HADITHI hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, Candle ni mabingwa wa kufalisha wanafunzi mashuleni na kutoa vipaji pamoja na wanaojiendeleza kielimu makazini. Candle wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
MWANAMKE ALIYENICHUNUKA 17 na Faki A Faki , 0713 340572
ILIPOISHIA
Geti la nyumba lilifunguka lenyewe kutokana na rimot iliyokuwa mbele ya
gari. Msichana akaliingiza gari ndani. Gari hilo
lilipoingia geti hilo
likajifunga tena.
Msichana huyo alisimamisha gari hilo
mbele ya mlango wa nyumba na kushusha vioo na kuniangalia kwa haiba na nikageuza macho yangu upande wa kioo changu kwa aibu..
“Tushuke!” akaniambia huku akifungua mlango na kushuka.
Na mimi nikashuka.
Msichana alitoa funguo na kufungua mlango wa nyumba.
“Karibu ndani Alfred” akaniambia huku akitangulia kuingia ndani na mimi
nikamfuata nyuma.
Ni vyema nikiri kuwa katika maisha yangu tangu nizaliwe sijawahi kuingia
ndani ya jumba zuri kama lile.
Nilijikuta nimeganda pale kwenye mlango nikiangalia humo ndani jinsi
mlivyokuwa mnapendeza na kujaa vyombo vya thamani. Niliona kama vile nikiingia,
viatu vyangu vitachafua.
“Mbona umesita kwenye malango?” Msichana akaniuliza alipoona nimesimama
kwenye mlango.
SASA ENDELEA
“Ngoja nivue viatu”
“Hapana. Ingia tu na viatu vyako. Mbona mimi sikuvua?”
Nikaingia lakini nilitembea kwa kunyata huku shingo yangu ikizunguka kama feni kuangalia huku na huku. Kila kitu nilichokiona
nilikishangaa.
“Karibu ukae” Msichana akniambia huku na yeye akiketi kwenye
sofa.
“Asante”
Nikakaa kwenye sofa mojawapo.
“Alfred naona umeshangaa sana”
Sauti ya yule msichana ilinishitua.
Badala yake nilitoa kicheko cha
uongo kwani ni kweli nilikuwa nimeshangaa.
Msichana naye akacheka na kuniambia.
“Hapa ndio kwangu. Karibu sana”
“Mbona kuko kimya. Unaishi na nani?”
“Ninaishi peke yangu, ndio maana nilitaka mlinzi”
Kauli ya yule msichana ilinishangaza zaidi.
“Unaishi peke yako jumba lote hili?”
“Ndiyo”
“Unapokwenda sehemu, nyumba inabaki tupu?”
“Ndiyo sababu nilihitaji mlinzi”
“Na si kwa usiku tu, hata kwa mchana anahitajika mlinzi” nikamwambia.
“Wewe utaweza kulinda usiku na mchana?”
“Tunaweza kuwa walinzi wawili, mmoja wa usiku mwingine wa mchana”
Nilipomwambia hivyo msichana huyo alitikisa kichwa.
“Mimi ninahitaji mlinzi mmoja tu” akaniambia.
“Kwa kweli itakuwa vigumu mlinzi mmoja kulinda usiku na mchana”
“Basi utalinda usiku kama
tulivyokubaliana. Kwa mchana sina wasiwasi sana na halafu mimi mwenyewe ninakuwepo
nyumbani muda mwingi. Ngoja nikupatie zile pesa”
Msichana huyo akanyanyuka na kuingia ndani. Baada ya muda kidogo
alirudi akiwa ameshika kitita cha noti nyekundu. Akanifuata pale nilipoketi. Na
mimi nikanyanyuka.
“Hizi hapa shilingi laki moja” akaniambia huku akinipa zile pesa.
Nikazipokea na kuzitia mfukoni bila kuzihesabu.
“Sasa twende nikakuoneshe maeneo ya hii nyumba”
Msichana huyo akatoka, na mimi nikamfuata. Alinizungusha pande zote za
ile nyumba, tukaishia kwenye banda lililokuwa kando ya geti.
