Sunday, January 4, 2015

Wakazi wa mji wa Wete wataka bodaboda



Kumekucha blog
Pemba,VIJANA mji wa Wete Wilaya ya Kaskazini Pemba wameitaka Serikali kuruhusu biashara ya kubeba abiria  maarufu kama (bodaboda) ili kuondokana na wimbi la vijana wasio na kazi na kuacha kujingiza katika  magenge ya wavuta bangi na wabwiaji wa unga.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti jana, vijana hao wamelalamika kuzuiwa kubeba abiria kwa madai kuwa  hakuna sheria inayoruhusu   kufanya hivyo.
Walisema kuruhusiwa kubeba abiria kwa kutumia pikipiki ingelileta mabadiliko makubwa kwa vijana mjini humo baada ya walio wengi kutokuwa na kazi na badala yake wamekuwa wakikaa katika baraza za kahawa na kupiga soga.
“Vijana wengi hawana ajira rasmi na wala hakuna kazi ya kufanya ukapata kipato ukaweza kujiendesha maisha yako---tumekuwa tukiwaona vijana wenzetu katika maeneo Bara wakibeba abiria na kujiuliza kwa nini na sie tusiwe kama wao” alisema Salim Ali
“Huku kwetu hakuna daladala za kuingia mashamba na katikati ya mji hivyo kuwepo kwa bodaboda ingekuwa msaada kwa jamii na sisi vijana kujikwamua na maisha na kuepuka kukaa katika baraza za kahawa na kupiga soga lisilo na maana” alisema
Kwa upande wake mkazi wa Chanjaani Shehia ya Gando, Shaban Nassour, amewataka vijana kujituma kwa kufanya kazi kwa bidii na kuacha kuilalamikia Serikali ili  kuwapatia kazi.
Aliwambia kuwa Serikali kazi yake ni kuharakisha palipo na maendeleo na kutoa msukumo na hivyo kuwataka kuonyesha dhamira ya kweli katika kujikomboa na umasikini katika maeneo yao kwa kufanya kazi kwa bidii.
Alisema kuna baadhi ya vijana wamekuwa wakilalamika kukosa kazi ilhali hawaonyeshi dalili zozote za kujituma na badala yake wamekuwa wakiilalamikia Serikali kutowapa kazi.
“Wakati mwengine baadhi ya vijana wenzangu huniona kama mtu nilietumwa na kuwa na maslahi----mimi ni mwanaharakati wa maendeleo kwa vijana wenzangu na ndio maana naumia sana kuwaona wakiwa hawana kazi na kujikalia katika magenge na baraza za soga” alisema Nassour
Aliwataka kufanya kazi kwa bidii na Serikali kuwaona na kuweza kuwasaidia katika mipango yao ya kujikomboa na umasikini na kuwa msaada kwa wengine ambao wamekuwa wakikata tamaa ya maisha.
                                                   Mwisho

No comments:

Post a Comment