SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
MWANAMKE 32
ILIPOISHIA
Mgosingwa alitia mkono kwenye
mfuko wa shati lake akatoa ganda kama la
kitambulisho akaniwekea mezani.
“hii si leseni yako
Mgosingwa?’ akaniuliza.
Nikalichukua lile ganda na
kulifungua. Naam. Ilikuwa ni leseni yangu niliyokuwa nimeitupa kule makaburini.
Pale pale uso wangu ulibadilika rangi kwa hofu iliyochanganyika na fadhaa.
Nikamtazama mgosingwa huku nikijiuliza ameipata wapi leseni yangu.
“Huku nikiendelea na tabasamu
langu la kulazimisha nilimuuliza.
“Mgosingwa umeipata wapi hii
leseni yangu?’
“Si nimekwambia unatakiwa
polisi?”
Jibu lake hilo
lilizidi kunichanganya na kunifadhaisha. Midomo yangu niliyokuwa ninailazimisha
kutabasamu huku nikiwa na fadhaa ilianza kutatizika na kutetemeka. Sasa
haikuweza tena kutabasamu.
“Mgosingwa unanichanganya.
Sasa nani kakupa hii leseni na kakupa kwa madhumuni gani?” nikamuuliza huku
nikiizuia modomo yangu isitetemeke wakati nikimuuliza hivyo.
Mgosingwa aligundua kuwa
nilikuwa nimetaharuki. Akacheka. Hata hivyo kwa vile uso wake ulikuwa
umekunjana kutokana na kuendeleza kilevi, kicheko chake hakikuufanya uso wake
upendeze, bali ulionekana kama anataka kulia.
“Mgosingwa hukumbuki uliiacha
wapi leseni yako?” akaniuliza.
Nikatikisa kichwa.
“Sikumbuki” Nilimjibu hivyo
ili nijue ataniambia nini.
“Mgosingwa jana usiku si
ulikuja kule makaburi ukafukua lile kaburi nikakukurupusha”
SASA ENDELEA
Aliponiambia hivyo nikanywea
na kumtazama. Alipoona nipo kimya aliendelea kunieleza.
“Wakati unakimbia mgosingwa
uliiangusha hii leseni yako”
“Kumbe wewe ndiye unayelinda
pale?” nikamuuliza.
“Nilipoacha kazi STC
niliajiriwa na kanisa kulinda yale makaburi. Sasa jana usiku niliondoka kidogo
kwenda kupata ulabu (kilevi), niliporudi nikakuta mtu amechimba kaburi na
kuingia ndani. Hii leseni niliiokota asubuhi ndio nikagundua kuwa ulikuwa wewe”
“Sasa Mgosingwa umeshakwenda
kutoa ripoti polisi?”
Polisi nimeshakwenda lakini
nilipoona hii leseni yako sikuwapa. Niliwambia huyo mtu sikumuona vizuri”
Hapo hapo nilitia mkono
mfukoni nakutoa pochi yangu. Niliifungua na kuchomoa noti za shilingi elfu
ishirini, nikampa.
“Asante
sana Mgosingwa, umenisaidia sana”
SASA ENDELEA
“Tunajuana Mgosingwa ,
hatuwezi kusalitiana” Mgosingwa aliniambia wakati akipokea zile pesa.
“Unajua lile kaburi ni la
shemeji yake mhasibu wetu. Mimi sikujua kabisa”
“Kwani ulikuwa unataka nini
Mgosingwa?”
“Kuna kitu nilikuwa nataka”
“Kitu gani?”
Kwanza nilisita kumwambia nilikuwa nataka nini lakini
nikaona ni vizuri nimwambie.
“Nilikuwa nataka kucha za
maiti”
“Mgosingwa unataka kwenda
kuroga au kuua mtu?”
“Hapana. Ni kwa mambo yangu
binafsi”
“Mgosingwa ungeniambia,
ningekupatia. Mimi Ndio nalinda yale makaburi”
“Bado ninazihitaji Mgosingwa,
nifanyie huo mpango”
“Utanipa shilingi ngapi?”
“Ukiniletea hizo kucha
nitakuongezea kumi nyingine”
“Fanya ishirini Mgosingwa,
kumi ndogo sana”
“Si kitu, nitakupa hizo
ishirini”
“Sasa Mgosingwa nitafutie
shepe na kiwembe. Niletee pale saa nne usiku. Mimi nitafukua kaburi, asubuhi
nitakuletea hizo kucha nyumbani kwako”
“Hakuna tatizo. Nitakuletea hilo shepe. Kiwembe
utanunua mwenyewe”
“Sasa Mgosingwa fanya kitu
kimoja, nipatie kianzio cha shilingi elfu kumi, hiyo kumi nyingine utanipa
asubuhi”
Nilitaka kucheka lakini
nilisita kwa sababu tulikuwa katika suala nyeti sana kwa upande wangu.
“Kwanini usisubiri hadi hiyo
asubuhi nikupe zote?” nikamuuliza.
“Ninahitaji hiyo pesa kwa
sasa”
“Mgosingwa si nimekupa elfu
ishirini za bure?”
“Mgosingwa si za bure, polisi
ungetoa ngapi ili wakuachie”
“Sawa. Sasa si hizo nimekupa”
“Hazitoshi Mgosingwa”
“Wewe unataka kwenda kulewa
tu” nikamwambia huku nikitia mkono kwenye mfuko wa suruali yangu.
Nilitoa pochi yangu
nikaifungua na kumpa shilingi elfu kumi alizotaka.
“Umeridhika?” nikamuuliza.
“Hapa Mgosingwa umeniokoa sana”
“Utapata chupa ngapi”
“Acha mzaha Mgosingwa. Mimi
siendi kulewa. Mke wangu amekwenda kwao kujifungua. Nilitaka kumtumia hzi pesa”
“Sawa Mgosingwa mtumie,
nilikutania tu”
“Sasa Mgosingwa niletee shepe
saa nne usiku pale pale”
“Sawa, nitakuletea”
Nikaagana na Mgosingwa na
kuondoka.
Nilipotoka kazini jioni
nilikwenda kununua shepe jingine nikaenda nalo nyumbani. Nikawa nasubiri saa
nne usiku ifike nimpelekee Mgosingwa.
Kwa mara ya kwanza niligundua
hata mlevi anaweza kuwa na manufaa yake. Sikutarajia kuwa Mgosingwa mlevu wa
gongo na pombe ya mnazi angeweza kunisaidia. Licha ya msaada wa kucha za maiti
alioniahidi, kile kitendo chake cha kuiokota leseni yangu na kuja kunipa
mwenyewe bila kuipeleka polisi ulikuwa msaada mkubwa kwangu.
Nilimshukuru sana
nikijua kama si yeye ningeumbuka. Pengine muda
ule ningekuwa niko mahabusi.
Ilipofika saa nne usiku
nililifunga lile shepe sehemu ya nyuma ya siti ya pikipiki yangu nikatoka.
Nilikwenda katika lile eneo
la makaburi analolinda Mgosingwa. Niliposimamisha tu pikipiki, Mgosingwa
akajitokeza. Alitazama kila upande, alipoona kuko kimya akasogea kwenye
pikipiki yangu na kunisaidia kulifungua lile shepe.
Ile hewa yake ya mwilini tu
ingetosha kumlewesha mtu. Alikuwa akinuka pombe aina ya gongo kama
vile alikuwa mtambo wa kuitengenezea. Muda ule tayari alikuwa ameshalewa.
Sikumlaumu. Kulinda makaburi
wakati wa usiku ilikuwa kazi ya kutisha. Alihitaji kupata kitu cha kutuliza
akili yake, vinginevyo anaweza kuota ndoto za maiti waliozikwa usiku kucha.
Hatukuungumza chochote.
Alipochukua lile shepe, alinionesha ishara kuwa tukutane asubuhi akatokomea
makaburini.
Nikapanda pikipiki yangu na
kuondoka. Nilipofika nyumbani nilifikia kuoga na kulala.
Kulikuwa kunaanza kupambazuka
nilipoamshwa usingizini kwa kishindo cha mlango wa mbele uliokuwa unabishwa.
Nikatazama saa yangu na kuona ilikuwa saa kumi na mbili kasorobo. Nikajiuliza
ni nani abishae mlango? Sikupata jibu.
Nikashuka kitandani na kuvaa
suruali yangu kisha nikafungua mlango wa chumbani mwangu na kutoka ukumbini.
Nilikwenda kwenye mlango wa mbele na kuuliza.
“Nani abishaye?”
“Ni mimi Mgosingwa!”
nikaisikia sauti ya Mgosingwa ikisikika kwa nje.
“Ahaa ni wewe!” nikasema huku
nikifungua mlango.
JE MGOSINGWA AMEPATA HIZO
KUCHA? JIBU UTALIPATA KESHO
No comments:
Post a Comment