HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU
ILIPOISHIA
Walipofika nyumbani kwa Mwana Alphonce alioneshwa chumba
atakachokuwa akikaa mpaka hapo atakapoondoka kurudi Dar es Salaam. Kilikuwa
chumba kipana kilichokuwa na kila kitu.
“Utakaa kwenye chumba hiki. Nafikiri kila kitu kimo. Kama kutakuwa
na kitu zaidi unahitaji utaniambia” Mwana limwambia Alphonce.
Alphonce alikuwa amefungua sanduku lake akitoa vitu vilivyokuwemo.
Mwana akamfungulia kabati.
“Kabati lina nafasi ya kutosha kuweka vitu vyako. Hakuna kitu
zaidi ya shuka na taulo”
Alphonce alianza kupanga vitu vyake kwenye kabati.
“Endelea kupanga, mimi niko sebuleni” Mwana akamwambia Alphonce na
kutoka.
Alphonce aliendelea kupanga nguo zake na vitu vyake vingine.
Alipomaliza alilifunga kabati na kutoka. Alikwenda sebuleni akaketi na Mwana.
“Naomba unipatie lile gazeti”
“Liko kwenye mkoba wangu” Mwana limwambia na kuuchukua mkoba wake
uliokuwa kando yake akaufungua na kulitoa gazeti hilo.
“Hili hapa”
Alimpa Alphonce ambaye alifungua ukurasa wa nne uliokuwa na zile
habari zilizomuhusu. Akazisoma tena.
SASA ENDELEA
“Zimekutia wasiwasi?”
“Hapana, ninashangaa huu upotoshaji wa habari zinyewe”
“Upotoshaji upi?”
“Hapa wanasema kwamba huyu kijana ameuawa kwa kisasi na si kwa
wizi”
“Ni kwa sababu polisi hawakupata ukweli”
“Wameegemea kwenye maelezo ya yule kijana aliyewambia kuwa
walikuwa wanatembea wakavamiwa na mtu wakati ukweli ni kwamba wote walikuwa ni
wezi. Walikuwa vijana watatu”
“Lakini ninaamini hakutakuwa na tatizo kwa upande wako,
hawatakupata”
“Mimi bado nitakuwa hapa Lagos kwa wiki nzima”
“Hata ingekuwa ni kwa mwezi mzima. Watu wanauawa kila siku katika
jiji hili. Hakuna anayekamatwa”
“Yaani jiji hili liko hivyo?”
“Ni majiji yote makubwa. Pale Johannasburg kila saa moja kunakuwa
na tukio la mauaji, haijambo hapa Lagos. Unataka uniambie Dar es Salaam hakuna
mauaji?”
“Mauaji yapo”
“Sasa…usidhani ni hapa tu. Miji inapokuwa mikubwa ina mengi. Mdogo
wangu aliuawa mbele yangu mwaka juzi kwa risasi. Waliomuua hawajapatikana hadi
leo!”
“Aliuawa kwa sababu gani?”
“Haikujulikana. Waliomuua walikimbia na gari lakini ilidaiwa
kwamba alikuwa akichukua mke wa mtu”
“Huyo mtu mwenye huyo mtu alifahamika?”
“Sasa la ajabu ni kwamba wakati polisi wanamfuatilia mtu huyo,
naye akauawa na watu wasiojulikana!”
“Kwa hiyo mauaji yanaonekana ni kitu cha kawaida hapa Lagos?”
“Kama nilivyokwambia ni katika majiji yote makubwa si Lagos peke
yake. Polisi wanadanganya tu kueleza kuwa wanamtauta muuaji, watu wakisahau na
habari inaisha”
Alphonce alitingishatingisha kichwa chake kumkubalia Mwana kabla
ya kumwambia.
“Ndiyo unataka nije niishi hapa?”
“Ndiyo. Unakuja kufanya kazi”
“Katika jiji hili la mauaji!”
“Umeanza kupata hofu. Ni wazi kuwa hutaweza kuishi mahali popote
katika dunia hii ya leo kwa sababu mauaji yapo kila mahali mpaka Marekani na
Ulaya. Lakini wanaouana wana visasi vyao ambavyo wewe havikuhusu”
“Nakumbuka siku moja Dar es Salaam wakati nikiwa mwanaunzi wa chuo
kikuu, mwanaunzi mwenzetu alipigwa risasi tatu na watu wawili waliokuwa
wamepanda pikipiki na hawakupatikana hadi leo”
“Hiyo ndiyo hali ya ulimwengu wa leo”
Wakati wanazungumza mtumishi wa ndani wa Mwana alipita akielekea
uani. Mwana alimuita.
“Nataka nikutambulishe kwa mgeni wetu” Mwana alimwambia na
kumuionesha Alphonce.
“Huyu mtu unayemuona ni mgeni wetu atakuwa hapa nyumbani kwa siku
kadhaa”
“Sawa. Nimemuona” Eda alijibu huku akimtazama Alphonce.
“Karibu sana” akamwambia.
“Asante” Alphonce alimjibu.
ITAENDELA
No comments:
Post a Comment