Saturday, February 14, 2015

SOMA HABARI KUU ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO, TZ

Uchambuzi huu unaletwa kwenu kwa hisani ya Mkombozi Sanitarium Clinic, Mabingwa wa tiba Asilia. Wapo Tanga Chuda na wanapatikana kwa simu 0654 361333
News_Alert_1369436086208_419918_ver1.0_320_240
MWANANCHI
Santnam Singh mwenye umri wa miaka 43 amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh 380,000/- baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na kisu katika Uwanja wa Kimataifa wa JNIA Dar ambapo mtuhumiwa huyo aliachiwa huru baada ya kulipa faini.
Akisoma hukumu hiyo leo, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Hassan Juma amesema kwamba mahakama imemtia hatiani mshtakiwa huyo kutokana na kukiri kutenda kosa hilo na kutakiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh 380,000.
Upande wa mashitaka ulithibitisha mashitaka yake bila ya kuacha shaka kwa kutoa kielelezo cha mashitaka hayo ambacho ni kisu.
Katika utetezi wake, Singh alidai kwamba anategemewa na familia yake na kwamba anaomba apunguziwe adhabu, ombi ambalo lilitupiliwa mbali.
Singh alidaiwa kwamba Januari 10 mwaka huu, maeneo ya Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar alikutwa na kisu kinyume na sheria.
JAMBO LEO
Mlinzi wa Makao makuu ya BIMA ambaye jina lake halijafahamika amezimia baada ya Polisi kupiga risasi juu kwa bahati mbaya wakati wakichukua fedha katika tawi la Benki.
Mlinzi mwenzake aliulizwa mwenzake alipo baada ya tukio hilo akasema kuwa amerudi nyumbani.
Askari alikuwa akiweka sawa silaha yake, lakini kwa bahati mbaya ikatoka..” aliongea shuhuda mmoja, Benard Adam ambaye ni mfanyabiashara.
JAMBO LEO
Maiti za watoto wachanga watatu wanaokadiriwa kuwa na umri wa mwezi mmoja zimekutwa zikiwa ndani ya mfuko wa rambo kwenye jokofu ndani ya nyumba ya mtu Johannesburg, Afrika Kusini.
Mfanyakazi wa ndani amesema aligundua harufu kali kutoka kwenye friji akahisi ni nyama imeharibika, baada ya kufungua akakutana na miili ya watoto hao.
Mfanyakazi huyo amesema aliagizwa kufanya usafi ili wakafanye mazishi ndipo alipogundua kuwepo kwa miili ya watoto hao kwenye friji hiyo.
NIPASHE 
Kamanda wa Kikosi cha Askari wa Usalama Barabarani Mohamed Mpinga amesema madereva wengi hawana nidhamu wanapokuwa wakiendesha vyombo vya usafiri na kusababisha 20% ya wanaopata ajali kufariki kutokana na matumizi ya pombe.
Wengi wa madereva wanapopimwa kipimo kinaonyesha wamelewa kwa asilimia 90, pia Kenya na Burundi ni kama Tanzania“—Kamanda Mpinga.
Aidha, alisema madereva wengi wanatumia pombe za viroba kwa kuchanganya kwenye maji, suala ambalo linazidi kuhatarisha usalama wa barabarani.
Kamanda Mpinga alisema ajali kwa Tanzania zimepungua kwa 39% mwaka 2013-2014, upungufu huo ni 29%, ajali zilizosababisha vifo ni 23,842 mwaka 2013 na mwaka 2014 ajali zilizosababisha vifo ni 14,360.
Mpinga amesema madereva waliopata ajali na kupata ulemavu wakudumu ni 12%, waliopata majereha ni 20,689 kwa mwaka 2013 na kwa mwaka 2014 waliopata majereha ni 14,530.
Mpinga alisema kuwa ajali zimepungua kutokana na Jeshi la Usalama Barabarani kusimamia sheria pamoja na kutoa adhabu kali kwa madereva wazembe na kufanya ukaguzi wa magari mabovu mara kwa mara.
NIPASHE
Wizi wa fedha kwa njia ya mtandao kupitia mashine maalum za kutolea fedha (ATM) unaendelea kuzitesa benki mbalimbali nchini ambapo kwa sasa wahalifu hao wanahamisha fedha za wateja wakiwa nje ya nchi kwa kutumia kadi za kutolea fedha.
Wizi huo hufanyika kwa kutumia kadi za kutolea fedha zinazoingiliana na benki zingine (smart card) ambazo mteja wa benki anaweza kutolea fedha akiwa popote duniani kupitia ATM.
Chanzo cha habari cha Gazeti la NIPASHE kimetaarifu kuwa wezi hao hucheza na password za watu wanaopenda kutoa fedha zao kupitia ATM zilizowekwa sehemu mbalimbali hasa kwenye vituo vya kujazia mafuta ambapo mmoja ya waathirika wa tukio la aina hiyo amesema juzi alipigiwa simu na ofisa mmoja wa benki akimuuliza kama siku hiyo alitoa fedha akiwa nje ya nchi.
Alisema ofisa huyo alimpigia simu baada ya benki kupata wasiwasi kwa kuwa taarifa hazionyeshi kama mteja huyo huchukua kiasi hicho kikubwa cha fedha kwa mara moja.
 “Nilipigiwa simu na mtu akaniuliza wewe ni fulani (akataja jina), akaniuliza  nimetoa fedha kiasi fulani nikiwa Mombasa? Nikamjibu sijatoa na sijawahi kutoa fedha nje”.
Chanzo hicho kilisema, ofisa huyo alimwambia kuna hamisho la fedha limefanyika kutoka kwenye akaunti yake nje ya nchi na kumtaka aende kwenye tawi lolote la benki hiyo ili aombe taarifa yake ya kibenki na kisha aandike barua ya kulalamika kuwa hajatoa fedha hizo kwenye akaunti yake.
Nilipoitazama nikaona fedha zangu zimehamishwa na mtu aliyekuwa Mombasa, Kenya,”; alisema mtu huyo na kuongeza kuwa alitakiwa kuandika barua kwa meneja wa benki hiyo kwenye Tawi hilo ili aombe kurejeshewa fedha hizo.
Alisema wakati huo akaunti yake ilikuwa imefungwa na kadi imezuiwa kutoa fedha na kutaka kujaza fomu ya kupata kadi nyingine ambayo alipewa ndani ya dakika tano na baada ya kukamilisha taratibu za madai alipata taarifa iliyomjulisha kuwa fedha zake zitarudishwa ndani ya siku 45.
Afisa mmoja wa benki ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini alikiri kuwa kuna wizi wa fedha wa mara kwa mara kwa njia ya mtandao ambao benki umeshaugundua.
Alisema wezi hao hutumia njia mbali mbali kujua password za watu ikiwemo ya kuweka kamera ndogo kwenye ATM na vile vile kwa kutumia utalaam wa kiteknolojia wa hali ya juu kusoma taarifa za benki na kuzitumia kuiba fedha kwenye akaunti za watu.
Alishauri wanaopenda kutoa fedha kwenye ATM waende kwenye ATM zilizo kwenye matawi ya benki husika kwa kuwa wanaoweka kamera sio rahisi kwenda kwenye matawi ya benki.
Gavana wa BoT, Prof. Benno Ndulu aliwahi kukaririwa akisema wameziagiza benki kuweka kifaa cha umeme (electronic chip) kwenye kadi zao za ATM ambazo si rahisi kughushi.
NIPASHE
Uchunguzi uliofanywa na Gazeti la NIPASHE umegundua Wanafunzi wa shule za sekondari jijini Dar es Salaam, wamejiingiza katika wimbi la utumiaji wa dawa za kulevya na uchezaji kamari, hali inayoodhofisha elimu huku bangi, heroin na cocaine zikiongoza kwa kuuzwa.
Wanafunzi hao kwa sasa wameunda mtandao maalum wa kuwakutanisha na wafanyabiashara wa madawa hayo ili kuepuka kukamatwa na polisi.
Moja ya eneo lililoshamiri kwa matukio hayo ni Toangoma jirani na shule mbili za sekondari ya Malela na Toangoma, ambapo hivi karibuni wanafunzi sita walikamatwa wakiwa na kete 116 ya bangi na misokoto sita huku mtu mmoja Bashir Hemed akitiwa mbaroni kwa kutuhumiwa kumiliki shehena ya bangi iliyokutwa eneo hilo.
Hamisi Zuberi ambaye aliongoza zoezi la kupambana na mtandao huo, alisema wanafunzi hao sita ni miongoni mwa wengine zaidi ya 100 waliokutwa wakinunua na kutumia.
Ni tukio baya hasa kutokea kwa idadi kubwa ya wanafunzi wakivuta bangi nje ya shule, ni mtandao mkubwa unaowahusisha wafanyabiashara na wanafunzi,”– Hamisi Zuberi.
Wanaokuja kuuza majani (bangi) mbona wapo wengi tu, tunaomba serikali iongeze kasi ya kuwakamata ili tuweze kusoma vizuri kwani mara nyingi wanapotoka kuvuta wanatusumbua darasani,” alisema mwanafunzi mmoja
Makamu wa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Toangoma, Florian Kilindo alikiri kuzidiwa na mtandao huo ambapo walimu walioufuatilia walitishiwa usalama wao hivyo kuitaka serikali kuingilia kati.
Imefika wakati sisi kama walimu tumeona hatuwezi tena kuwadhibiti, kila mara tumeomba msaada wa polisi kuja kuwakamata lakini bado mtandao unazidi kukua na kuhatarisha usalama wetu na wanafunzi wengine darasani,” alisema.
Mwalimu Kilindo, aliwalaumu wazazi kukwepa majukumu ya kuwafuatilia watoto wao, badala yake wanaona kazi hiyo inafanywa na walimu pekee.
Uongozi wa shule hiyo umewasimamisha masomo wanafunzi wanaohusishwa na utumiaji wa dawa hizo hadi hapo Bodi ya shule hiyo itakapokaa na kuwajadili.
Polisi wametuambia wamewaachia huru kwa sababu hawana sheria ya kuwashikilia wanafunzi kwa muda mrefu, hapa tunavyoongea wameachilia lakini sisi tumewasimamisha masomo,” – Mwalimu Kilindo.
Diwani wa Kata ya Toangoma, Rashid Mikuki amesema amesikitishwa kuona wanafunzi wanaoacha shule na badala yake wanaishia porini kuvuta bangi.
Waziri wa Elimu na Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa alipoulizwa kuhusu suala hilo, alionyesha kushtuka na kusema kwamba hakutarajia kulisikia na aliahidi kulifanyia kazi.
RAIA TANZANIA
Wiki mbili tangu tarehe ya mwisho itangazwe na TRA kwa wanufaika wa fedha za Escrow kulipa kodi, taarifa zilizolifikia gazeti la RAIA TANZANIA ni kwamba agizo hilo limeanza kutekelezwa.
Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade amesema fedha hizo zimekusanywa kutoka katika Ankara za malipo (invoices) walizopelekewa wadaiwa mwishoni mwa mwaka jana japo amesema kuhusu kiasi kilichokusanywa ni siri kama ambavyo taarifa za walipa kodi wengine huwekwa siri.
Sisi tunafanya kazi kwa mujibu wa Sheria  na walipa kodi wanatakiwa kulipa kodi husika. Siwezi kukutajia kiwango kilichokusanywa”—Rished Bade.
Wakati wa Bunge lililopita Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema kiwango cha pesa kinachotakiwa kukusanywa ni sh. Bil 26 na iwapo TRA wakikusanya kiwango hicho cha pesa basi ni furaha kubwa kwake.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia , niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com

No comments:

Post a Comment