Monday, March 21, 2016
WACHIMBAJI WA MADINI KALALANI WAMLILIA MAJIMAREFU
Tangakumekuchablog
WANAWAKE wanaojihusisha na shughuli za uchimbaji madini waliopo kata ya Kalalani Wilayani Korogwe Mkoani Tanga wamemuomba mbunge wao Stephen Ngonyani kuangalia uwezekano wa kuwapatia semina ya kuwajengea uwezo hatua ambayo itawawezesha kuendesha utendaji kazi wao kwa tija.
Wanawake hao wachimbaji wadogo wadogo walitoa ombi hilo juzi wakimweleza mbunge wao kuwa ukosefu wa elimu juu ya shughuli wanayoendelea kuifanya hawajaweza kupiga hatua yoyote ya maendeleo ambapo sasa wamemuomba kiongozi wao huyo kuwasaidia ili kuweza kunufaika.
Anna Julius ambaye ni mwenyekiti wa UWT kata ya Kalalani alisea kwamba elimu ya masuala ya madini ina umuhimu mkubwa kwa wananchi wa kada yao ambao wengi wao wamelazimika kuingia kwenye shughuli hiyo kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali hususani ulezi ndani ya familia zao.
Aidha mwanamama huyo aliendelea kusema kwamba sababu nyigine iliyochangia wao kuingia kwenye shughuli ya uchimbaji wa madini ni baada ya baadhi ya waume zao kuzikimbia familia kuhamia sehemu nyingine zinazoelezwa kuwa na mfumuko wa madini wakiamini kuwa wanaweza kupata mafanikio.
Akijibu ombi hilo Mbunge Ngonyani almaarufu Profesa Maji Marefu aliwaahidi wanawake hao kuwatatulia kero yao hiyo kwa kuhakikisha kuwa halmashauri inawafikishia maafisa maendeleo ili kuwapatia elimu inayohitajika wananchi hao wa kata hiyo mpya ya Kalalani iliyotokana na Mashewa.
Hata hivyo mbunge Maji Marefu alitanabaisha kwamba anayafahamu matatizo yanayowasibu wananchi wa Kalalani akitaja Umeme,maji huku kubwa zaidi ikiwa ni ukosefu ardhi ya kutosha kwa ajili ya wachimbaji wadogo wadogo ambao kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakihangaika pasipo maeneo.
Kutokana na ombi hilo Maji Marefu licha kuahidi kushughulikia suala hilo la wanawake hao pia alisema madini yana umuhimu mkubwa ambapo aliwataka wananchi wa Kalalani kumuandalia andiko kuhusu masuala ya madini ili kuweza kulipeleka kwa waziri wa madini Sospeter Mhongo.
Kwa upande mwingine Maji Marefu alisema kuwa masuala ya wakulima na wafugaji wakati wote atajitahidi kuyapatia utatuzi kwa misingi ya haki akiwaahidi wananchi hao wa Kalalani kuwa hatawaangusha na kutanabaisha kuwa serikali inawategemea mchango wa sekta hizo mbili.
Mbunge Maji Marefu katika ziara yake hiyo alitumia mkutano huo wa hadhara kujibu kero kuhusu josho la mifugo akiwaahidi wafugaji kuwa atakwenda halmashauri ya wilaya kumuona mkuu wa idara husika ili kuona ni jinsi gani anavyoweza kulishughulikia tatizo hilo la ukosefu wa josho kwa ajili ya wafugaji.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa Tangakumekuchablog
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment