Tuesday, May 12, 2015

WAUGUZI WATAKIWA KUTUNZA SIRI



Tangakumekuchablog
Tanga, MWENYEKITI wa kamati ya Afya Baraza la Madiwani halmashauri ya jiji la Tanga, Sele Boss Mustafa, amewataka wauguzi kuzingatia maadili ya kazi zao na kuacha kutoa siri za wagonjwa.
Akizungumza katika kongamano la shamrashamra kuelekea maadhimishoya siku ya wauguzi Duniani jana, Mustafa alisema kuna baadhi ya wauguzi wamekuwa wakivunja maadili ya kazi zao kwa kutoa siri za wagonjwa.
Alisema kufanya hivyo ni makosa na kutaka kuwepo kwa sheria kali kwa watu ambao wako na tabia kama hiyo na kudai kuwa mgonjwa huwa katika wakati mgumu mtaani mara baada ya kutoka hospitali.
“Kwa vile leo nimepata nafasi ya kuzungumza nanyi basi niwaase wale ambao wako na tabia ya kutoa siri za wagonjwa kuacha kufanya hivyo-----ni jambo baya na halifai kufanywa” alisema Mustafa
“Ili kuweza kudhibiti tabia hii ni lazima kuwepo kwa sheria ambazo zitamuwajibisha atakaetoa siri za mgonjwa kwani kuna baadhi ya wagonjwa hawatoi ushirikiano mzuri kwa wauguzi kwa hofu ya siri yake kutangazwa” alisema
Amewataka wauguzi hao kuwa na mshikamano na upendo pamoja na kuipenda kazi yao mbali ya changamoto nyingi ambazo wamekuwa wakikumbana nazo na kusema kuwa mchango wao kwa jamii unatambulika.
Akizungumz akatika kongamano hilo, Muuguzi wa jiji, Ester Kimweri amewataka wauguzi kuwa karibu na wagonjwa pamoja na kuwapa maneno mazuri kwa kuwafariji.
Alisema kuwa na utamaduni huo kutawafanya wagonjwa kupata faraja wakati wote wanapokuwepo hospitali jambo ambalo pia linaweza kuwa sababu ya kupona maradhi wanayokabiliana nayo.
“Wauguzi wenzangu tuendelee na mshikamano wetu kama kawaida pamoja na kutoa maneno mazuri kwa wagonjwa ili kuwapa faraja----huu ndio utamaduni wetu hasa sisi tuliopo hapa” alisema Kimweri
Amewataka wauguzi hao kufanya kazi kwa bidii kwani mbali ya kazi pia wako na fungu mbele ya Mungu kwani huduma zao ni njema na hivyo kuwataka kuendeleza kasi ya utoaji wa huduma.
                                                       Mwisho

No comments:

Post a Comment