Thursday, January 29, 2015

WAGANGA WAKUU WA HOSPITALI ZA WILAYA WAPEWA SOMO



Kumekucha blog
Tanga,WAKURUGENZI na Waganga wakuu wa hospitali za Wilaya Mkoani Tanga, wametakiwa kupita kila kijiji na kitongoji kutoa elimu ya  kujiunga na mfuko wa bima ya afya ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo iliyojiwekea.
Akifungua kikao cha kujadili mpango wa mfuko wa Afya ya jamii na kusaini mkataba wa uhamasishaji wa CHF kwa Wilaya ya Lushoto na Muheza leo, Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Salim Mohammed Chima alisema elimu ya mfuko wa afya ya jamii inahitajika na kuwataka viongozi wenye dhamana kuacha  kujifungia maofisini.
Alisema viongozi wengi wamekuwa wakishindwa kutekeleza wajibu wao wakiwemo watu wenye dhamana kushindwa  kuhamasisha jamii kujiunga na mifuko wa bima ya afya ya jamii.
“Leo nawafungulia kikao chenu wenyewe cha kujadili na kuweka mikakati ya jamii kujiunga na mfuko wa afya ya jamii---baada ya hapa kila mmoja ahakikishe anatimiza wajibu wake” alisema Chima na kuongeza
“Tumekuwa tukikemea tabia ya wakuu wa idara na viongozi wenye dhamana kujifungia maofisini na kushindwa kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa mikataba ya utumishi wa umma” alisema
Alisema tabia ya viongozi kujifungia maofisini na kuacha kutekeleza wajibu wao ataikomesha ikiwemo utoro   pamoja na muda wa kuingia na kutoka kazini na hivyo kutoa agizo la kila mmoja kujua wajibu wake katika kazi.
Awali akizungumza katika kikao hicho, Mganga mkuu wa Mkoa, Asha Mahita, alipinga vikali ukosefu wa madawa katika hospitali zake na kuwabebesha mzigo waganga wa hospitali za Wilaya kwa uzembe wa kuacha kuagizia dawa.
Alisema malalamiko yanayotoka kwa wananchi juu ya ukosefu wa madawa ni uzembe wa waganga wakuu wa hospitali na hivyo kutoa wito kwa kila mmoja kuhakikisha kituo chake kinakuwa na dawa za kutosha ili kuondosha malalamiko kutoka kwa wananchi.
“Hakuna ukosefu wa madawa hospitalini na ikotokea ni waganga wakuu wa hospitali kufanya uzembe wa kuacha kuagizia-----dawa zipo za kutosha na hili nitalishughulikia mimi mwenyewe” alisema na kuongeza
“Tena natoa wito kwa wananchi popote katika mkoa huu mgonjwa aendapo hospitali na kuelezwa kuwa hakuna dawa awasiliane na ofisi yangu au mimi mwenyewe nitalivalia njuga ” alisema Mahita
Kwa kauli hiyo, Mahita aliwataka waganga wakuu wa hospitali za Wilaya kuhakikisha vituo vyao havipungukiwi na madawa na kudai kuwa hakuna upungufu huo na yoyote ambaye atafanya uzembe atamchukulia hatua.
                                                Mwisho

No comments:

Post a Comment