Sunday, February 19, 2017

HADITHI, ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU SEHEMU YA 35

HADITHI
 
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU
 
ILIPOISHIA
 
Mwana alilielekeza gari kwenye geti la nyumba moja ya kifahari ya ghoroa moja. Gari hilo lilipokuwa karibu na geti hilo, lilifunguka na kuwa wazi. Gari likaingia ndani na kutokea kwenye ua mpana ulokuwa na kila kitu. Ulikuwa na sehemu ya taiz, sehemu ya bustani na sehemu ya barabara za gari linapoingia na kutoka.
 
Pia kulikuwa na banda kubwa lililoweza kuingia zaidi ya magari manne. Mwana aliliingiza gari kwenye banda hilo na kulisimamisha.
 
“Hapa ndio nyumbani kwangu, tushuke” Mwana alimwambia Alphone wakati akifungua mlango.
 
Alphone naye alifungua mlango. Wakashuka kwa pamoja. Mtumishi wa ndani alikuja kumpokea mkoba Mwana akatangulia nao ndani.
 
“Karibu bwana Alphonce, jisikie uko nyumbani” Mwana alimwambia Alphonce wakati wakitembea kuelekea kwenye jumba hilo.
 
Wakaingia kwenye sebule iliyokuwa imetulia.
 
SASA ENDELEA
 
“Karibu ukae” Mwana alimkaribisha Alphone huku akimuonesha safu za makochi.
 
Alphonce alikaa kwenye kochi mojawapo na Mwana akakaa. Aliuweka mguu wake juu ya mwingine, akamtazama Alphonce.
 
“Ungependa kinywaji gani, cha baridi au moto?”
 
“Kama nataka kinywaji cha baridi utanipatia nini?”
 
“Sema ungependa nini, kinywaji kikali?”
 
“Hapana, kama kuna juisi ya matunda nipatie”
 
“Eda!” Mwana alimuita mtumishi wake. Eda alipofika alimwambia awapatie jagi la juisi na bilauli mbili.
 
Eda alipoondoka Alphonce akaizungushia macho nyumba ya Mwana na kukiri moyoni mwake kuwa ilipendeza. Alijiambia kama atajenga nyumba atatumia plani ya nyumba ile.
 
Eda aliwaletea chano kilichokuwa na jagi la juisi na bilauli mbili, akawamiminia juisi na kila mmoja kumpa bilauli yake.
 
Alphonce na Mwana walielekezeana bilauli wakafanya “chiaz” kabla ya kuzipeleka bilauli midomoni.
 
“Unatarajia kuondoka lini?” Mwana alimuuliza Alphonce mara tu alipoirudisha bilauli na kuiweka kwenye stuli ndogo ya kioo iliyokuwa ubavuni mwa kochi alilokaa.
 
“Baada ya wiki moja nitaondoka. Likizo yangu inakaribia kwisha”
 
“Lakini umelionaje jiji, linakufaa kwa kuishi?”
 
Alphonce akatingisha kichwa kuonesha kumkubalia.
 
“Linafaa”
 
“Kwa hiyo utakapoondoka nikutarajie lini tena”
 
“Tutakuwa tunawasiliana”
 
“Nina mpango pia wa kukutafutia nyumba na usafiri”
 
“Sawa”
 
Walizungumza kwa karibu masaa mawili kabla ya Mwana kumrudisha Alphonce hotelini. Alipomfikisha hotelini hapo Mwana alijiegesha kwenye siti na kulizima gari.
 
“Alphonce, nimefikiria kitu kimoja, kwanini unaharibu pesa kukaa katika chumba cha hoteli?” akamuuliza.
 
“Kumbe ningefanya nini?” Alphonce akamuuliza huku akimbetulia nyusi.
 
“Kwanini usikae nyumbani kwangu katika hizi siku zoko chache zilizobaki, ile nyumba iko tupu. Ninaishi na waanyakazi wangu tu”
 
Alphonce aliwaza kidogo kisha akamwambia.
 
“Acha tu niendelee kukaa hapa”
 
“Kwanini?”
 
“Kwa sababu nilishapanga kukaa hoteli, bajeti yangu inaniruhusu”
 
“Ndiyo, lakini mimi nimeshakuwa mwenyeji wako na tumesaidiana mambo muhimu. Ninachukulia kwamba tumeshakuwa marafiki”
 
“Ni kweli lakini nisingependa kukupa jukumu”
 
“Jukumu gani?”
 
“Mimi nikikaa kwako, tayari nitakuwa nimeshakupa jukumu”
 
“Ondoa wazo hilo Alphonce, twende ukakae nyumbani kwangu”
 
“Sawa. Kesho nitarudisha chumba”
 
Mwana alipojibiwa hivyo akaliwasha gari.
 
“Nitakufuata asubuhi”
 
“Sawa”
 
Alphonce akafungua mlango wa gari la Mwana na kushuka.
 
“Jioni njema” alimwambia Mwana kwenye dirisha.
 
“Pia na wewe” Mwana alimjibu na kutia gea. Alirudi kinyume nyume akaligeuza gari na kuondoka.
                                             ******** 
Alipoingia chumbani mwake Alphonce alikabiliwa na wazo moja tu la kuhamia Nigeria. Alijadiliana na nafsi yake kuhusu wazo hilo alilolipata kutoka kwa Mwana kwamba aende akafanye kazi nchini humo.
 
Kwa upande mmoja aliliona lilikuwa wazo zuri, kama kutakuwa na maslahi zaidi na mazingira mazuri ya kazi kama alivyoambiwa. Lakini kwa upande mwingine, kuacha kazi na kuhamia nchi nyingine kwa ahadi ya kuajiriwa huko, aliona ni kama kutia mkono gizani kwani hakuwa na uhakika hali ngekuwaje.
 
Alijiambia angehitaji kuwaza zaidi na kujishauri zaidi kabla ya kuwa na maamuzi ya kuhamia nchini humo.
 
Asubuhi kulipokucha, Mwana kama alivyomuahidi alimfuata. Alimkuta akifungua kinywa kwenye eneo la mkahawa la hoteli.
 
Mwana likuwa ameshika gazeti.
 
“Habari ya asubuhi?” Mwana alimsalimia Alphonce huku akiketi.
 
“Nzuri, habari ya nyumbani?”
 
“Nashukuru tumeamka salama. Nimekuja kukuonesha hili gazeti”
 
“Lina habari gani?”
 
Mwana alimfungulia ukurasa wa nne wa gazeti hilo ambao ulikuwa na habari ya yule kijana aliyeuawa na Alphonce kwa kuchomwa kisu cha moyo. Ukurasa huo pia ulikuwa na picha  ikionesha mwili wake ukiwa umelala chini katika eneo alilouawa.
 
“Ile habari wameiandika hapa” Mwana alimwambia Alphonce huku akimpa lile gazeti.
 
Alphonce alilichukua na kuanza kuisoma ile habari. Ilikuwa ni kama ile aliyoisikia kwenye televisheni jana yake lakini kulikuwa na maneno yaliyomtisha kwamba polisi wanamtafuta aliyemuua kijana huyo wakiamini kuwa alikuwa na kisasi naye.
 
Kijana mmoja ambaye Alphonce aliamini alikuwa miongoni mwa wezi wenzake aliwaeleza polisi kuwa walikuwa katika matembezi wakavamiwa na mtu mmoja ambaye alimpiga kisu mwenzake na kisha kutoroshwa na gari.
 
Hata hivyo alisema hakuwahi kuiona namba ya usajili ya gari hilo kwa saabu alikuwa anakimbia baada ya mwenzake kuuawa.
 
Kijana huyo aliendela kuwaeleza polisi kuwa akimuona mtu huyo anaweza kumtambua na anaamini kuwa ni mgeni wa jiji hilo.
 
Alphonce alipoisoma habari hiyo aligindua kuwa alikuwa amefanya kosa kutokwenda kuliripoti polisi tukio hilo na hivyo kuwapa mwanya polisi wa kubuni kuwa kijana huyo aliuawa kwa kisasi wakati alikuwa mwizi.
 
“Umeona kwamba polisi wanakutauta?” Mwana akamuuliza Alphonce.
 
“Lakini mimi sikumuua kwa kisasi. Huyu kijana pamoja na wenzake walitaka kunipora”
 
“Lakini polisi hawatakupata, utahamia kwangu” Mwana alimtuliza.
 
“Ngoja nirudishe chumba tuondoke”
 
“Nakusubiri kwenye gari”
 
“Sawa”
 
Alphonce alikuwa ameshamaliza alichokuwa anakula akainuka na kurudi chumbani kwake. Alichukua sanaduku lake na mkoba wake akatoka. Alikwenda mapokezi akalipa pesa alizokuwa akidaiwa na kukirudisha chumba hicho.
 
Alipotoka nje ya hoteli aliliona gari la Mwana akalifuata. Mwana likuwa ameketi ndani ya gari akashuka na kumpokea lile sanduku ambalo aliliweka katika siti ya nyuma.
 
Wakajipakia kwenye gari hilo na kuondoka. Wakati amekaa kwenye siti Alphonce alikuwa akiwaza kuhusu ile habari ya kutafutwa na polisi. Ilikuwa imemtia wasiwasi sana kwa kujua kuwa alikuwa amefanya kosa kutokwenda kuripoti polisi na kuwaeleza ukweli.
 
Akajiambia endapo atakamatwa huenda tatizo hilo likawa kubwa kuliko alivyokuwa akidhani hapo mwanzo. Kwa upande mwingine alimshukuru Mwana kwa kumzindua na kuonesha kumjali.
 
“Madaktari wamemruhusu yule mwanamke aende zake” Mwana alimwambia Alphonce wakati gari hilo likiwa katika mendo.
 
“Mpaka leo asubuhi alikuwa akiendelea vizuri?” Alphonce akamuuliza.
 
“Baada ya kumpima waliona alikuwa akiendelea vizuri”
 
“Kuna ndugu zake wowote waliomfuata?”
 
“Hakukuwa na ndugu yake yeyote aliyefika isipokuwa nilitoa gari na dereva apelekwe nyumbani kwake. Ameshapelekwa”
 
“Umeanya vizuri”
 
Walipofika nyumbani kwa Mwana Alphonce alioneshwa chumba atakachokuwa akikaa mpaka hapo atakapoondoka kurudi Dar es Salaam. Kilikuwa chumba kipana kilichokuwa na kila kitu.
 
“Utakaa kwenye chumba hiki. Nafikiri kila kitu kimo. Kama kutakuwa na kitu zaidi unahitaji utaniambia” Mwana limwambia Alphonce.
 
Alphonce alikuwa amefungua sanduku lake akitoa vitu vilivyokuwemo. Mwana akamfungulia kabati.

No comments:

Post a Comment