Thursday, February 9, 2017

ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU

HADITHI
 
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU
 
ILIPOISHIA
 
Kweka liendelea kushangaa jinsi msichana huyo alivyokuwa akimtambua. “Amejuaje kuwa natokea Dar es Salaam?” Akajiuliza.
 
Hakutaka kumficha kitu, akamwambia.
 
“Ndiyo natokea Dar es Salaam. Umejuaje?”
 
“Nimekisia tu. Na niliwahi kufika Dar es Salaam na nikaona watu wanazungumza kama wewe”
 
“Ulifika lini?”
 
“Miaka miwili imeshapita, nilikaa wiki mbili”
 
“Mimi hii ni mara ya kwanza kufika Lagos na sina mwenyeji”
 
“Unalionaje jiji letu?”
 
“Jiji ni zuri lakini kuna uwizi ambao uko waziwazi”
 
“Samahani” Mwana akamkatiza na kumuuliza.
 
“Nakirudishe pale hoteli”
 
“Ndiyo nirudishe”
 
SASA ENDELEA
 
Mwana alikuwa amefika katika barabara panda, akashika barabara ya upande wa kulia na kuongeza mwendo.
 
“Nimekuja kuitafuta familia ya babu yangu” Kweka akatamka ghafla.
 
“Familia ya babu yako?”
 
“Niliambiwa kuwa babu yangu aliyemzaa baba yangu alitokea huku”
 
“Baba yako na mama yako wako wapi?”
 
“Wamekufa nchini Tanzania. Hawakuwahi kutupa historia zao. Lakini tulichokuwa tunafahamu ni kuwa wazazi wetu walitokea Congo”
 
“Walitokeaje Congo wakati umesema babu yako alitoka Nigeria?”
 
“Taarifa kuwa babu yangu alitokea Nigeia niliipata nilipofika Congo kuiulizia familia yetu. Niliambiwa kuwa baba yake baba yangu alitoka Nigeria akaoa mwanamke wa kikongo na kumzaa baba yangu. Baba naye akaja Tanzania akaoa mwanamke wa Kitanzania na kutuzaa sisi, mimi na mwenzangu”
 
“Inaonekana babu yako aliondoka miaka mingi”
 
Niliambiwa alipokufa alikuwa na umri wa miaka mia moja”
 
‘Si rahisi kuipata familia yake. Kama umekuja ni kama umekuja kutalii tu na kuiona nchi aliyotoka babu yako”
 
“Inabidi nikubaliane na wewe kwa sababu sioni dalili ya kupata fununu yake yoyote”
 
“Ni miaka mingi sana na pengine tangu alipoondoka huku hakurudi tena”
 
“Inawezekana, wazee wa zamani ndivyo walivyokuwa, wakishafika sehemu wakioa ndio basi husahau kwao”
 
Mwana alilisimamisha gari kwenye eneo la kuegesha la hoteli.
 
“Nimekufikisha” akamwambia Kweka.
 
“Asante sana, nakutakia jioni njema”
 
Kweka alifungua mlango na kushuka.
 
“Kwaheri” akamwambia Mwana na kuelekea hoteli.
 
Mwana aliirudisha gari kinyumenyume na kuondoka.
 
Kweka aliingia hotelini akaingia chumbani mwake na kujipumzisha kitandani.
 
Alikuwa na wiki moja tangu alipowasili nchini humo kwa lengo la kuitafuta familia ya babu yake. Hata hivyo maelezo ya Mwana yalikuwa yamemkatisha tamaa. Akaona amalize wiki moja kisha aondoke kurudi Dar.
 
Wazo la yule mtu aliyemuua lilimnyima furaha. Aliona alikuwa ametenda kosa ingawa alikuwa akijihami. Aliamini kwamba kesi ile ingefika polisi ingemletea matatizo japokuwa ni yeye aliyetaka kuibiwa.
 
Kwa upande mwingine alimshukuru yule msichana aliyemsaidia kumuondoa mahali pale haraka, vinginevyo wangetokea watu na kuwaarifu polisi. Alijiambia pengine isingekuwa kesi ya kuibiwa, ingekuwa kesi ya mauaji na ni yeye ambaye angeshitakiwa.
                                     ************
Asubuhi kulipokucha Kweka alikwenda kwenye mkahawa wa hoteli akanywa chai. Baada ya hapo alibaki mkahawani kutazama taarifa za televisheni.
 
Ghafla akaisikia taarifa ya yule kijana aliyemuua kwa kumchoma kisu. Kijana hiyo alioneshwa akiwa amelala mahali pale pale alipoanguka.
 
Taarifa za kipolisi zikaeleza kuwa kijana huyo alikutwa mahali hapo akiwa na jeraha la kuchomwa na kitu chenye ncha kali sehemu za moyo wake. Na polisi walikuwa wakiendelea na uchunguzi kumtafuta mtu aliyesababisha tukio hilo.
 
Ilikuwa taarifa iliyomshitua Kweka. Akaondoka kwenye mkahawa huo na kurudi chumbani mwake. Wakati anakaa kwenye kitanda, alisikia kelele huko nje. Akanyanyuka na kwenda kwenye dirisha kuchungulia.
 
Aliona watu walikuwa wamekusanyika barabarani. Akona gari alilolidhania kuwa ni la Mwana limesimama pembeni mwa barabara. Kulikuwa na mwanamke aliyekuwa amelala mbele ya gari hilo akitapatapa huku damu zikimtoka sehemu za miguuni na midomoni.
 
Kweka akahisi kwamba yule mwanamke alikuwa amegongwa na gari hilo na ndio sababu ya watu kukusanyika. Mara akamuona Mwana akitoka kwenye gari na kwenda mbele ya gari hilo kumtazama mwanamke huyo.
 
Kweka akatoka mle chumbani na kwenda mahali lilipotokea tukio hilo. Alijipenyeza katika kundi la watu akamfuata Mwana aliyekuwa amechanganyikiwa.
 
“Kitu gani?” Kweka akamuuliza.
 
“Imetokea ajali, nimemgonga huyu mwanamke kwa bahati mbaya. Nilikuwa namkwepa muendesha pikipiki”
 
Kweka akamtazama yule mwanamke aliyekuwa akiendelea kutapatapa pale chini kisha akambeba.
 
“Fungua mlango tumuwahishe hospitali” akamwambia Mwana.
 
Mwana akafungua mlango haraka. Kweka alimlaza yule mwanamke kwenye siti kisha akafunga mlango. Alifungua mlango wa upande wa pili wa dereva akajipakia. Mwana naye aliingia garini akaliwasha gari na kuliondoa kwa kasi.
 
“Nashukuru umenisaidia, nilikuwa nimechanganyikiwa” Mwana akamwabia Kweka wakati anaendesha.
 
“Matukio ya aina ile yanachanganya akili lakini inatakiwa uwe makini na uchukue hatua za haraka haraka ili kuokoa maisha”
 
“Ni kweli. Nitampeleka kwenye hospitali yangu”
 
“Wewe una hospitali?”
 
“Nina hospitali yangu. Ilikuwa ni ya mume wangu, alipofariki nikabaki nayo mimi”
 
“Wewe ni daktari?’
 
“Hapana. Mume wangu ndiye aliyekuwa daktari”
 
“Hata mimi fani yangu ni ya udaktari”
 
“Daktari wa nini?”
 
“Mimi ni daktari bingwa wa upasuaji”
 
Mwana akamtazama Kweka usoni.
 
“Sikukutambua. Unafanya kazi aliyokuwa akifanya mume wangu”
 
“Hivi sasa niko kwenye likizo, ndio sababu nimekuja huku”
 
“Ninashukuru sana kwa kunifahamisha hilo”  
 
ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment