HADITHI
YALIYONIKUTA TANGA (14)
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
Baada ya kumaliza maelezo yake
ambayo yaliwashangaza maafisa hao, kamanda wa polisi akataka na mimi nieleze
kilichotokea.
“Kwanza ulifikaje katika eneo hilo
na ulikuwa na Sajenti Erick au ulikuwa peke yako?” akaniuliza.
“Nilikwenda peke yangu” nilimjibu.
“Kufuata nini?”
Niliona kama nitauma uma maneno
nitajikuta nikiwekwa ndani, jambo la msingi ni kueleza ukweli wote.
“Kuna msichana niliwasiliana naye
kwenye simu akataka nimfuate katika eneo hilo”
“Ni nani?”
“Wakati tunawasiliana nilikuwa
simjui lakini baadaye niligundua alikuwa ni yule msichana ambaye mama yake
tulimshitaki kwa kukutwa na kete za madawa ya kulevya na mama mwenyewe akafia
mahabusi”
“Umesema wakati mnawasiliana ulikuwa
humjui,?”
“Nilikuwa simjui”
“Uliwasiliana vipi na mtu ambaye
ulikuwa humjui?”
SASA ENDELEA.
Swali hilo lilinifanya nieleze
ukweli wa tukio zima la kuwasiliana na Maimuna. Nilianzia pale alipokosea namba
akanitumia meseji. Kamanda baada ya kunisikiliza aliniuliza.
“Kwa hiyo ulipokuwa unakwenda
kuonana naye ulikuwa na madhumuni gani?”
“Nilikuwa nataka tuwe marafiki, si
unajua afande mimi sina mke”
Nilipojibu hivyo Kamanda wa polisi
akamtazama Afisa upelelezi kisha akaendelea kunihoji.
“Enhe, ulipofika hapo mahali
alipokwambia mkutane nini kilitokea”
“Nilipofika pale sikumkuta,
nikampigia simu kumuuliza yuko wapi”
“Ndiyo”
“Akanijibu kwamba yuko nyumbani kwao
hivyo nimfuate na akanielekeza njia ya kufika nyumbani kwao”
“Ukaenda?”
“Nikaenda. Njia yenyewe ni ya kwenye
mapori. Mahali kwenyewe kuna nyumba moja moja na kuko giza”
“Ulipofika?”
“Nilikutana naye njiani. Akanipeleka
kwenye hiyo nyumba. Tuliingia ndani akanikaribisha ukumbini halafu yeye
aliondoka akaniambia nimsubiri. Lakini kuna kitu kimoja nataka kueleza”
“Eleza”
“Yule msichana nilimgundua kuwa ni
yule ambaye mama yake alishitakiwa kwa kukutwa na madawa ya kulevya hivi
karibuni akafia mahabusi. Nadhani unakumbuka afande”
“Nakumbuka na niliambiwa alikuwa na
binti yake ambaye aliwatoroka” Kamanda alimwambia.
“Basi huyo binti ndiye huyo msichana
mwenyewe”
“Kwa hiyo hakushituka kukuona”
“Hakushituka”
“Na wewe hukumuuliza kitu?”
“Wakati kumbukumbu zinanijia kujua
ni yeye alikuwa ameshaondoka na kuniacha peke yangu pale ukumbini ambako
aliniambia nimsubiri”
“Alikwambia anakwenda wapi?”
“Hakuniambia. Basi pale pale nilipitiwa
na usingizi wa ghafla. Nilipozinduka ilikuwa saa tisa usiku. Yule msichana
sikumuona…” nikaendelea kueleza kilichotokea baada ya hapo.
Kile kisa kiliwafanya maafisa hao wa
polisi watazamane kwa mshangao.
“Una maana yule mwanamke aliyekufa
ulimkuta akiwa mzima akichimba kaburi?” Afisa upelelezi ndiye aliyeniuliza.
“Ndiyo. Mimi nilishangaa sana
kumuona” nikamjibu.
“Umetuambia kwamba watu hao ni
majini?” Kamanda akauliza.
“Ni majini. Hata wenzangu waliokuja
wameona kuwa ni majini”
“Hivi majini ni imani tu au ni
viumbe kweli?”
“Kwa tukio hili mimi nimethibitisha
kwamba majini si imani, wapo!”
“Kwa hiyo majini ndio wamemchinja
Erick?’
“Ndio. Nafikiri ni kwa kisasi cha
ile kesi kwa sababu yeye na mimi ndio tuliomkamata yule mwanamke”
“Kwa hiyo walikuwa wanataka
kukuchinja na wewe?”
“Ndiyo”
“Kwa vile kuna tukio la mauaji ya
polisi na kiserikali hatuamini kuwepo majini, tutawachukulia kuwa hao ni watu
na inabidi tukio zima lithibitishwe” Kamanda wa polisi akaniambia kisha
akamtazama Afisa upelelezi.
“Itabidi tufike katika eneo hilo la
tukio, tupige picha pamoja na kuchukua maelezo kwa watu wa karibu na eneo hilo”
Afisa upelelezi akamwambia kamanda.
“Sawa, itabidi tufike”
“Kuna mtu mmoja tumekuja naye kwa
ajili ya kuandikisha maelezo” Yule inspekta niliyekuwa naye akasema.
“Ni nani?” Kamanda akamuuliza.
“Ni mwananchi tu mkazi wa jirani na
mahali palipotokea hilo tukio na ndiye aliyetupigia simu kutujulisha kuwa kuna
polisi waliolala juu ya makaburi”
“Hebu mlete hapa”
Inspekta alitoka na baada ya muda
kidogo alirudi akiwa na mtu huyo.
Aliwasalimia wale maafande kwa uoga.
“Karibu sana” Kamanda alimwambia ili
kumtoa hofu.
“Asante” Mtu huyo alijibu.
“Hebu tueleze ulichokiona huko
Magomeni hadi ukapiga simu polisi” Kamanda alimwambia.
“Niliona polisi wamelala juu ya
makaburi saa kumi na mbili asubuhi wakati nakwenda shamba, ndio nikapiga simu”
“Hao polisi walikuwa wamelalaje?”
Kamanda alimuuliza.
“Walikuwa wamelala usingizi kabisa
na walikuwa na bunduki”
“Hapo mahali ulipowaona palikuwa na
nyumba?”
“Hapana, lile ni eneo la makaburi
tu”
Kamanda wa polisi akanitazama kabla
ya kuuliza tena.
“Tumepata maelezo kwamba wale askari
waliingia kwenye nyumba, wakazirai na walipozinduka wakajiona wako juu ya
makaburi na ile nyumba hawakuiona tena”
“Inawezekana. Pale mahali panatokea
miujiza mara kwa mara. Inasemekana pana majini”
“Wewe uliwahi kuwaona?”
“Mimi sijawahi kuwaona lakini kuna
mtu aliwahi kuona mwanamke mrefu kama mnazi amesimama pale usiku”
“Alipomuona nini kilitokea?”
“Yule mtu alikimbia na aliuporudi
tena akiwa na wenzake, huyo mwanamke hawakumuona tena”
Je nini kitafuatia? Usikose
kuendelea na hadithi hii kesho.
Nakuhakikishia kukufikishia kila kinachonifikia mtu wangu kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment