WAKATI Mahakama Maalumu ya Ufisadi na Uhujumu Uchumi ikitarajiwa kuanza wakati wowote, majengo ya mahakama hiyo yanatarajiwa kukabidhiwa kesho kutwa jumatatu.
Jaji Mkuu, Mohamed Othman Chande, alisema jana kuwa mkandarasi aliyekabidhiwa kazi ya kukarabati majengo hayo yaliyopo katika Shule Kuu ya Sheria, pembeni mwa kituo cha mabasi cha Simu 2000, Ubungo Dar es Salaam, yako katika hatua za mwisho za ukarabati.
Akizungumza katika viwanja vya Karimjee baada ya kuapisha mawakili wapya 623 wa Mahakama Kuu, Jaji Chande alisema tayari Bunge limeshapitisha muswada wa sheria ya uanzishwaji wa mahakama hiyo.
Alisema kwa sasa muswada huo utawasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuusaini ili uwe sheria, kisha sheria hiyo itatangazwa katika gazeti la Serikali ili kuruhusu shughuli za mahakama hiyo kuanza.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Mahakama iko tayari kuendesha Divisheni hiyo ya Mahakama na baada ya kukabidhiwa majengo hayo, wataanza kutoa semina kwa majaji na watumishi wengine wa mahakama hiyo, kuhusu divisheni hiyo itakavyoendesha shughuli zake.
Aliweka wazi kuwa mpaka sasa hakuna kesi hata moja iliyokwishatambuliwa kwamba itashughulikiwa na mahakama hiyo.
No comments:
Post a Comment