“Hili ndilo banda la mlinzi. Utakuwa unakaa humu” Msichana huyo
akaniambia.
“Sawa”
“Hebu tuingie ndani ulione vizuri”
Tukaingia ndani ya lile banda. Kulikuwa na meza iliyokuwa na simu
pamoja na kiti.
“Hii simu unaweza kunipigia mimi kama
utakuwa na dharura yoyote” akaniambia.
“Sawa”
“Ninachokusisitiza ni kuwa usilale usiku hasa kuanzia saa tisa hadi saa
kumi na moja alfajiri. Wezi hupenda kuja katika muda huo kwa sababu watu
wanakuwa wamekolewa na usingizi. Umenielewa?”
“Nimekuelewa”
“Na mara kwa mara uwe unazunguka kwenye maeneo ya nyumba
niliyokuonesha, wezi wanaweza kuruka ukuta bila wewe kujua”
“Ni kweli. Mara kwa mara nitakuwa nazunguka”
“Ninayo tochi ya mawe sita, nitakupa pamoja na sime. Wakati mwingine
taa huzimika, itakusaidia kumulika kwenye kiza”
“Sawasawa”
“Sasa tutoke nikurudishe nyumbani”
Tukatoka kwenye lile banda. Msichana huyo alifunga mlango wa nyumba
yake. Tukajipakia kwenye gari lake
na kutoka. Hakukuwa na
haja ya kushuka kufungua geti au kulifunga kwani geti hilo lilifunguka na kujifunga lenyewe kwa
rimoti iliyokuwa mbele ya gari.
Wakati tunaendelea na safari, yule msichana akaniuliza.
“Unaishi wapi?”
“Ninaishi Makorora”
“Mna nyumba yenu pale?”
“Ni chumba cha kupangisha”
Baada ya hapo tulibaki kimya mpaka tulipoingia eneo la Makorora.
“Unaishi mtaa gani?” akaniuliza.
“Ninaishi nyumba ya tatu kutoka hospitali ya Makorora”
Tulipofika hospitali ya Makorora nilimuonesha nyumba niliyokuwa
ninaishi, akanipeleka hadi barazani.
“Asante
kwa msaada wako” nikamshukuru wakati nafungua mlango ili nitoke kwenye gari.
“Asante
na wewe kwa kunikubalia uwe mlinzi wangu”
“Usiwe na wasiwasi, leo natarajia kuandika ile barua ya kuacha kazi.
Kesho nitaipeleka ofisini”
“Sasa niambie nikupitie kesho saa ngapi ili unipe uhakika kuwa unakuja
kuanza kazi kwangu?”
“Nipitie saa kumi na moja jioni”
Saa kumi na moja jioni!. Kwanini isiwe mchana? Muda ulioutaja ni wa
kujiandaa kuja kuanza kazi”
“Na ndio muda huo ninaotaka uje ili tuondoke pamoja”
“Kama mwenyewe unataka hivyo sawa,
nitakuja hiyo saa kumi na moja”
Nikashuka kwenye gari.
“Ushinde salama” akaniambia wakati anaondoka.
Jioni ile nilishughulika kuandika ile barua ya kuacha kazi, nikaitia
kwenye bahasha na kusubiri asubuhi niiwasilishe ofisini kwetu.
Hatua ile ya kupata mwajiri mpya ambaye ameniahidi kuwa ataniongezea
mshahara, kwa kweli kilinifariji. Niliwaza kwamba endapo nitapata mshahara wa
kutosha, nitanunua fanicha za chumbani mwangu na kuondoa zile zilizokuwemo
ambazo zilikuwa zimepitwa na wakati na zilikwa zimechakaa.
Niliendelea kujiambia baada ya kununua fanicha zingine ikiwemo tv na
deki yake, nitatafuta msichana wa kumuoa ili nifungue ukurasa mpya wa maisha
yangu.
FUATILIA HADITHI HII HAPO KESHO hapa hapa Tangakumekuchablog
|
Monday, April 18, 2016
HADITHI, MWANAMKE ALIENICHUNUKE SEHEMU YA 17
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment