Wednesday, May 13, 2015

WAANDISHI WAHABARI WAAASWA VITAMBULISHO VYA TAIFA

Tanga, WAANDISHI wa habari Tanga, wametakiwa kuvitumia vyombo vyao vya upashaji habari kuielimisha jamii katika zoezi la uchukuaji wa alama na upigaji picha ili kila mmoja kuweza kupata kitambulisho cha Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Abdalla Lutavi, alisema vyombo vya habari viko na nafasi kubwa ya kulifanikisha zoezi la vitambulisho vya Taifa.

Alisema jamii kubwa ya watu hasa wa vijijini bado haina uelewa mpana  wa kuwa na vitambulisho vya Taifa na hivyo kuvitaka kuzipa nafasi kubwa ya kutoa   elimu ya kwenda kujisajili na kuweza kupata kitambulisho.

“Zoezi hili bila vyombo vya habari linaweza kuiwanyima makundi ya watu haki ya kuwa na kitambulisho cha Taifa----nawaombeni sana kuelimisha jamii umuhimu wa vitambulisho” alisema Lutavi na kuongeza

“Hebu sasa vyombo vya habari kujikita maeneo ya vijijini kwani kuna makundi ya kijamii bado hayana uelewa wa kuwa na kitambulisho cha taifa----ili kuweza kulifanikisha hili ni ninyi waandishi wa habari kuandika sana juu ya kitambulisho cha taifa” alisema

Alisema waandishi wengi wa habari wamekuwa waking’ang’ania habari za mjini na kusahau makundi ya jamii za vijijini na hivyo kukosa fursa nyingi za kihabari pamoja  mambo mengine ya kijamii.

Akizungumza katika mkutano huo, Afisa habari mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Rose Mdami, aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi katika kujisajili kwani vitambulisho hivyo viko na umuhimu mkubwa katika Nyanja mbalimbali za kijamii.

Alisema kuacha kufanya hivyo mtu ataweza kupoteza haki na fursa nyingi zikiwemo za utambulisho wa utaifa na hivyo kuwataka kujitokeza na kutoa vielelezo sahihi.

“Nawaomba Watanzania wenzangu kujitokeza kwa wingi katrika zoezi la upigaji picha na uchukuliwaji wa alama pamoja na kutoa taarifa sahihi----hii itasaidia mustakbali mzima wa zoezi la vitambulisho” alisema Mdami

Aliwataka kuzitumilia vyema siku zilizotolewa za upigaji picha na alama na kihakikisha kila mmoja ameweza kulifanya jambo hilo muhimu binafsi na kwa Taifa.

                                                     Mwisho

Tangakumekuchablog




No comments:

Post a Comment