HADITH hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha cha Tiba Asilia cha Mkombozi Sanitarium Clinic Tanga, Mkombozi ni mabingwa wa kutibu magonjwa sugu na yaliyoshindikana, Mkombozi wako na mashine za kisasa za kipimia mwili mzima .Mkombozi wamehamia barabara ya 12 Ngamiani Tanga mkabala na Ofisi za Mabasi yaendayo Moshi, Arusha hadi Singida, simu 0654 361333
Tangakumekuchablog
Nilikuwa bado
kijana na umri wangu ulikuwa wastani wa miaka ishirini na mitano. Sikuwa
nimepata elimu ya kutosha baada ya wazazi wangu wote wawili kufariki dunia
wakati nikiwa mdogo.
Nilianza maisha
ya kuhangaika tangu nikiwa mdogo baada ya wazazi wangu hao kufariki dunia.
Nilianza kuajiriwa kazi ndogondogo ili nipate pesa za kujikimu na nilipofikia
umri wa miaka kumi na minane ndipo nilipopata ajira rasmi.
Ajira yenyewe ni
ya kazi ya ulinzi. Niliajiriwa katika kampuni moja ya ulinzi, kazi yangu ikiwa
ni kulinda zamu usiku. Kwa vile sikuwahi hata kupitia mafunzo ya mgambo
nilifundishwa hapo hapo jinsi ya kutumia bunduki na jinsi ya kukabiliana na
wezi na majambazi.
Lindo langu la
kwanza lilikuwa katika eneo la Gofu. Unapoingia katika jiji la Tanga eneo hilo unakutana nalo mwanzo
mwanzo. Halikuwa eneo la makazi ya watu isipokuwa viwanda vidogo vidogo na
maghala ya makampuni mbalimbali.
Wakati wa mchana
eneo hilo
linakuwa limechangamka kwa sababu kunakuwa na pilikapilika za wafanya kazi
lakini ikifika usiku mahali hapo hupooza na kuwa kimya kabisa.
Mimi nilikuwa
ninalinda ghala la kampuni moja ambayo wamiliki wake walikuwa ni Waasia.
Ghala hilo lilikuwa liko mbali kidogo na maghala mengine na
unapoliacha ghala hilo
unaelekea katika maghala ya zamani ambayo yalikwa hayatumiki tena.
Nilikuwa
ninaingia kazini saa 12 jioni na kutoka saa 12 asubuhi. Kama si dhiki ya
kimaisha niliyokuwa nayo nisingekubali kwenda kukesha usiku katika eneo hilo kwani lilikuwa linatisha sana.
Siku za mwanzo
mwanzo nilipoanza kazi nilikuwa na hofu na wasiwasi lakini kadiri siku
zilivyoendelea hofu ilinipungua.
Nikawa najiambia
pengine ni kwa sababu sijaizoea kazi yenyewe ndiyo maana ninapata hofu, lakini
nikiizoea hofu itaondoka.
Nilipata
mshahara wangu wa kwanza ukanisaidia kununua vitu vidogo vidogo vya
chumbani mwangu. Nilikuwa nimepangisha chumba katika eneo la Chumbageni ambalo
halikuwa mbali sana
na lilipokuwa lindo langu. Ofisi zetu ndizo zilikuwa katikati ya jiji.
Siku moja
nilipokuwa katika lindo langu nikirandaranda huku na huku nilimuona
msichana mmoja akipita katika barabara iliyokuwa karibu na lile ghala
ninalolinda
Nilishituka kwa
sababu kwanza ilikuwa ikikaribia kuwa saa nane usiku. Nilijiuliza yule msichana
alikuwa anatoka wapi usiku ule?. Pili nilishituka kwa sababu mahali alikokuwa
anaelekea hakukuwa na makazi ya watu bali kulikuwa na maghala ya zamani
yasiyotumika tena na viwanda vilivyokufa.
Nikasimama na
kumuangalia. Kwa vile barabara ilikuwa mbali kidogo, msichana huyo hakuniona au
pia inawezekana aliniona lakini hakunijali. Alikuwa akitembea kwa hatua
za haraka lakini bila kuonesha kuwa alikuwa na wasiwasi.
Alikuwa amevaa
vazi jeupe la aina ya dera lililoficha kabisa miguu yake na alijitanda ushungi
mrefu uliofanana na rangi ya dera alilovaa.
Wakati akitembea
kulikuwa na mlio wa ko! ko! ko! uliokuwa ukisikika kwenye miguu yake. Nikahisi
alikuwa amevaa viatu vya mchuchumio ambavyo vilikuwa vikitoa mlio kila
alipopiga hatua.
Kwa vyovyote
vile kitendo cha msichana huyo kuwa peke yake usiku huo na akitembea kwa
kujiamini bila kuonesha wasiwasi kilionesha ujasiri.
Punde tu akawa
amelipita eneo hilo
na kupotea kwenye kiza. Hata hivyo niliendelea kuusikia ule mlio wa viatu vyake
ko! ko! ko! japokuwa mwenyewe sikuwa nikimuona tena.
Nikawa najiuliza
msichana yule alikuwa nani, anakwenda wapi na anatoka wapi. Lakini sikupata
jibu.
Usiku wa siku ya
pili yake muda kama ule nikaanza kuisikia tena
ile sauti ya viatu ko! ko! ko!. Nilipotupa macho barabarani nikamuona yule
msichana akitokea kwa mbali. Alikuwa amevaa mavazi yaleyale na akitembea kwa
mwendo wake uleule wa harakaharaka lakini bila kuonesha kuwa alikuwa na
wasiwasi.
Wakati huo
nilikuwa nimeketi kwenye kiti baada ya kuchoka kurandaranda. Nikawa namtazama.
Alipita karibu na lile lindo kisha akaendelea na safari yake. Punde tu akapotea
kwenye kiza.
“Huyu msichana
anakwenda wapi saa hizi?” nikajiuliza.. Hata hivyo kama
ilivyokuwa usiku wa jana yake sikupata jibu.
Ilipofika saa 12
asubuhi nilibadilishana lindo na mlinzi mwenzangu, nikarudi nyumbani.
Kama kawaida yangu
ya siku zote nilipofika nyumbani nilioga kisha nikalala. Sikuamka hadi saa sita
mchana. Nilivaa nguo zangu za kiraia, nikaenda katika mkahawa uliokuwa jirani
na nyumba niliyopanga chumba. Nikala ugali na maharage. Nilikuwa natamani nile
nyama au samaki lakini uwezo nilikuwa sina..
Kila inapofika
saa kumi jioni hununua kabisa chakula ambacho nitakula usiku. Chakula hicho hukiweka
kwenye chombo kinachotunza joto. Kwa hiyo ninapokwenda kazini jioni ninakuwa na
mfuko wangu wenye chakula changu cha usiku pamoja na chupa ya maji.
Lakini si chupa
ya maji safi
yanayouzwa madukani bali ni maji ya bomba ambayo huyatia kwenye chupa tena bila
kuyachemsha.
Chakula
ninachokwenda nacho hukila inapofika saa tatu usiku halafu naendelea na kazi
yangu. Sikuwa nikivuta sigara kama ilivyo kwa walinzi wengine ambao
huvuta sigara sana
usiku kwa sababu ya baridi.
Nilikuwa na koti
langu la mvua ambalo hulivaa usiku ili kujikinga na baridi. Ninapovaa koti hilo huwa sisikii baridi.
Tangu
nilivyofika katika lindo hilo
saa 12 jioni, niliona dalili za kunyesha mvua kwani wingu lilikuwa
limejikusanya na kulikuwa na upepo mkali.
Hata hivyo
hakukunyesha mvua lakini hali ya hewa haikuwa nzuri.
Ilipofika saa
nane usiku nikausikia tena ule mlio wa viatu vya yule msichana, ko! ko! ko!.
Nilipotupa macho barabarani nikamuona. Alikuwa amechanganya mwendo kwani matone
ya mvua yalikuwa yameanza kuanguka
Msichana huyo
alipokuwa karibu na lindo langu, mvua ikaanguka kwa kishindo. Nikamuona anakuja
mbio kuelekea kwenye lile ghala kujificha mvua.
Alipofika
alipitiliza moja kwa moja hadi karibu na lango la ghala hilo mahali ambapo nilikuwa nimesimama. Mvua
ilikuwa hainipati kwa sababu palikuwa pamepauliwa bati.
‘Asalaam
alaykum’ akanisalimia.
Nilikuwa Mkristo
lakini nilikwishaizoea salamu hiyo ya kiislamu.
Nikamuitikia.
‘Alaykumu salaam’
Alinitupia jicho
mara moja tu kisha akauelekeza uso wake chini. Alikuwa amejikunja kwa sababu ya
baridi na nguo zake zilikuwa zimetota kwa mvua.
Ingawa alinitazama
mara moja tu lakini uso wake niliuona. Alikuwa na pozi la kisomali. Na kama hakuwa msomali alikuwa chotara wa kiarabu. Alikuwa
mweupe mwenye nyusi zilizopakwa wanja. Macho yake yalikuwa makubwa yenye mboni
za kijivu, pia aliyakoleza wanja mzito na kuwa na mvuto wa kipekee.
Midomo yake
alikuwa ameipaka rangi ya waridi. Ilikuwa na papi za ukubwa wa wastani. Alikuwa
amevaa mkufu wa dhahabu kwenye shingo yake.
Mara moja eneo hilo likaenea hewa ya
manukato ya udi wa mawaridi na manukato ya Al-uud na marashi alivyokuwa
amefukiza nguo zake.
‘Hujambo?’
Nilijaribu kumsemesha ili niweze kumuuliza, anatoka wapi na anakwenda wapi.
‘Sijambo’
akanijibu bila kunitazama. Alikuwa akitetemeka kwa baridi iliyompata.
‘Pole sana. Unatoka wapi saa
hizi?’
Endelea
kufuatilia muendelezo wa hadithi hii hapo kesho hapahapa Tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment