Tanga, JESHI la Polisi Mkoani Tanga
limewakamata wahamiaji haramu 25 wenye asili ya Ethopia wakiwa wamefichwa
kwenye gari aina FUSO wakitokea Rombo
Mkoani Kilimanjaro wakisafirishwa kuelekea Tunduma.
Wahamiaji hao ambao pia walikuwemo wanawake watano walikutwa
wakiwa wamechoka kwa njaa huku baadhi yao wakilalamika kukaa muda mrefu kwenye
gari na kukosa huduma muhimu ikiwemo maji ya kunywa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa
Polisi Mkoani Tanga, Benedict Wakulyamba, amesema tukio hilo lilitokea juzi saa
4 usiku katika kizuizi cha polisi Mombo.
Amesema kwa sasa wanawashikilia pamoja na dereva wa gari hilo
na kondakta wake na mara baada ya uchunguzi kukamilika watapelekwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Katika tukio jengine jeshi la polisi limekamata silaha nne
aina ya Gobore Wilayani Kilindi ambazo zilikuwa zikitumika katika uhalifu.
Silaha hizo zimekamatwa wakati wa msako unaofanywa na jeshi
hilo baada ya taarifa za kuwepo kwa watu ambao wanasadikiwa kuwa majambazi
kuendesha vitendo vya kihalifu.
No comments:
Post a Comment