Wednesday, March 9, 2016

MAJIMAREFU ATAKA KUKOMESHWA WATOTO KUSOSESHWA SHULE



Tangakumekuchablog
Korogwe, MBUNGE wa jimbo la Korogwe Vijijini, Stivin Ngonyani (CCM) maarufu Profesa Majimarefu, amewataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao shule na kuacha kuwatumikisha kazi na kuwafungia ndani.
Akizungumza katika mikutano yake ya kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kwa mara ya pili kata ya Mswaha na Magila Gerezani, Majimarefu alisema kuna baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwatumikisha watoto wao katika kazi za mifugo na kilimo.
Alisema tabia hiyo imekuwa ikiwanyima watoto kupata elimu jambo ambalo linaweza kuwavurugia maisha yao mbeleni hivyo kuwataka wazazi na walezi kuacha kuwatumikisha badala yake wakupeleka shule.
“Tunatambua kuwa maeneo yetu kilimo na mifugo ndio tegemeo la watu wengi, lakini neema hii tuliojaliwa isiwe sababu ya watoto wetu kuwakosesha elimu tutambue msingi wa maisha ni elimu” alisema  na kuongeza
“Kama tutawakazania watoto wetu katika elimu vijiji vyetu vitabadilika na kuwa vyenye maendeleo, tuko na changamoto za miundombinu ya barabara na huduma nyingi za kijami ikiwemo afya na elimu” alisema
Akizungumzia kuongezeka kwa migogoro ya ardhi ya wafugaji na wakulima, Mbunge huyo alisema maeneo yote yenye migogoro Serikali imedhamiria kuimaliza kwa kuangalia chanzo cha mgogoro huo.
Alisema kuna baadhi ya maeneo migogoro imekuwa ikiundwa na watu hivyo kuwataka kuacha kufanya hivyo na kusema kila penye mgogoro wa ardhi uchunguz utafanyika.
“Kuna migogoro ya ardhi mingi imekuwa ya kutengenezwa na watu wenye tamaa ya pesa na kusahau maslahi ya wananchi, mimi niseme kila penye mgogoro Serikali itafika na kuchunguza na ambae ni chanzo atawajibishwa” alisema Majimarefu
Alisema wafugaji na wakulima kila mmoja kujua mipaka yake na kuepuka muingiliano wa kupitisha mifugo ili kila mmoja kuiendeleza sekta yake lengo likiwa ni kujiletea  maendeleo.
Mbunge huyo aliwashukuru wananchi hao kwa kumchagua kwa mara ya pili kuwa Mbunge wao na kuwaahidi kuwa nao bega kwa bega na hivyo kuwataka ushirikiano ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
                                             Mwisho


No comments:

Post a Comment