Tanga, MBUNGE wa jimbo la Tanga mjini,
Mussa Mbarouk (CUF) amesema anaunga mkono
vita ya kupambana na madawa ya kulevya ila ukamataji na utajaji wa
majina unatakiwa kufuata sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana
akizungumzia ukamatwaji wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mussa alisema
ionekanavyo ni kuuwa upinzani nchini.
Alisema kitendo cha jeshi la polisi kuzingira nyumbani kwake
amekitaja kuwa ni vitisho lengo lake ni kuwabadilisha Watanzania kifikra ili
CCM iendelee kutawala.
“Naunga mkono mapambano ya madawa ya kulevya kwa waingizaji
wauzaji na hata watumiaji, ila mifumo yake inakinzana na haki za binadamu”
alisema Mussa na kuongeza
“Katika jimbo langu nimeanza harakati za kuhakikisha biashara
ya madawa ya kulevya inatokomezwa na kuvunja vijiwe vyote vya watumiaji wa
mirungi na unga” alisema
Akizungumzia vijana kufanya kazi na kuacha kukaa
vijiweni Mbunge huyo alisema kuna fursa
nyingi za kufanya ikiwemo kuunda vikundi na kupata mikopo.
Alisema kuna baadhi ya vijana wamekuwa wakishinda vijiweni na
kushindia kahawa wakati fursa nyingi za kujipatia kipato zikiwepo na
kuwakumbusha kuwa wanaweza kuja wageni na kuzichukua.
Alisema ujio wa bomba la mafuta ni fursa nzuri kwa vijana
kuchangamka kwa kubuni miradi na kuunda vikundi kuweza kunufaika na mikopo
katika taasisi za fedha.
“Ujio wa bomba la mafuta ni fursa nzuri kwa vijana kubuni
aina ya miradi na kuunda vikundi, watakuja wageni na kuhodhi maeneo muhimu na
mwisho kujutia” alisema
Aliwataka vijana wa Tanga kutambua kuwa miaka mitano mbeleni
Tanga itakuwa Mkoa wa kibiashara jambo ambalo litawavutia watu wengi wa ndani
na nje ya nchi baada ya bomba la mafuta kukamilika.
Mwisho
Mbunge wa Tanga mjini, Mussa Mbarouk (CUF) akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuzungumzia vita ya madawa ya kulevya na ukamataji wake.
No comments:
Post a Comment