Sunday, February 12, 2017

HADITHI, ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU SEHEMU YA 31

HADITHI
 
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU
 
ILIPOISHIA
 
Saa saba mchana wakati Kweka anakula chakula, Mwana alimpigia simu.
 
“Vipi huko?” Alphonce akamuuliza.
 
“Nimefurahi. Madaktari wangu wameniambia yule mwanamke amezinduka na anazungumza” Sauti ya Mwana ikasikika kwenye simu.
 
“Wamekwambia anaendelea vizuri?”
 
“Anaendelea vizuri. Unadhani atahitajika kuwa katika uangalizi wa madaktari. Nina maana anatakiwa kuendelea kukaa hospitali”
 
“Madaktari wako wamesemaje?”
 
“Hawakutaka kuingilia kwa sababu kazi uliifanya wewe”
 
“Nitakuja kumuona halafu nitajua kama mnaweza kumruhusu”
 
“Nikupitie saa ngapi?”
 
“Nipitie saa tisa”
 
“Sawa. Nitakupitia muda huo”
 
SASA ENDELEA
 
Ilipofika saa tisa Mwana alifika pale hoteli akamchukua Kweka na kwenda naye hospitalini kwake.
 
Waliingia katika chumba alichokuwa amelazwa mwanamke huyo, wakamkuta akizungumza na muuguzi mmoja.
 
Muuguzi alipowaona wakiingia aliondoka na kuwaacha.
 
“Unajisikiaje?” Alphonce akamuuliza.
 
“Najisikia vizuri kidogo” Mwanamke huyo alijibu.
 
“Sehemu gani inakusumbua hadi sasa?”
 
“Nasikia maumivu kwenye miguu”
 
Alphonce aliitazama miguu yake. Miguu yake yote miwili ilikuwa imefungwa bendeji.
 
“Inauma kwenye majereha?”
 
“Ndiyo”
 
“Hebu kunja vidole vya miguu yote miwili”
 
Mwanamke alivikunja vidole vyake vya miguu.
 
“Vikunjue”
 
Akavikunjua.
 
“Maumivu yatapungua baadaye” Alphonce alimwambia.
 
“Unajua kama ulipata ajali?” Mwana akamuuliza.
 
“Ninajua. Kuna gari lilinogonga”
 
“Hilo gari baada ya kukugonga lilikimbia. Wasamaria wema ndio walikuleta hapa hospitali” Mwana alimdanganya ili kujitoa kwenye hatia.
 
“Nashukuru sana”
 
“Pia umepoteza mimba yako”
 
“Nimembiwa kuwa mimba yangu imetoka, lakini nashukuru mimi mwenyewe nimepona” Mwanamke huyo alisema.
 
Jibu hilo likamfariji Mwana. Akatabasamu.
 
“Una watoto?” akamuuliza.
 
“Ninaye mmoja”
 
“Una mume?”
 
“Tulishaachana, ninaishi peke yangu”
 
Mwana akahisi kuwa hakutakuwa na tatizo kubwa. Akamtazama Kweka.
 
“Unaonaje, anaweza kurudi nyumbani leo?”
 
“Mwache alale hadi kesho asubuhi” Kweka akamjibu.
 
Mwana akamtazama yule mwanamke.
 
“Dokta amesema kesho asubuhi ndio utarudi nyumbani”
 
“Sawa”
 
“Asante sana. Sisi tunaondoka, tutakuja kukuona baadaye”
 
“Nashukuru sana”
 
Mwana na Alphonce wakaondoka.
 
“Nikupeleke nyumbani ili ujue ninapoishi” Mwana akamwambia Alphonce walipokuwa nje ya hospitali.
 
“Sawa. Tunaweza kwenda”
 
Wakajipakia kwenye gari. Mwana akaliwasha gari na kuondoka.
 
“Alphonce kwanini usije kufanya kazi huku Nigeria?” Mwana akamuuliza Alphonce wakati gari ikiwa kwenye mwendo.
 
“Una maana niache kazi kwetu”
 
“Unaangalia maslahi yako, ukija huku utapata maslahi zaidi”
 
“Una hakika kwamba nitapata kazi huku Nigeria?”
 
“Nitakuajiri mimi kwenye hospitali yangu. Nina daktari mmoja tu ambaye ni bingwa wa upasuaji na hivi sasa yuko likizo”
 
“Ni suala linalofikirika”
 
“Fikiria, mimi niko tayari kukuajiri”
 
“Na utanilipa mshahara mzuri”
 
“Na nitakulipa kwa dola. Nimeuona utaalamu wako”
 
“Basi nipe muda nitafakari”
 
Pakapita ukimya wa sekunde kadhaa kabla ya Mwana kumuuliza Alphonce.
 
“Una mke na watoto”
 
Alphonce akatikisa kichwa.
 
“Sijaoa bado”
 
“Unasubiri nini?”
 
“Ni uamuzi tu, bado sijaamua kuoa”
 
“Nitakuozesha msichana wa Kinigeria”
 
“Utanitafutia mchumba huku huku?”
 
“Ndiyo”
 
“Unataka nihamie kabisa?”
 
“Si vibaya”
 
Alphonce akacheka.
 
Mwana alikuwa akiishi katika eneo maalumu ambalo huishi watu wenye pesa zao. Majumba yaliyokuwa katika eneo hilo yalikuwa ni yale ya kiahari na mahekalu yanayoshindana kwa ubora.
 
Mawaziri wa serikali, wafanyabiashara wakubwa na maafisa wa mashirika ya kimataia walikuwa ni miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.
 
Mwana alilielekeza gari kwenye geti la nyumba moja ya kifahari ya ghoroa moja. Gari hilo lilipokuwa karibu na geti hilo, lilifunguka na kuwa wazi. Gari likaingia ndani na kutokea kwenye ua mpana ulokuwa na kila kitu. Ulikuwa na sehemu ya taiz, sehemu ya bustani na sehemu ya barabara za gari linapoingia na kutoka.
 
Pia kulikuwa na banda kubwa lililoweza kuingia zaidi ya magari manne. Mwana aliliingiza gari kwenye banda hilo na kulisimamisha.
 
“Hapa ndio nyumbani kwangu, tushuke” Mwana alimwambia Alphone wakati akifungua mlango.
 
Alphone naye alifungua mlango. Wakashuka kwa pamoja. Mtumishi wa ndani alikuja kumpokea mkoba Mwana akatangulia nao ndani.
 
“Karibu bwana Alphonce, jisikie uko nyumbani” Mwana alimwambia Alphonce wakati wakitembea kuelekea kwenye jumba hilo.
 
Wakaingia kwenye sebule iliyokuwa imetulia.
 
“Karibu ukae” Mwana alimkaribisha Alphone huku akimuonesha safu za makochi.
 
Alphonce alikaa kwenye kochi mojawapo na Mwana akakaa. Aliuweka mguu wake juu ya mwingine, akamtazama Alphonce.

Itaendelea kesho usikose hapahapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment