Friday, March 25, 2016

AFRICAN SPORTS MAJANGA



Tangakumekuchablog
Tanga, KOCHA Mkuu wa African Sports, Ramadhani Oluto, amewashushia lawama wachezaji wake kwa kuruhusu kipigo cha mabao mawili kutoka kwa Toto African nyumbani na kusema ni rehema za Mungu tu zitakazowabakisha ligi kuu.
Akizungumza mara baada ya kumalizika mpira uwanja wa Mkwakwani juzi, Oluto alisema wachezaji wake walicheza mpira mbovu kipindi chote cha dakika 45 cha kwanza na walipozinduka walikuwa wameshalala mabao mawili.
Alisema hakufurahishwa na mpira ambao wameucheza mbele uwanja wa nyumbani na kusema amehuzunishwa kwani mchezo huo hawakutakiwa kupoteza ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kubakia ligi kuu msimu ujao.
“Niseme wazi kuwa wachezaji wangu leo wamecheza ovyo sana na sikufurahishwa na uchezaji wao, kipigo cha mabao mawili nyumbani ni aibu na fedheha” alisema Oluto na kuongeza
“Kama wachezaji wangu hawatabadilika aina ya uchezaji uwanjani ligi inaweza kutuwia vigumu kwani ukipoteza mchezo mmoja na gharama ambayo huwezi kuifidia” alisema
Aliwataka wakazi wa Tanga na washabiki wa timu hiyo kuwaombea dua ili kuweza kushinda mechi zilizo mbele yao na kuendelea kushiriki ligi msimu uajo.
Kwa upande wake kocha wa Toto Africans ya Mwanza , John Tegete, alisema kipigo walichotoa cha bao mbili ni kulipiza kisasi cha kaka zao Coastal Union walichokipata mwanzo mwa juma hili.
Alisema mchezo huo ni kama miujiza kwani matokeo yanafanana na mchezo wa Coastal kwani nao African Sports baada ya kuwafunga mabao mawili ya harakahara walichanganyikiwa na kupoteza muelekeo.
“Huu mchezo ni kama ule tuliocheza na kaka zao Coastal Union kwani wao walitufunga mabao mawili ya harakahara na kutulewesha, kipindi cha pili tulizinduka na kupata bao moja kama ilivyotokea leo hii” alisema Tegete
Alisema awali walikuwa na hofu ya kupoteza mchezo kama ilivyokuwa kwa Coastal hasa ikiwa tulikuwa ugenini na kucheza na timu ambayo iko na changamoto ya kushuka daraja.
Alisema wachezaji wake walijituma na kuonyesha morali wa ushindi ila kipindi cha pili African Sports walicharuka na kuliandama lango lao na kubahatika kuambulia goli moja.
Alisema jambo ambalo wanajivunia ni kuwa wao wataendelea kubaki ligi kuu msimu ujao na kusema kuwa hiyo haimaanishi kuwa wameridhika badala yake ni kuhakikisha kila mchezo iliyosalia wanaibuka na ushindi.
                                            Mwisho

 Wachezaji wa African Sports ya Tanga wakilishambulia lango la Toto African ya Mwanza wakati wa mchezo ligi kuu Tanzania Bara uwanja wa Mkwakwani juzi. Toto African ilishinda 2  ,  1.









Mshambuliaji wa Toto African ya Mwanza, William Kiranzi akiwania mpira na beki wa African Sports ya Tanga, Ayoub Saleh, wakati wa mchezo ligi kuu Tanzania Bara uwanja wa Mkwakwani juzi, Toto ilishinda mabao 2  ,  1.

No comments:

Post a Comment