Monday, March 28, 2016

ACHENI KILIMO CHA BANGI, MAJIMAREFU AWAMBIA WAKULIMA



Tangakumekuchablog
Korogwe, MBUNGE wa  jimbo la Korogwe Vijijini (CCM) Stivin Ngonyani maarufu Majimarefu amewataka wananchi wanaoishi milimani kuacha  kulima kilimo cha bangi na badala yake kulima kilimo cha chakula.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa wananchi kata ya Makumba na Magoma jana, Majimarefu aliwataka wananchi kuitumia ardhi hiyo kwa kulima mazao na nafaka na kuacha kilimo cha bangi ambacho hakina faida.
Aliwataka wananchi hao kutambua kuwa  uwezekano wa kitisho cha njaa unaweza kuikumba Wilaya ya Korogwe endapo wakulima  hawataacha kulima bangi  na kuitumia ardhi kwa matumizi bora .
“Ndugu zangu wakulima wa kijiji hiki na vyenginevyo ambavyo vimezungukwa na milima mikubwa , sina uhakika ila nasikia kuna wakulima  wanalima bangi na kuacha kulima mahindi” alisema Majimarefu na kuongeza
“Sitokuwa tayari kuona wananchi wananyemelewa na balaa la njaa kwa sababu tu ardhi yao kuna kikundi kinalima bangi, nitakuwa mmoja wa makamanda wa kufanya operesheni usiku mchana” alisema
Akizungumzia juu ya wajibu wa wananchi kuhoji mapato na matumizi, Mbunge huyo aliwataka kuwepo ushirikiano wa wananchi na viongozi wa Serikali ili mapato yanayopatikana maeneo yao yatumike kwa  njia sahhi.
Alisema kuna baadhi ya viongozi wenye dhamana wanaacha kuwasomea mapato na matumizi wananchi hivyo kuzusha mgogoro jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo.
Alisema kutowasomea wananchi mapato na matumizi ni njia za ufisadi na kuwanyonya wananchi wanaolipa  kodi zao hivyo kuwataka wenye tabia hiyo kuacha mara moja na kuwa wawazi.
“Mapato na matumizi ni wajibu wa viongozi wa Serikali kuwasomea wananchi mapato na matumizi , kuacha kuwasomea kunaonyesha kuna ufisadi ambao haukubaliki” alisema Majimarefu
Aliwataka wananchi na viongozi wa Seikali kushirikiana ili pesa zinazopatikana ziweze kutumika katika kazi za maendeleo ikiwa na pamoja na kupeana taarifa ambazo zitasukuma kasi ya maendeleo.
                                                Mwisho

  Mbunge wa jimbo la Korogwe Vijijini (CCM) Stivin Ngonyani maarufu Majimaefu, akiwahutubia wananchi wa kata ya Makumba katika mkutano wa wananchi kusikiliza kero zinazowakabili ndani ya kata hiyo.




Wananchi kata ya Magoma Wilayani Korogwe Mkoani Tanga, wakimlaki Mbunge wao Stivin Ngonyani maarufu Majimarefu alipowasili kwa mkutano wa kuwashukuru na kusikiliza kero zinazowakabili

No comments:

Post a Comment