Tuesday, January 27, 2015

VIONGOZI WA SERIKALI NA MITAA NGUVUMALI WAFUNDWA KUHUSU MAZINGIRA



TANGAKUMEKUCHABLOG
Tanga, MEYA wa jiji la Tanga, Omar Guledi, ametoa agizo kwa mabalozi wa nyumba  kumi na wenyeviti wa Serikali za mitaa kuwahamasisha wananchi kuweka mazingira ya usafi maeneo yao na atakaekaidi achukuliwe hatua za kisheria.
Akizindua mradi wa utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa kata ya Nguvumali na kushirikisha viongozi wa kata, Serikali za mitaa na viongozi wa dini leo, Gulledi alisema magonjwa ya miripuko na homa za mara kwa mara hazitoisha hadi jamii yenyewe itakapobadilika juu ya usafi wa  mazingira.
Alisema kufuatia kukaribia kwa msimu wa mvua ni wajibu wa kila kaya kuweka mazingira ya usafi katika maeneo yao ikiwa na pamoja na kuifanyia usafi mifereji iliyoziba ili kuwa rahisi mvua inaponyesha maji kutembea.
“Kwanza niipongeze Asasi ya Nguvumali commity development of invironment kwa kubuni jambo hili ambalo liko na faida ya kila mtu----mazingira yetu bado hayaridhishi na kuna kitisho cha mvua kubwa mbele yetu” alisema na kuongeza
‘Tumesikia kutoka kwa wataalamu wetu kuwa kuna mvua kubwa zinatarajia kunyesha na kama hatutaweka maeneo yetu katika usafi tutajazana mahospitalini kwa kuugua magonjwa ya miripuko” alisema Gulledi
Alisema ili kuweza kulifanikisha zoezi hilo ni wajibu wa viongozi wa dini na Serikali kuielimisha jamii kuweka mazingira ya usafi na yoyote ambaye atakuwa kikwazo awajibishwe kwa mujibu wa taratibu na sheria.
Kwa upande wake, Katibu wa Asasi ya Nguvumali Commity Development of Enviromment (NCDE), Frank Mgunda, alisema kuongezeka  vitendo vya uharibifu wa mazingira katika vyanzo vya maji na uchimbaji wa madini katika misitu.
Alisema Asasi hiyo itafanya kampeni ya nyumba kwa nyumba kutoa elimu ya mazingira kwa kuanzia mjini hadi vijijini kabla ya msimu wa mvua kuanza kunyesha ikiwa na pamoja na vijiji vinavyoishi kandokando ya vyanzo vya maji na misitu.
“Sisi tumedhamiria hasa kutoa elimu ya mazingira kwani kama yanavyonekana bado hayaridhishi na tuko katika hatari ya kukumbwa ukame miaka ya mbele na maeneo yetu kuwa jangwa baada ya kukithiri ukataji wa miti na uchimbaji wa madini holela .
Alisema elimu hiyo itakuwa ya kila kaya pamoja na kupita katika shule za msingi na sekondari lengo likiwa ni kuhakikisha mazingira yetu yanakuwa katika hali ya kuridhisha.
                                                 Mwisho

No comments:

Post a Comment