SIMULIZI
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA
BABU, SEHEMU YA (1)
Jina langu ni Kassim Fumbwe.
Nina umri wa miaka ishirini na minane. Mkazi wa jiji la Dar es Salaam.
Wazazi wangu walifariki dunia
wakati nikiwa mdogo. Nakumbuka tulikuwa tunasafiri kutoka Dodoma kuja Dar, basi tulilokuwamo
likagongana na lori uso kwa uso.
Baba yangu na mama yangu
pamoja na abiria wengine kadhaa walifariki hapo hapo. Mimi nikanusurika.
Nakumbuka nilipata jeraha
dogo tu kwenye mkono wangu wa kushoto baada ya kukatwa na vioo vya dirisha
vilivyokuwa vimevunjika.
Babu yangu mzaa baba, Mzee
Fumbwe Limbunga alipopata habari ya ajali ile alitoka Dar kwa gari lake akaja
Morogoro. Majeruhi wa ajali ile tulikuwa tumelazwa katika hospitali ya
Morogoro.
Mimi sikuwa nimeumia sana lakini kwa vile
wazazi wangu walikuwa wamefariki ilibidi nibaki hapo hospitali ili niweze kutambuliwa
na kuchukuliwa na ndugu zangu.
Babu alipokuja akanichukua.
Aliichukua pia miili ya marehemu baba yangu na mama yangu.
Siku ya pili yake habari za
ile ajali zilichapwa kwenye magazeti. Kila gazeti lilikuwa limechapa picha
yangu ikielezea jinsi nilivyonusurika kimiujiza.
Baada ya msiba huo, nikawa
ninaishi na babu. Babu yangu alikuwa tajiri lakini alikuwa hana mke. Aliachana
na mke wake tangu alipokuwa kijana na hakutaka kuoa tena.
Kwa hiyo alinitafutia
mtumishi wa kunihudumia kwa kila kitu ikiwa ni pamoja na kunipeleka shule.
Nilipoanza masomo ya sekondari babu akanihamisha katika nyumba yake nyingine.
Zote zilikuwa Tegeta lakini zilikuwa mitaa tofauti.
Ile nyumba aliyonihamishia
upande mmoja ilikuwa na mpangaji, upande mwingine ndio niliokaa mimi.
Kila jumatatu babu alikuwa
akinipa pesa za kutumia kwa wiki nzima. Baadhi ya siku nilikuwa ninapika
mwenyewe nyumbani na siku nyingine nilikuwa ninakula kwenye mikahawa..
Baada ya kumaliza masomo yangu
nilipata kazi Morogoro. Lakini babu alinishauri niache kazi nifanye biashara.
Aliponipa mtaji nikaacha kazi. Nilifungua maduka matatu ya vifaa vya ujenzi
pale Morogoro.
Yalikuwa maduka makubwa.
Niliajiri karibu wafanyakazi kumi na watano. Kila duka lilikuwa na wafanyakazi
watano. Biashara ilianza vizuri. Baada ya miezi sita tu nikaja Dar kununua gari
la kutembelea.
Sasa nikawa nafikiria
kutafuta mke nioe. Sikumaliza hata mwaka mmoja ile kasi ya biashara ikaanza kupungua.
Maduka yangu yaliyokuwa yamejaa vitu yakaanza kuwa matupu. Haukupita muda mrefu
nikaanza kupunguza wafanya kazi. Mwisho kila duka likabaki na mfanyakai mmoja.
Nilifikia mahali nikahisi
kuwa pengine sikuwa na nyota ya kujiajiri. Nikajuta kuacha kazi niliyokuwa nayo
mwanzo. Ikabidi yale maduka mawili niyafunge nikabaki na duka moja ambalo
nililisimamia mwenyewe. Duka hilo
nalo likafilisika nikalifunga. Nikawa sina kazi.
Nilifikiria kwenda kumueleza
babu ili anipe mtaji mwingine lakini nilishindwa kwani nilijua asingekubali
tena kunipa pesa zake. Nikauza lile gari. Siku ile nauza gari babu akanipigia
simu na kunijulisha kuwa alikuwa anaumwa na alikuwa amelazwa katika hospitali
ya Aga Khan.
Nikapanda basi kuja Dar.
Nilipofika Dar nilikwenda moja kwa moja katika hospitali katika hospitali ya
Aga Khan..
Vile nafika tu na babu yangu
anakata roho. Hata sikuwahi kuzungumza naye lolote.
Kifo chake babu
hakikunishitua sana kwa sababu alikuwa na mali
na mimi ndiye ambaye ningemrithi.
Dereva wake nilimkuta hapo
hapo hospitali, alinieleza kuwa Mzee Fumbwe alianza kuumwa siku tatu zilizopita
lakini usiku uliopita ndio alizidiwa. Presha ilikuwa juu na sukari ilipanda.
Hali ikawa mbaya.
Kwa kushirikiana na dereva huyo
tuliuchukua mwili wa Mzee Fumbwe siku ya pili yake kwa ajili ya maziko. Baada
ya maziko nikaanza mchakato wa kukagua mali za marehemu.
Nilichokuwa nikikifahamu awali
ni kuwa babu yangu alikuwa na maduka kadhaa Dar es Salaam. Alikuwa na vituo vitatu vya
mafuta na malori sita.
Pia alikuwa na nyumba alizokuwa
amezipangisha ambazo sikujua zilikuwa ngapi.Nilikuwa nikijua nyumba mbili tu,
ile aliyokuwa akiishi yeye na ile niliyokuwa nikikaa mimi kabla ya kuhamia
Morogoro.
Mali zake nyingine alikuwa akizijua yeye mwenyewe.
Niliingia chumbani mwake nikafungua makabati na kuanza kupekuwa nyaraka zake
alizozihifadhi kwa lengo la kutambua mali hizo.
Jambo ambalo lilinishangaza,
nilikuta hati ya nyumba yake aliyokuwa akiishi na hati za gari alilokuwa
akilitumia. Sikukuta hati wala nyaraka nyingine zinazohusu mali zake.
Wakili wake nilikuwa
namfahamu. Nikaenda ofisini kwake barabara ya Samora na kumjulisha kuhusu kifo
cha mteja wake.
“Oh mzee amefariki?”
akaniuliza kwa mshituko.
“Amefariki juzi, tumemzika
jana”
“Alikuwa mgonjwa?”
“Wakati anaumwa mimi nilikuwa
Morogoro. Juzi akanipigia simu yeye mwenyewe akaniambia kuwa anaumwa na
amelazwa hospitali. Muda ule ule nikapanda gari kuja kumuona. Mpaka nafika Dar
nikakuta ameshafariki”
“Oh pole sana. Aliwahi kuniambia kuwa mwanawe
alifariki dunia”
“Mwanawe ni baba yangu.
Alifariki mimi nikiwa mdogo”
“Kwa hiyo mrithi wake utakuwa
wewe. Kwa maana hakuwahi kuandika wasia wowote ila alinieleza kuwa hakuwa na
ndugu wala mtoto mwingine isipokuwa mjukuu”
Wakili alipoleta suala la
urithi akawa amenirahisishia tatizo lililokuwa limenipeleka kwake.
“Hilo ndilo lililonileta kwako”
“Umefanya vizuri kuja kunifahamisha.
Sasa unatakiwa ufungue mirathi mahakamani ili uweze kumrithi babu yako”
“Kabla ya kufungua mirathi
kuna suala moja ambalo limenishitua sana”
“Suala gani?”
ITAENDELEA kesho hapahapa tangakumekuchablog, Usikose uhondo huu nini kitaendelea
No comments:
Post a Comment