Friday, January 30, 2015

YALIYONIKUTA TANGA (8)

HADITHI
 
YALIYONIKUTA TANGA (8)
 
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
 
Nikairudisha ile simu mfukoni. Wakati nairudisha ilikuwa kama ninaizima akili yangu kwani hapo hapo sikujielewa tena. Sikujua kama nilipotewa na fahamu au nilipitiwa na usingizi wa ghafla. Sikuweza kujua.
 
Nilipozinduka nilijiona nimechoka, kitu ambacho kilinipa dalili kuwa nililala kwa muda mrefu pale kwenye kochi. Nikatazama saa yangu na kuona ilikuwa saa tisa usiku. Nikataharuki. Mwenyeji wangu hakuwepo. Nilikuwa bado niko peke yangu.
 
Nikajiuliza Maimuna alikuwa amekwenda wapi tangu muda ule. Nikanyanyuka na kuanza kumtafuta mwenyeji wangu. Niliingia ukumbini nikaita “Maimuna!”
 
Lakini sikupata jibu. Nikasukuma mlango wa chumba cha kwanza ambao ulikuwa wazi. Nikachungulia ndani. Chumba kilikuwa kitupu lakini kulikuwa na boksi kubwa lililowekwa nyuma ya mlango.
 
Nilichungulia ndani ya lile boksi nikaona kitu kilichonishitua. Nikaingia mle chumbani na kutazama vizuri. Ndani ya lile boksi niliona kichwa cha binaadamu, tena kilikuwa kichwa cha Sajenti Erick!
 
SASA ENDELEA
 
Kwa kweli nilipatwa na mshituko mkubwa. Vile ambavyo nilitoka usingizini nilijihisi kama nilikuwa kwenye ndoto ya kutisha. Kwa kutoamini macho yangu nilikitazama kile kichwa tena na tena. Akili yangu ilinithibitishia kuwa sikuwa kwenye ndoto na nilichokiona ni kichwa cha binaadamu na ni cha Sajenti Erick!
 
Nikawa najiuliza Sajenti Erick alichinjwa muda gani na alichinjwa na nani na kwanini kichwa chake kipo pale? Nikakumbuka kwamba nilipigiwa simu na kachero mwenzangu aliyenieleza kuhusu kutoonekana kazini kwa Sajenti Erick mchana kutwa wa siku ile.
 
Kile kichwa kwa jinsi kilivyoonekana hakikuchinjwa muda mrefu. Jeraha lake lilikuwa bado bichi na lilikuwa linavuja damu. Macho ya Sajenti Erick yalikuwa wazi kuonesha kuwa wakati anachinjwa alikuwa ameshituka.
 
Akili ya kupelelezi ikaanza kunijia. Nikazungusha macho yangu kwenye kile chumba. Sikuona mahali popote palipokuwa na damu, hali iliyoonesha kuwa Sajenti Erick hakuchunjwa mle chumbani.
 
Wakati nayarudisha macho yangu kwenye lile boksi nikaona magazeti kwenye pembe moja ya kile chumba. Nikaenda kuyatazama. Yalikuwa magazeti mawili yaliyowekwa pamoja. Juu ya magazeti hayo kulikuwa na kete tatu ambazo nilishuku zilikuwa kete za kokeni.
 
Nilizishika na kuzinusa. Kwa vile nilikuwa na uzoefu na unga huo haramu niligundua harufu yake. Ilikuwa ni kokeni. Nikaziweka kando. Sasa nilishika yale magazeti. Nilianza kuangalia mojawapo. Kwenye ukurasa wa mbele kulikuwa na habari ya ajuza (kikongwe) aliyekamatwa Tanga na kete za madawa ya kulevya.
 
Picha yake ilikuwa imechapwa. Nilipoitazama nikagundua ilikuwa ni ya yule mwanamke tuliyemkamata siku ile mimi na Sajenti Erick. Kumbe habari zake zilichapwa kwenye gazeti. Nikatazama tarehe ya lile gazeti nikaona ni la siku za nyuma.
 
Nikashika lile gazeti jingine. Katika ukurasa wake wa mbele kulikuwa na habari iliyohusu kifo cha yule kikongwe ambacho kilitokea katika mahabusi ya polisi.
 
Mpaka muda ule nilikuwa sijaelewa kitu. Nilikuwa nikijiuliza mengi ambayo hayakuwa na majibu. Wakati naliweka lile gazeti nikaona kitone cha damu kikidondoka kwenye kiganja changu. Nikashituka na kutazama juu.
 
Huko juu niliona kitu cha kushitusha. Niliuona mwili wa Sajenti Erick usio na kichwa ukiwa umening’inizwa kwenye miti iliyopaulia nyumba! Lile jeraha la kwenye shingo ndilo lililotonesha tone la damu  lililotua kwenye kiganja changu.
 
