Tuesday, May 12, 2015

SOMA MAKUBWA YALIYOJIRI MAGAZETINI LEO, MAY 12 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wananfunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo pia kiko na hosteli na kutoa kozi ya Kiingereza na Computer. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 7727246

NEWSHABARILEO
Mkazi wa kata ya Kisalala, Sumbawanga Lydia Shazi mwenye umri wa miaka 29 amejifungua watoto watatu wote wa kiume kwa siku tofauti katika hospitali mbili tofauti.
NIPASHE
Kampuni ya majisafi na majitaka Dar es salaam DAWASCO imetangaza zawadi ya 500,000 kwa yeyote atakayefanikiwa kufichua wezi wa maji katika maeneo yanayopita mabomba ya maji nchini.
 Mtendaji wa DAWASCO Cyprian Luhemela alisema Serikali imejipanga kushirikiana na wananchi na vyombo vya ulinzi likiwemo jeshi la Polisi kudhibiti hali hiyo inayoshamiri kila siku.
Alisema kumekuwepo na upoteaji mkubwa wa maji na kufanya wananchi wengi kukosa maji huku wachache wakinufaika.
Aliwahakikishia wananchi watakaotoa taarifa kwa DAWASCO kuhusu wizi wa maji kwamba zitakuwa siri kati ya mtoa taarifa na mpokeaji ili kulinda usalama wao.
Walisema kwa sasa wameamua kubadilisha sharia badala ya kuwashtaki wezi wa maji kwa kutumia sharia za kawaida sasa watawashtaki kama wahujumu uchumi.
MTANZANIA
Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na athari za mvua na mafuriko Dar es Salaam imeongezeka kutoka wanane na kufikia 12.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema jana kuwa kati ya watu hao mwanaume mmoja anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 35-38, mwili wake ulipoolewa baada ya kuzama kwenye tope katika mto Msimbazi, Magomeni.
Alisema mwili huo wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya uchunguzi na utambuzi.
Kamanda aliyataja majina ya watu wengine waliofariki dunia kuwa ni Valerians Eradius (13) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Kigogo ambaye alikufa Mei 10 mwaka huu baada ya kuangukiwa na ukuta.
Mwingine ni Gervas Shayo (28) mkazi wa Mbezi juu ambaye alikufa maji Mei 8 mwaka huu pamoja na mwanamke mmoja anayekadriwa kuwa na umri kati ya miaka 40 na 45 ambaye jina lake halikufahamika ambaye alikutwa katika bonde la Mkwajuni akiwa amefariki dunia.
Uzoefu unaonyesha kuwa jinsi maji yanavyoendelea kupungua kutokana na kupungua kwa mvua ndivyo madhara yanaonekana.
“Ninawaomba wananchi waendelee kutoa taarifa mapema wanapoona mwili wa mtu aliyekufa ili hatua zichukuliwe mara moja ikiwa ni pamoja na kuiondoa miili ya watu watakaokuwa wamekufa kutokana na athari za mvua inayoendelea kunyesha Dar es Salaam,” Kova.
MWANANCHI
Kada wa CCM Buni Ramole, amejipalia mkaa kutokana na kauli yake kwamba helikopta ya Mbunge wa Moshi Mjini (CHADEMA), Philemon Ndesamburo ni mbovu na ingeweza kumuua.
Ndesamburo kupitia kampuni ya mawakili ya Materu, amemtaka kada huyo kumlipa fidia ya Sh100 milioni na kumwomba radhi, akieleza kuwa kauli hiyo imemdhalilisha na kumvurugia biashara.
Kada huyo wa CCM, anadaiwa kukodi helikopta hiyo Aprili 18, mwaka huu na kwenda nayo katika mkutano wa hadhara wa chama hicho tawala uliofanyika katika viwanja vya Pasua mjini Moshi.
Hata hivyo, baada ya gazeti hili kuripoti tukio hilo, kada huyo alijitokeza hadharani na kukanusha kwamba helikopta hiyo hakuikodi kwa Ndesamburo bali kwa kampuni ya General Aviation Services (T) Limited.
Akizungumza na wanahabari katika ofisi za CCM wilaya ya Moshi Mjini, kada huyo alienda mbali na kudai kuwa helikopta hiyo aliyokuwa aitumie wakati wa kampeni Oktoba mwaka huu, ni mbovu na ingeweza kumuua.
“Nimechukua (chopa) makusudi ili kuwaonyesha wananchi kuwa Chopa si maendeleo. Watu wa Moshi wanafikiri Chopa ni maendeleo, Chopa kazi yake ni kuvuta watu na nimeshaiagiza itakuja, hii niliyokodisha awali ni mbovu kwanza ingeweza kuniua,” .
Hata hivyo, Ndesamburo kupitia mawakili wake hao, amemwandikia barua kada huyo akimtaka akanushe madai hayo, kwani ni ya kashfa na yanaathiri vibaya biashara yake ya Chopa.
”Kwa barua hii tunakutaka ndani ya siku saba, utangaze kwenye gazeti la Mwananchi kwamba taarifa yako ilikuwa si ya kweli na uombe radhi kwa mteja wetu na kumlipa fidia ya Sh100 Milioni,”imedai barua hiyo iliyoandikwa Mei 6 mwaka huu.
Mawakili hao wamedai kuwa wanayo maagizo ya kumfikisha kada huyo mahakamani kama hatatimiza masharti hayo na Ndesamburo atadai fidia kubwa zaidi ya Sh100 Milioni anazodai.
MWANANCHI
Siku moja baada ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kutoa tuhuma nzito dhidi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kuandikisha wapigakura wasio na sifa, tume hiyo imeibuka na kukanusha vikali.
Mkurugenzi wa ZEC, Salum Kassim Ali alisema jana kuwa hakuna majina ya marehemu yanayoendelea kutumika katika Daftari la Kudumu la Wapigakura hivyo CUF iache kuipotosha jamii.
Alikuwa anajibu madai ya Maalim Seif kuwa ZEC iliandikisha na kuruhusu wapigakura wenye umri chini ya miaka 18, walioandikishwa mara mbili, wasiokuwa wakazi na waliotumia ama majina au picha za watu wengine.
Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema madai hayo yamebainika katika utafiti uliofanywa na chama hicho ili kubaini hujuma zilizofanywa na SMZ na taasisi zake ambazo zinaweza kufanyika pia katika uchaguzi ujao.
Katika majibu yake, Ali alisema sheria na taratibu za uchaguzi kabla ya kupiga kura, yaani daftari huhakikiwa na majina kubandikwa hadharani katika vituo vya kupigia kura zilifanyika, hivyo kama kungekuwa na dosari, zilipaswa kuwekewa pingamizi.
Alisema sekretarieti ya ZEC inafanya kazi zake kwa maelekezo ya makamishna wake wakiwamo wawili kutoka CUF ambao wanafanya nao kazi kwa ushirikiano mkubwa na hayakuwahi kujitokeza malalamiko hayo.
Alisema kabla ya kuanza uandikishaji mwezi huu, ZEC ilikutana na wadau vyama vya siasa na kuwaeleza mambo manne yatakayofanyika ambayo ni uandikishwaji wa mwisho kwa wapiga kura, kuhakiki daftari la wapigakura, ikiwamo kuondoa waliokufa, kubadilisha taarifa na kuhamisha taarifa za wapigakura.
Alisema endapo kungekuwa na kasoro, makamishna hao wa CUF ndiyo wangekuwa wa mwanzo kulalamika kwa vile wapo jikoni na siyo viongozi wa chama wanaolalamika kwenye vyombo vya habari.
“Kama kweli ana ushahidi wa kile anachokizungumza, kwa nini haleti malalamiko yake ZEC badala yake analalamika kwenye vyombo vya habari?” alihoji.
Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, Mohamed Juma Ame alisema viongozi wenye dhamana wanapaswa kufanya utafiti na kupata ukweli kabla ya kutoa shutuma nzito ili wananchi wapate taarifa sahihi.
MWANANCHI
Mwili wa mtoto Imran Mwerangi aliyefariki dunia katika Hospitali ya Apollo, India alikokuwa amepelekwa kwa matibabu, unatarajiwa kuwasili leo.
Imran (6), ambaye alipooza mwili mzima na kupata mtindio wa ubongo baada ya kudungwa sindano katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alifariki dunia saa 11.45 alfajiri ya Mei 8.
Mtoto huyo ambaye alikuwa akipelekwa katika hospitali hiyo, kila baada ya miezi sita kwa ajili ya uchunguzi wa maendeleo ya afya yake kutokana na athari za sindani hiyo, alifikishwa huko Jumatano iliyopita baada ya hali ya afya yake kubadilika na kuvimba mwili mzima.
Alifariki dunia wakati madaktari wakihangaika kupata mishipa ya damu kwa ajili ya vipimo.
Baba wa marehemu, Iddy Mwerangi alisema jana kuwa taratibu za kuurudisha mwili wa marehemu kwa ajili ya mazishi zimefanywa na Ubalozi wa Tanzania nchini India na kwamba mwili huo unatarajiwa kuwasili.
Mwerangi ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), alisema wakati mwili wa marehemu ukitarajiwa kuwasili jioni, mama wa marehemu, Amina Machuro, atawasili mchana. “Baada ya mwili huo kuwasili nchini muda huo, moja kwa moja tutaanza safari kuelekea Mdaula, (Morogoro) kwa ajili ya mazishi,”  Mwerangi.
Imran alidungwa sindano hiyo, Julai 29, 2011 alipopelekwa Muhimbili kwa ajili ya matibabu ya upasuaji mdogo wa nyama zilizokuwa zimeota katika njia ya hewa, puani.
Baada ya kudungwa alitelekezwa ICU bila matibabu kwa zaidi ya miezi sita, akipumua kwa msaada wa mashine, huku ikimlazimu mama yake kumgeuzageuza kila baada ya saa mbili kwa kipindi chote hicho.
Licha ya kutokupata matibabu kwa muda wote huo, juhudi za wazazi wake kuomba rufaa ili apelekwe nje kwa uchunguzi zaidi hazikuzaa matunda hadi gazeti hili lilipoibua taarifa za mkasa wa mtoto huyo Februari 2012 na kuulazimu uongozi wa hospitali hiyo kuunda jopo la madaktari bingwa kuchunguza tukio hilo.
Baada ya ripoti ya uchunguzi huo, ndipo mtoto huyo aliposafirishwa kwenda kutibiwa India.
Aliruhusiwa kurejea nyumbani baada ya madaktari kuridhishwa na maendeleo ya afya yake, akitakiwa kurudi Appolo kila baada ya miezi sita kwa ajili ya uchunguzi.
MWANANCHI
Askofu Mkuu wa Kanisa la General Mission Center Limited (GMCL) la jijini hapa, Nabii David Mpanji juzi alimkabidhi mafuta ya upako, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba kwa ajili ya kung’arisha nyota yake katika harakati zake za kuwania urais.
Nabii Mpanji alisema mafuta hayo yanaashiria ufalme na utawala na kusisitiza kwamba kitendo hicho ni kudhihirisha kuwa Nchemba, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, anafaa kuliongoza Taifa.
Tukio hilo lilifanyika kwenye ibada maalumu iliyoambatana na harambee ya kuchangia vifaa vya redio ya kanisa hilo iliyoendeshwa na Nchemba na Sh53 milioni zilipatikana.
Alimtaka Nchemba kutamka nia yake ya kugombea urais mbele za watu, huku akisisitiza kuwa Taifa linahitaji mtu anayeweza kusimamia wananchi wenye kipato cha chini na kumtaja mbunge huyo wa Iramba Magharibi kuwa amethubutu kufanya hivyo.
“Mimi nasema wazee wasikuumize kichwa, hata Biblia inasema fahari ya wazee ni mvi zao lakini fahari ya vijana ni nguvu zao. Tunahitaji Watanzania wazalendo na jasiri ambao wanaweza kusema bila kuogopa kama wewe (Nchemba),” .
Akizungumza katika ibada hiyo, Nchemba aliwashukuru Watanzania wenye imani naye na kubainisha kuwa muda ukifika atasema nia yake.
“Imebaki kitambo kidogo nitasema kwani mimi ni kiongozi wa chama, hivyo natakiwa kufuata taratibu na kanuni cha chama, nawaomba mvute subira kidogo nitasema tu,” alisema.
Nchemba alisema upako huo ni dalili tosha za Watanzania kutambua mchango wake katika kuwatumikia na yeye hatawaangusha… “Tutavuka mto tukifika mtoni.”
Mwigulu ambaye aliongozana na waimbaji maarufu wa nyimbo za Injili akiwamo Boniface Mwaitege na Moses Makondeko, alisema katika suala hilo (la urais) anamtegemea sana Mungu.
Aliwataka wananchi kuwa na uchungu na nchi yao kwa kutanguliza uzalendo kwani ni vigumu kupata kiongozi mzalendo katika Watanzania wasio kuwa na uzalendo.
Akisoma risala mchungaji wa kanisa hilo, Aquina Mhanze alisema mahitaji ya kanisa hilo ni Sh200 milioni kwa ajili ya kukamilisha vifaa vya redio na ofisi na kwamba kwa sasa kuna Sh15 milioni.
Alisema kuwa kati ya fedha hizo, Sh150 milioni ni kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya redio na Sh50 milioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya redio.
Usiwe mbali nami na nitakusogezea kila kinachonifikia hapa hapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment