Friday, January 30, 2015

SOMA HABARI KUU ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO,TZ

Soma stori  zilizopewa uzito kwenye Magazeti ya leo Tanzania January 30, 2015, nimekuwekea hapa

roun
MTANZANIA
Taarifa ya mwaka ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ya hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu na mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2013, imebua wizi wa kutisha wa fedha za umma uliofanywa na taasisi hizo.
Hayo yalibainika jana wakati Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alipokuwa akiwasilisha ripoti ya kamati hiyo, ambapo alisema katika ripoti za ukaguzi kwa Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL), imebainika kuwa ililipa mabilioni ya fedha kwa ajili ya ndege iliyoikodi kutoka Shirika la Ndege la Wallis Trading Inc la China, ndege ambayo ni hewa kwa kuwa haipo nchini.
Hadi sasa Serikali imelipa dola za Marekani 26,115,428.75, (Sh bilioni 45.17) na sasa inadaiwa dola za Marekani 23,996,327.82 (Sh bilioni 41.51), ndege hiyo ilikuwa mbovu na ilifanya kazi nchini kwa miezi sita pekee badala ya miaka sita kama mkataba wa ubinafsishwaji ulivyotaka:-Zitto.
Taarifa hiyo ya PAC, ilibainisha pia kuwa katika ujenzi wa jengo la watu mashuhuri (VIP) katika Uwanja Ndege wa Kimatifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, kuna ufisadi wa takriban Sh bilioni tisa.
Ilisema pia jengo hilo lilianza kujengwa bila kibali cha Baraza la Mawaziri na kuwa thamani ya gharama za ujenzi wa jengo hilo hazijulikani kwa kuwa nyaraka muhimu hazipo.
Kwa upande wa Mamlaka ya Bandari (TPA), imebainika kutumia Sh bilioni 9.6 kwa ajili ya vikao vya wafanyakazi na mamilioni mengine kujilipa kwa ajili ya posho za safari bila kuwa na kibali kutoka serikalini.
Zitto alisema pia kamati yake imebaini kuwa misamaha ya kodi imezidi kuongezeka na kufikia Sh trilioni 1.8 mwaka 2014, huku zaidi ya Sh bilioni 80.45 za misamaha hiyo kwa mwaka zikitumika kwa njia zisizo halali.
NIPASHE
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), imepoteza Sh. bilioni sita katika ujenzi wa gati kwenye Ziwa Tanganyika kutokana na kila mkandarasi anayepewa kazi hiyo kuingia ‘mitini’ kabla ya kumaliza kazi hiyo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Madeni Kipande, alimweleza Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, wakati akielezea hali ya utendaji kazi wa mamlaka hiyo alipofanya ziara juzi.
Alisema kumekuwa na changamoto nyingi katika utekelezaji wa miradi ukiwamo ujenzi wa gati Ziwa Tanganyika na Bandari ya mwambani mkoani Tanga.
Kipande alisema mfano katika utekelezaji wa ujenzi wa bandari ya Mwambani Tanga, kampuni 34 zilinunua vitabu kwa ajili ya kuomba zabuni ya ujenzi wa bandari hiyo lakini hadi inafika mwisho wa kurudisha vitabu hakuna hata kampuni moja iliyorudisha.
Kuhusu wizi bandarini, aliiomba serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi kusaidia kuwabana mawakala wa mizigo bandarini kwa kutumia sheria iliyopo kwa kuwa wamekuwa mawakala wa wezi.
Alisema mawakala hao wamekuwa wakiwabambikizia bili wateja na kwamba kuna haja kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuweka bei zinazolingana ili wateja wasiwe wanabambikiziwa bili.
NIPASHE
Sakata la kupigwa na kudhalilishwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba na wafuasi wengine wa chama hicho, limeibua mapya, baada wabunge wa upinzani kuja juu wakitaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe wawajibike au Bunge liwawajibishe.
Wengine, ambao wabunge wanataka wawajibike ni Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Ernest Mangu, naibu wake (DIGP), Abdukrahman Kaniki, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa jeshi hilo, Paul Chagonja pamoja na wote waliohusika na kadhia hiyo.
Pia wametaka viongozi wengine wa polisi waliohusika ama kutoa amri au kutekeleza unyama huo wachukuliwe hatua za kisheria na jeshi hilo lifumuliwe na kuundwa upya.
Walisema hayo kwa nyakati tofauti wakati wakichangia bungeni mjadala kuhusu hoja iliyohusu jambo la dharura, iliyotolewa na Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia na kauli ya serikali, kuhusiana na yaliyotokea Januari 27, mwaka huu, Mbagala, jijini Dar es Salaam.
Katika mjadala huo, Waziri Chikawe pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, walipatwa na wakati mgumu wakijaribu ama kutoa hoja za kuzuia mjadala kuhusu suala hilo kufanyika bungeni au kuwatetea polisi na kumkandamiza Prof. Lipumba.
NIPASHE
Watu watatu wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kuhifadhi na kuuza sigara za magendo maeneo ya Mbagala jijini Dar es Salaam kwa lengo la kukwepa kulipa kodi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Siro, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Efeso Tweve, Omary Metson na Frank Mrema.
Alisema operesheni hiyo iliendeshwa na Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Biashara hiyo ya magendo ilianza kushamiri tangu mwaka 2012 kutokana na serikali kutoza kodi kubwa kwa bidhaa ya sigara na inakadiriwa kuwa asilimia nne ya sigara zote zinazouzwa Tanzania, ni za magendo.
Sigara hizi zinatengenezwa Tanzania kihalali kabisa kwa  ajili ya kuuzwa nchi za nje, lakini baadhi ya wafanyabiashara walioko kwenye mtandao wa bidhaa za magendo huzirudisha nchini bila kulipia kodi:-Siro.
Aidha, serikali hupoteza wastani wa Sh. bilioni 10 kila mwaka kama kodi kutokana na biashara hiyo ya magendo na kwamba kwa sasa kodi za Tanzania kwa sigara inafikia asilimia 36 ya bei za reja reja za bidhaa hiyo.
MWANANCHI
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda amevipa siku 14 viwanda vinavyozalisha bidhaa zilizo chini ya kiwango kuziondoa sokoni sambamba na kuujulisha umma namna watakavyoziharibu na kuziteketeza.
Waziri Dk Kigoda alitoa amri kwa kampuni tatu kuondoa bidhaa zake sokoni baada ya kugundulika kuzalishwa chini ya kiwango na kusisitiza kuchukua hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayekaidi agizo hilo.
Kupitia taarifa kwa umma iliyochapishwa jana, Waziri Kigoda alisema kampuni hizo zinatakiwa kutekeleza agizo hilo na kutoa taarifa ya utekelezaji kwa Shirika la Viwango la Taifa (TBS).
Kampuni zilizobainika kuzalisha bidhaa zilizo chini ya viwango ni pamoja na Kiwanda cha Devideic Group Ltd kinachotengeneza maji ya matunda aina ya Into, Ufresh Limited cha Tegeta kinachozalisha juisi aina ya Ufresh na Kampuni ya Kutengeneza Chumvi ya Sea Salt.
Ofisa Mdhibiti wa TBS, Deusdedit Paschal alisema chumvi inayozalishwa na kiwanda hicho ina madini joto ya miligramu 14.9 pekee wakati kiafya chumvi hutakiwa kuwa na miligramu 30-60.
MWANANCHI
Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) itaona muda wa uandikishaji wananchi katika Daftari la Wapigakura kwa ajili ya Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa hautoshi, atawasilisha suala hilo bungeni ili uongezwe.
Pinda alisema hayo bungeni mjini Dodoma jana katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu bungeni alipokuwa akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe aliyemtaka kueleza Serikali ina mpango gani kuhakikisha hakuna tatizo litakalotokea katika uandikishaji, hasa ikizingatiwa kuwa muda uliopo hautoshi na majaribio ya uandikishaji kwa BVR umeibua kasoro nyingi.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema: “Aliyoyasema Mbowe, Serikali haiwezi kuyapuuza hata kidogo na ni kweli mchakato huo umekuwa na matatizo kidogo hasa ya fedha na Serikali imekuwa ikipambana ili kuweza kufanikisha mchakato huo,” alisema Pinda.
Jana, Mbowe alisema majaribio ya uandikishaji wa kutumia mashine za kielektroniki za BVR katika majimbo ya Kawe, Wilaya ya Mlele na Kilombero yameibuka na changamoto mbalimbali na huku nchi ikitakiwa kuandikisha wapigakura zaidi ya milioni 24 na kuhoji kuhusu muda uliopangwa wa uandikishaji, hasa ikizingatiwa kuwa zimebaki siku 90 kufikia kwenye kura ya maoni huku mashine moja ikiwa na uwezo wa kuandikisha watu 22 kwa siku.
MWANANCHI
Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia mwalimu mmoja wa shule ya sekondari kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa kidato cha tatu na kumuumiza sehemu za siri.
Kamanda Koka Moita alisema mwalimu huyo alimwita mwanafunzi huyo katika chumba hicho na kuanza kumtomasa mwilini na baadaye alimvua nguo kwa nguvu, kisha kumuingilia.
Alisema kutokana na maumivu aliyoyapata alipelekwa Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi kwa matibabu. Kamanda Moita alisema mtuhumiwa baada ya kutenda kosa hilo alikamatwa.
JAMBOLEO
Watu wasiojulika wamevamia ofisi ya muhasibu katika shule ya St.Christina  ya Jimbo katoliki Tanga  iliyopo kata ya Maweni na kuiba shilingi milioni 126 kisha kuichoma ofisi hiyo kwa lengo la kupoteza ushahidi.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo,kaimu kamanda wa Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki alisema miongoni mwa fedha zilizoibwa ni karo za wanafunzi ambapo hadi sasa jeshi la polisi linamshikilia mlinzi na wenzake watano ambao wanatiliwa shaka.
Ndaki alisema upelelezi unaendelea kufanyika ili kuwabaini wahusika wa tukio hilo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia,www.tangakumekucha.blogspot.com

No comments:

Post a Comment