Mwili ule uliunda picha ya kutisha sana hasa kwa vile mtu mwenyewe nilikuwa namfahamu. Ujasiri wa kipolisi niliokuwa nimebaki nao uliniishia pale pale. Kama nisingekuwa makini ningekurupuka na kutoka mbio kwani hisia zangu zilishanusa hali ya hatari.
 
Nilijua kuwa hata mimi maisha yangu yalikuwa hatarini. Mahali nilipoingia palikuwa sipo!. Nikainua hatua ili nitoke katika kile chumba. Baada ya kupiga hatua mbili nilikanyaga mahali palipotitia! Nikajiona natumbukia chini.
 
Lilikuwa shimo la urefu wa kama futi nne. Miguu yangu ilipotua chini nikaona kitu kinanizongazonga kwenye miguu kikinipandia juu. Nikajaribu kukishika. Nikaona nimeshika kichwa cha nyoka!
 
“Yesu wangu!” nilishituka na kukivuta juu. Haikuvutika kwani sehemu yake ya mkia ilikuwa imenizonga kwenye mguu. Nilitaka kuwania kupanda juu ya lile shimo nitoke  lakini nilijiambia nikikiacha kile kichwa nyoka yule atanigonga.
 
Nikakipeleka kichwa hicho chini ya mguu mwingine kisha nikakikanyaga kwa kupiga mguu wangu chini. Kile kichwa kilipasuka. Ndipo nilipoweza kutoka kwenye lile shimo. Nilikuwa nahema kama niliyekuwa nafukuzwa.
 
Nilipotoka tu kwenye shimo hilo nilikwenda ukumbini nikaelekea kwenye mlango wa nje. Nilipoushika ili niufungue nikaona ulifungwa kwa nje. Mlango haukufunguka!
 
Nikasikia sauti za watu waliokuwa wakizungumza huko nje. Sauti ya mwanaume na mwanamke. Zilikuwa zikisikika kwa mbali lakini zilikuwa zikikaribia kwenye ule mlango. Nikajua ni watu  wanakuja.
 
Nikatega masikio kuwasikiliza.
 
“Sasa mama yuko wapi?” Ilikuwa sauti ya kiume iliyouliza.
 
“Mama yuko uani, anachimba kaburi kabisa” Sauti iliyojibu niliitambua, ilikuwa ni ya yule msichana aliyenikaribisha mle ndani.
 
“Na huyo polisi mwingine aliyewabambikia kesi yuko wapi?” Ile sauti ya kiume ikauliza tena.
 
“Nilimuacha ukumbini amelala, sijui kama atakuwa ameamka”
 
“Sasa acha tumshughulikie na yeye kama mwenzake”
 
“Mama yangu, nimekwisha!” nikajiambia niliposikia maneno hayo. Kumbe tatizo lilikuwa ni ile kesi tuliyombambikia yule mwanamke.
 
Sasa akili yangu ilitanzuka. Nilimkumbuka yule msichana. Alikuwa ndiye yule aliyekuwa na yule mwanamke kwenye ile nyumba tulipokwenda kuwakamata. Yule msichana alikimbia, tukamshikilia mama yake peke yake.
 
Kwa hofu kwamba ningeuawa kama alivyouawa Sajenti Erick, nilikimbilia kwenye mlango wa uani. Niliukuta mlango upo wazi, nikatoka uani ambako kulikuwa kiza lakini kulikuwa na mbalamwezi.
 
Kwenye pembe moja ya ua huo nilimuona bibi mmoja ameshika shepe akichimba shimo. Nilipomuona tu nikakumbuka yale maneno ya yule msichana niliyemsikia akisema “Mama yuko uani, anachimba kaburi kabisa”
 
Nikajiuliza lilikuwa kaburi langu au ni la Sajenti Erick? Wakati namtazama yule bibi nikamkumbuka. Alikuwa ni yule mwanamke tuliyemkamata na kumbambikia kesi ya kumkuta na madawa ya kulevya.
 
Jambo ambalo lilinishangaza ni kuwa mwanamke huyo alikufa akiwa mahabusi lakini muda ule nilimuona akiwa hai tena akionekana akiwa na nguvu za kutosha.
 
 Kitu ambacho kilikuwa cha ajabu zaidi ni kuwa bibi huyo alikuwa uchi wa mnyama na mwili wake ulikuwa umejaa manyoya meupe marefu. Nikaiona miguu yake, ilikuwa na kwato kama miguu ya punda!
 
Je nini kitatokea? Usikose kuendelea na hadithi hii kesho.
 Na usisite kutembelea blog hii kila wakati kwa habari nyingi nzuri na za kusisimua, ni tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment