Sunday, May 10, 2015

WALALAMIKIA UCHAFU SOKONI MGANDINI TANGA

Tangakumekuchablog

Tanga,WAFANYABIASHARA soko kuu la Mgandini Tanga, wameutaka uongozi wa soko kujenga  miundombinu ya maji ili nyakati za mvua kunyesha kuondokana na kero ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi na tope.

Wakizungumza na waandishi wa habari sokoni hapo jana, wafanyabiashara hao walisema kipindi hiki cha mvua wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu na wateja kukimbia.

Walisema kwa hali ilivyo sasa ni vigumu kwa wateja kufika sokoni hapo kwani mazingira ni magumu ya kumshawishi mteja kufika na kununua bidhaa baada ya eneo kubwa kujaa maji na kufanya tope.

“Mazingira ya soko kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha ni hatari----eneo kubwa la soko limejaa maji na tope kwa kweli hii ni hatari” alisema Kassim Mvumo mfanfabiashara wa nyanya

“Kila mwaka huwa tunawambia viongozi wetu kuwa soko hili halina miundombinu ya kupitisha maji----sasa wenyewe wanajionea” alisema
Alisema soko ambalo limekuwa likitegemewa na wakazi wengi jijini humo uongozi wa soko unatakiwa kuliweka katika mazingira mazuri ili wateja kuepuka kulikimbia.

Akizungumzia kero hiyo, Mwenyekiti wa soko hilo, Adam Tindikai, alisema kero hiyo wanaitambua na uongozi wa soko unafanya jitihada na halmashauri ya jiji ili kuweza kuimaliza kero hiyo.

Alisema kwa sasa wako katika jitihada ya kuondosha maji yaliyotuwaa katika tope pamoja na kuondosha takataka ikiwa na pamoja na kuweka mazingira mazuri  ya soko hilo.

“Kweli tuko na changamoto nyingi katika soko letu hasa vipindi vya mvua----ila tuko katika jitihada za kukabilia na kero hasa nyakati za mvua ili kuwawezesha wateja wanaotumia soko hili kuacha kulikimbia” alisema Tindikai

Amewataka wateja na wafanyabiashara kuwa na uvumilivu kipindi hiki cha mvua wakati uongozi wa soko uko katika jitihada kuhakikisha kero zinamalizwa kwa wakati.

                                                    Mwisho




No comments:

Post a Comment