kumjua
mtu ambaye alimuoa mke wako?”
“Sikutaka kumjua”
“Na bila shaka ulikuwa na
kisasi naye?”
Simon akatikisa kichwa.
“Kisasi cha nini. Wanawake si
wamejaa tele”
“Jana majira ya saa sita
mchana ulikuwa wapi?”
“Nilikuwa katika shughuli
zangu”
“Utakataa kwamba ulionekana
katika hoteli ya Suzy saa sita mchana”
Hapo Simon hakutaka kukubali.
Aliona akikubali tu atahusishwa na mauaji
ya Dokta Kweka.
“Sikuwahi kufika katika
hoteli hiyo”
“Vicky alikuona ukitoka katika
mlango wa hoteli, ulikwenda kufanya nini?”
“Labda amenifananisha, sikuwa
mimi”
“Tulikuwa tunamtafuta mtu
aliyemuua Kweka. Bila shaka utakuwa ni wewe. Umemuua
kwa kisasi cha kuchukuliwa mke wako”
“Si kweli na pia sijui kama Kweka ameuawa”
“Sasa nakwambia kwamba Kweka
ameuawa na wewe utakuwa mtuhumiwa wetu namba mbili kwa sababu ulionekana katika
eneo la tukio”
Simon akawekwa ndani baada ya
alama zake za vidole kuchukuliwa.
Kwa upande mmoja alikuwa na
wasiwasi wa kukabiliwa na kesi nyingine ya mauaji na kwa upande mwingine alijiambia
hakukuwa na ushahidi kuwa yeye ndiye aliyemuua Kweka. Kuonekana katika eneo la
tukio la mauaji
hakumaanishi kwamba umeua, alijiambia.
Akakumbuka kwamba alipofika
pale hoteli alizifuta alama za vidole vyake kwenye kitasa cha mlango wa chumba
alichokuwemo Kweka na hivyo kuondoa ushahidi mwingine kuwa alifika mahali hapo.
Hata hivyo alimlaani Vicky
kwa kujua kuwa ndiye aliyemtaja baada ya yeye kukamatwa na kusuka mipango ya
kumpigia simu ili na yeye akamatwe.
Temba baada ya kumuweka ndani
Simon alichukua gari na kuelekea hospitali ya Muhimbili ilikokuwa maiti ya
Kweka ili achukue alama za vidole za marehemu.
Alikuwa na shaka sana na Simon. Alijiambia
upo uwezekano mkubwa kuwa Simon ndiye aliyemuua Kweka kwa sabubu ya kumchukulia
mke wake.
Alipofika hospitali ya
Muhimbili Temba alitaka apelekwe mochwari ili achukue alama za vidole za Kweka
kwa ajili ya uchunguzi wao. Alipelekwa mochwari na kufunguliwa sehemu iliyokuwa
imewekwa mwili wa Kweka.
Kwa mastaajabu makubwa, mwili
wa Kweka haukuonekana! Mhudumu wa mochwari alidhani mwili huo ulikuwa umewekwa
sehemu nyingine, akaanza kutafuta. Nusu saa baadaye ikagunduliwa kuwa mwili wa
Kweka haukuwemo mochari.
Ulikuwa umetoweka!
Kulikuwa na maiti tatu ambazo
zilichukuliwa na jamaa zao asubuhi ile. Kwa kushuku kwamba mwili wa Kweka
ulitolewa kwa makosa. Temba azunguka na gari katika sehemu zote zilikopelekwa
maiti hizo na kugundua kuwa maiti ya kweka haikuwa miongoni mwa maiti
zilizotolewa.
Akarudi kituoni kutafakari
suala la kupotea kwa maiti ya Kweka. Mara tu alipoketi, polisi mmoja aliingia
ofisini mwake na kumwambia.
“Afande kuna jambo la
kutatanisa”
“Jambo gani?”
“Yule mtu aliyeuawa jana
amekuja akiwa mzima, anataka mke wake atolewe!”
“Eti nini? Unamaanisha
Kweka?’
“Kweka ndiyo”
“Haiwezekani! Kweka amekufa
na nimeishuhudia maiti yake!”
“Yuko nje afande!”
“Mlete”
Polisi huyo alitoka. Baada ya dakika chache aliingia
akiwa amefuatana na Dokta Kweka.
Temba alimtolea macho ya
mshangao. Kweka alimpa mkono Temba ili kumsalimia. Temba akaukwepa.
“Wewe nani?” akamuuliza.
“Mimi Dokta Kweka”
“Natoka kuzimu!” Kweka
alijibu.
Uso wa Temba ulinywea,
akamtazama yule polisi aliyengia na daktari huyo.
“Nenda kamlete Vicky”
akamwambia.
Polisi huyo alitoka. Baada ya muda kidogo aliingia akiwa
na Vicky. Vicky alishituka alipomuona Kweka ndani ya ofisi hiyo.
“Huyu ndiye mke wako?” Temba
akamuuliza Kweka.
“Ndiye yeye”
Vicky alikuwa bado
akimshangaa Kweka.
“Mke wangu nimekufuata twende
zetu” Kweka akamwambia Vicky.
“Wewe si uliuawa?” Vicky
akamuuliza kwa mshangao.
Kweka alikenua midomo
akacheka. Akamshika mkono Vicky huku akimtazama Temba.
“Kuna kesi yoyote
inayomkabili?” akamuuliza.
“Kesi inahusu kuuawa kwako
wewe” Temba alimjibu.
“Sasa mimi niko hapa.
Mmeniona niko hai, bado kuna kesi tena?”
“Na maiti yako pia imetoweka
kule hospitali!”
“Kwa hiyo sidhani kama kuna kesi tena”
Temba akanyamaza kimya.
“Namchukua”
Kweka alitoka na Vicky huku
Temba na polisi mwenzake wakimkodolea macho.
Walipotoka, Temba alimtazama
yule polisi mwingine.
“Anasema anatoka kuzimu!”
“Ni maajabu ya mwaka.
Nimepata hofu sana”
Masaa mawili baadaye Simon
naye aliachiwa na kesi ikafutwa kimyakimya.
Mara tu Simon alipoachiwa
alikwenda New Africa kuliangalia gari
alilokuwa ameliacha asubuhi alipokamatwa. Akalikuta mahali pale pale
alipoliegesha. Alifungua mlango akaitazama ile bastola aliyokuwa ameificha
chini ya siti, akaiona ipo. Akajipakia na kuondoka.
Alikwenda nyumbani kwa James.
Wakati anafika James naye alikuwa anatoka na gari. Alipomuona Simon akashuka
kwenye gari.
“Vipi mbona hukutokea
asubuhi?” akamuuliza.
“Nilikamatwa na polisi,
nimeachiwa sasaa hivi” Simon alimjibu huku akishuka kwenye gari.
“Ulikamatwa kwa kosa gani?”
“Kwa mauaji ya Kweka. Tuingie ndani tuzungumze”
James alifunga mlango wa gari
yake akaingia nyumbani kwake huku Simon akimfuata nyuma. Wakati anapita
mlangoni alimwambia Simon.
“Karibu ndani”
Walikwenda kuketi sebuleni.
“Niambie imekuwaje?” James
akamuuliza kwa wasiwasi.
“Jana wakati natoka pale
hoteli baada ya kumuua Kweka nilimuona yule mke wangu Vicky akishuka kwenye
teksi, kumbe na yeye aliniona. Nafikiri baada ya yeye kukamatwa na polisi
alinitaja mimi”
“Kwanini akutaje wewe?”
“Alinitaja kwa kudhani
nilikuwa na kisasi na Kweka na hivyo polisi walihisi kwamba mimi ndiye
niliyemuua”
“Sasa walikupata wapi?”
“Walitumia mbinu. Walimwambia
Vicky anipigie simu kutaka nikutane naye New Africa Hotel. Nilipofika New Africa nikakamatwa”
“Na huyo Vicky ulikutana naye
hapo?”
“Ndiyo nilikutana naye.
Wakati tunazungumza ndio polisi wakatokea na kunikamata”
“Mlipofika kituo cha polisi
ikawaje?”
“Mimi nilikanusha kumuua
Kweka na pia nilikanusha kufika katika hoteli ya Suzy. Niliwekwa ndani tangu
asubuhi. Hii saa tisa ndio wakaniachia”
ITAENDELEA kesho, Usikose
No comments:
Post a Comment