HADITHI HII INALETWA KWENU KWA HISANI YA MKOMBOZI SANITARIUM CLINIC, MABINGWA WA TIBA ASILIA, WAPO CHUDA TANGA, 0654361333
KISIWA CHA HARISHI (30)
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
Rais wa Zanzibar akawasiliana na Rais mwenzake wa
Comoro na kuzungumza naye.
“Binti yako Yasmin ninaye
hapa” Rais wa Zanzibar
alimwambia Rais wa Comoro.
“Nimepata habari zake na
nimeshukuru sana
kusikia kwamba mwanangu bado yuko hai. Sisi tulidhani ameshakufa” Rais wa
Comoro alisema kwenye simu.
“Ni kweli kwamba alipotea
siku ya harusi yake mwaka mmoja uliopita?”
“Nikweli. Lilikuwa tukio la
kushangaza sana!”
“Ameniambia alikuwa akiishi
katika kisiwa kimoja kisicho na watu na hajui alifikaje katika kisiwa hicho”
“Binti yangu alipata masahibu
makubwa lakini nashukuru kuwa amenusurika”
“Huyu hapa, ongea naye”
Rais alimpa Yasmin mkono wa
simu ili azungumze na baba yake.
“Asalam alaykum baba!” Yasmin
alimwamkia baba yake.
“Wa alaykum salam
warahmatulahi wabarakat. Hujambo mwanangu?”
SASA ENDELEA
“Sijambo baba. Matatizo
yaliyonitokea ni kama ulivyoyasikia”
“Nimeyasikia na nimemtuma
kaka yako Umar na maofisa wangu kuja kukuona. Nimeambiwa kuwa mmeshakutana”
“Tumekutana na kaka ninaye
hapa”
“Nimefurahi kwamba uko naye
kwa rais mwenzangu. Je wewe afya yako ikoje?”
“Afya yangu si nzuri lakini
pia si mbaya sana.
Nikija huko mtaniona”
“Ulikuwa unaishi vipi huko
kisiwani ulikokuwa?”
“Nimeishi kwa taabu tu baba.
Nikija nitawaeleza vizuri”
“Ningependa uzungumze na mama
yako ili umtoe wasiwasi lakini hatapatikana kwa sasa kwa sababu mimi bado niko
ikulu”
“Hakuna wasiwasi baba. Mwambie
mama mimi ni mzima. Ni masahibu tu yamenikuta na ishallah nitakutana naye”
”Si mtakuja hii leo?”
“”Kama
tutaruhisiwa kuondoka tutakuja leo”
“Sawa. Sasa mpe simu
mheshimiwa rais”
Yasmin akampa samu rais wa Zanzibar.
“Umeshazungumza na mwanao?”
Rais wa Zanzibara akamuuliza rais wa Comoro kimzaha.
“Tumezungumza kidogo.
Unatarajia wataweza kuondoka leo hii kurudi Comoro”
“Kwa vile ndege iko tayari
sioni cha kuwazuia kuondoka leo”
“Basi ningependa uwaruhusu
kuondoka na mtupatie taarifa muda ambao wanaondoka”
Baada ya maraisi hao kumaliza
kuzungumza, rais wa Zanzibar
alizungumza na maofisa wake.
“Nataka mhakikishe kuwa ugeni
huu unaondoka leo kurudi Comoro. Na kwa upande wa huyu binti apatiwe mahitaji
yote ya kibinaadamu kwa gharama ya serikali wakati akiwa hapa nchini kwetu bila
kumsahau kijana Zahrani aliyekuwa naye kule kisiwani”
Baada ya rais kutoa agizo hilo aliagana na sisi na
kuwatakia safari njema akina Yasmin.
Yasmin alimuahidi rais wa Zanzibar kuwa hataisahau Zanzibar na atarudi kuitembelea tena
atakapojaliwa.
Tulipotoka ikulu tulipelekwa
katika hoteli ya Bwawani ambako tulipatiwa huduma mbalimbali kama
vile chakula, nguo na mahali pa kupumzika. Hapo tulikutana na watu mbali mbali
waliopata habari zetu na kututembelea. Walikuja maofisa wa serikali na pia
mawaziri.
Kusema kweli nilipata
umaarufu mkubwa kutokana na Yasmin. Kwa vile mwenzangu alikuwa binti wa rais na
alikuwa akieleza mara kwa mara kuwa kama si
mimi na yeye angeangamia, watu waliotutembelea walikuwa wakitupa pole pamoja na
kunipongeza.
Maelezo yetu yalionekana kama kioja kikubwa kwa vile yalimuhusisha jini anayeitwa
Harishi ambaye alimteka Yasmin nchini Comoro na kumpeleka katika kile kisiwa
cha mauti.
Taarifa zilipowafikia
waandishi nao walianza kumiminika katika hoteli ya Bwawani kutuhoji na kutupiga
picha.
Baadhi ya waandishi hao baada
ya kupata maelezo kutoka kwangu na kwa Yasmin, walimuhoji Yasmin kutaka kujua
jinsi tulivyoishi katika kisiwa hicho tukiwa peke yetu.
Mwandishi: “Mliishije na
Zaharani mkiwa watu wawili wa jinsia tofauti katika kisiwa hicho?”
Yasmin: “Tuliishi kama
marafiki”
Mwandishi: “Mlitarajia kuwa
mngeokoka?”
Yasmin: “Kusema kweli
hatukutarajia ingawa tulikuwa tunaomba sana”
Mwandishi: “Mlikuwa mnalalaje
usiku?”
Yasmin: “Usiku wa jana ndio
tulilala pamoja lakini pia hatukulala usingizi kwa sababu tulijua kuwa
tungeuawa”
Mwandishi: “Sasa umeshaokoka.
Unadhani utaendelea kuwa karibu na Zahrani?”
Yasmin: “Bila shaka.
Tulipokuwa kule kisiwani nilimpa ahadi Zahrani kuwa kama tutasalimika atanioa”
Mwandishi: “Una maana kwamba
umempenda Zahrani?”
Yasmin akacheka kabla ya
kujibu. “Nimempenda sana”
Mwandishi: Je sasa unadhani
utatimiza ahadi uliyomuahidi?”
Yasmin: “Ndiyo nitaitimiza”
Mwandishi: “Kwa hiyo una
mpango wa kuoana na Zahrani?”
Yasmin: “Mpango bado, ni
mawazo tu ambayo naamini hayatabadilika”
Mwandishi: “Umetuambia kuwa
kabla ya kupotelea katika kisiwa mlichokua mnaishi ulikuwa unaolewa na mwana wa
mkuu wa jeshi la ulinzi la Comoro, je kijana huyo akitaka muoane tena itakuwaje
wakati umeshamuahidi Zahrani kuwa mtaoana?”
Yasmin: “Nadhani atakuwa
ameshaoa”
Kaka wa Yasmin Umar Sharif
Abdulatif ambaye alikuwepo wakati Yasmin anahojiwa alithibitisha kuwa aliyekuwa
anamuoa Yasmin kabla ya Yasmin kupotea Comoro alishaoa mke mwingine na walikuwa
wanaishi Ufaransa. Visiwa vya Comoro vilikuwa koloni la Ufaransa.
Mwandishi: “Kwa hiyo
unatarajia kwenda Comoro na Zaharani?”
Yasmin: “Natarajia hivyo”
Mwandishi: “Ndoa yenu
itafanyika lini?’
Yasmin: “Siku yoyote wazazi
wetu watakaponiidhinisha kuolewa na Zaharani”
Mwandishi aliyekuwa akimuhoji
Yasmin alinigeukia mimi.
Mwandishi: “Je
umeyachukuliaje maelezo ya Yasmin?”
Zahrani: “Yamenifurahisha sana”
Mwandishi: “Uko tayari kuoana
na msichana ambaye baba yake ni rais wa nchi?”
“Zahrani: “Kama
wazazi wake watakubali niko tayari”
Mwandishi: “Mtakuwa mnaishi
wapi mtakapooana, Zanzibar au Comoro?’
Zahrani : “Popote tu
tutakapokubaliana”
Mara tu baada ya waandishi wa
habari kuondoka maofisa usalama kutoka ikulu ya Zanzibar
walinitambulisha kwamba umefika wakati ambapo nitaachana na Yasmin kwa vile
muda wa safari yao
ya kurudi Comoro ulikuwa umefika.
Kauli ile ilinivunja moyo
hasa kwa vile nilitegemea kuondoka na Yasmin. Yasmin akawaomba maofisa hao
waniache niende naye Comoro.
“Hatumzuii mtu yeyote kwenda
mahali popote anapotaka ila Zahrani hana hati ya kusafiria” Afisa mmoja
alimwambia Yasmin.
ITAENDELEA KESHO, USIKOSE UHONDO HUU HAPO KESHO SAFARI YA ZAHRAN ITAKUWEPO AU KUTATOKEA MIZENGWE?
No comments:
Post a Comment