SIMULIZI
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA
BABU 2
ILIPOISHIA
“Kuhusu mali za marehemu. Babu yangu
alikuwa tajiri lakini katika kumbukumbu zake nimekuta hati ya nyumba moja
aliyokuwa anaishi pamoja na hati ya gari alilokuwa akitumia”
“Sasa kama hakuna hati wala
nyaraka zozote utazijuaje mali
zake nyingine?”
“Kwanza
hizo nyaraka zitakuwa zimekwenda wapi?”
“Nenda kapekue vizuri.
Inaweekana aliuza baadhi ya mali
zake”
Kutokana na ushirikiano
alionipa wakili huyo kutafiti mali
alizokuwa akimiliki marehemu babu yangu, tuligundua kuwa mpaka marehemu
anafariki duniani hakuwa na mali
yoyote aliyoacha zaidi ya nyumba aliyokuwa akiishi pamoja na gari lake.
Hata baada ya kufungua mirathi mahakamani na kuthibitishwa kuwa mimi ndiye mrithi wa
marehemu, sikukuta pesa ya maana katika akaunti yake ya benki. Akaunti yake
ilikuwa na shilingi elfu kumi tu.
SASA ENDELEA
Kwa Kweli mimi na wakili wa
marehemu tulishangaa sana.
Kila mtu alikuwa akifahamu kuwa Mzee
Fumbwe alikuwa ni miongoni mwa matajiri wazawa wa jiji la Dar es Salaam. Jinsi
alivyokufa akiwa masikini ni jambo ambalo halikueleweka.
Katika utafiti nilioufanya
baadaye niligundua kuwa Mzee Fumbwe alikuwa ameuza baadhi ya mali zake zikiwemo nyumba na vituo vya mafuta siku chache kabla ya
kufariki dunia.
Lakini uchunguzi wangu
ulishindwa kubaini marehemu alipeleka wapi pesa zake kwani benki hakukuwa na
kitu.
Kwa kipindi cha karibu wiki
mbili nilikuwa nikiendelea kufanya utafiti kwenye nyaraka za marehemu ili
kupata uhakika kwamba kweli babu hakuwa na kitu.
Nikaja kugundua kitabu cha
kumbukumbu cha marehemu ambacho alikuwa akiandika mambo yake. Nilipopekua karasa
na kitabu hicho niliona kulikuwa na watu ambao walikuwa wakifanya biashara na
babu na kwamba babu alikuwa akiwadai wafanyabiahara hao pesa nyingi.
Nilikuta majina ya wafanya
biashara wanne. Katika watu hao ni mmoja tu aliyekuwa akiishi hapo Dar, wengine
walikuwa wakiishi nchi za nje. Mwenyewe aliandika kama
ifuatavyo
Abdul Baraka wa Mbezi Dar es Salaam. Namdai dola
milioni moja.
(Aliandika na namba ya simu
yake)
Isaac Chusama wa Harare Zimbambwe. Namdai
dola milioni mbili na laki tano.
(Aliandika namba ya simu yake
na mtaa aliokuwa anaishi)
Benjamin Muhoza wa Gaborone Botswana.
Namdai dola milioni moja na laki tano.
(Aliandika namba ya simu yake
na mtaa aliokuwa akiishi)
Dumessan Dube wa Cape Town Afrika Kusini.
Namdai dola milioni tatu.
(Aliandika namba ya simu yake
na mtaa aliokuwa akiishi)
Hapo nikajua kuwa marehemu
babu alikuwa akidai fedha nyingi kwa watu waliokuwa wakiishi nje ya nchi.
Kitabu hicho cha kumbukumbu
kiliendelea kunjulisha siri ya babu ambayo nilikuwa siifahamu. Babu alikuwa
akifanya biashara ya madini. Tena madini ya Tanzanite na kwamba alikuwa
akiwauzia wafanya biashara hao.
Kumbukumbu za nyuma za kitabu
hicho zilionesha ameshawahi kuwauzia madini wafanyabiashara hao kwa thamani ya
dola ya Kimarekani. Na kwamba alikuwa akilipwa kwa awamu.
Nikajiuliza babu alikuwa
akipata wapi madini mengi kiasi cha kumpatia mamilioni hayo ya dola?
Swali jingine nililojiuliza
ni wapi babu yangu alikokuwa anaficha fedha hizo, isingewezekana afe akiwa hana
kitu.
Niliitafuta paspoti yake na
nikaipekua. Nikagundua kuwa mara kwa
mara alikuwa akitembelea Zimbabwe,
Botwana na Afrika kusini.
Nilipopekua zaidi kwenye
mafaili yake nikaipata mikataba yake na wafanya biashara hao. Alikuwa amelipwa
pesa nusu na nusu alikuwa akiwadai. Tarehe
ya kuwafuata wafanya biashara hao wammalizie deni lake ilikuwa
imeshapita.
Nikajiambia kama nitafanikiwa
kupata fedha hizo nitakuwa tajiri mkubwa hapa Dar kwani kwa pesa za Kitanzania
dola hizo zilikuwa ni mabilioni ya shilingi.
Kwa vile marehemu aliandika
namba za simu zao, nikaanza kumpigia Abdul Baraka aliyekuwa hapo Dar.
Nilimpigia kwa kutumia laini ya marehemu. Simu yake haikupatikana.
Nikampigia Isaac Chusama wa Harare. Simu iliita kwa sekunde chache kisha ikapokelewa.
Nikashangaa kusikia sauti
ikinisalimia kwa Kiswahili.
“Habari yako Bwana Fumbwe?”
“Nzuri lakini mimi siye Bwana
Fumbwe. Bwana Fumbwe amefariki wiki tatu zilizopita, mimi ni mjukuu wake.
Naitwa Kassim Fumbwe”
“Heh! Mzee Fumbwe amefariki?”
“Amefariki. Hivi sasa ni wiki
tatu zimeshapita”
“Oh pole sana”
“Asante. Sasa kumbukubu za babu
zinaonesha kwamba alikuwa akikudai dola milioni mbili na laki tano. Na mkataba
wa makubaliano yenu ninao hapa”
“Ndio ni kweli ananidai”
“Kwa vile tarahe ya kumlipa
imeshapita, ninataka nije Harare
unipatie hizo fedha. Mimi ndio mrithi wake”
“Sasa nitakuaminije Bwana
Fumbwe?”
“Nitakuja na hati zote
zikiwemo hati za mahakama zinazoonesha kwamba mimi ndiye mrithi wa marehemu,
cheti cha kifo chake na mikataba ya makubaliano yenu”
Pakapita kimya cha sekunde
kadhaa kabla ya sauti ya mtu wa upande wa pili kusikika tena.
“Unatarajia kuja lini?”
“Baada ya siku mbili tatu.
Hivi sasa ninajiandaa kwa safari”
“Utakapokuja utanijulisha”
“Sawa”
Isaac akatangulia kukata
simu.
Hapo hapo nikampigia Benjamin
Muhoza. Nilishukuru naye alipopokea simu.
ITAENDELEA kesho usikose nini kitajiri katika Uhondo huu
No comments:
Post a Comment