HADITHI na Faki A Faki, 0713 340572, 0655 340572
SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
SITASAHAU NILIVYOGEUZWA
PAKA
ILIPOISHIA
Tulipowapa taarifa
polisi, polisi watatu wakatupakia kwenye gari na kwenda nao katika eneo la
tukio.Hapo nilihojiwa maswali na nikajibu kila nilichoulizwa.Baada ya hapo
polisi hao waliichukua ile maiti na ile bunduki ya majambazi pamoja na kile
kiganja. Wakaniambia nirudi nyumbani lakini saa tatu nifike kituo cha polisi
kuandika maelezo.
Polisi hao wakaondoka na
ile maiti.Afisa wetu akaniruhusu niende nyumbani kubadili nguo kwani zilikuwa
zimetota na kujaa tope.Nikarudi nyumbani.Nilimueleza mjomba
kilichotokea.Akanipa moyo kwa kuniambia.
“Hayo ni matukio ya
kawaida katika kazi zetu lakini umefanya kitendo cha kijasiri”
Ilipofika saa tatu
nikawa kituo cha polisi.Nilikuwa nimeshaoga na kubadili nguo isipokuwa si
kunywa chai kwa sababu ya wasiwasi.
Nikiwa kituo cha polisi
niliingizwa katika ofisi ya afisa upelelezi ambaye alichukua maelezo
yangu.Baada ya kumaliza kuchukua maelezo yangu alinipongeza kutokana na ujasiri
wangu.
Tukio hilo la ujambazi
lilisababisha nipande cheo kazini kwangu.Nikavalishwa v mbili begani. Pia ukawa
ndiyo mwanzo kwa walinzi wa usiku wanaolinda sehemu nyeti kupewa bunduki. Kwa
vile mimi nilikuwa sijapata mafunzo ya kutumia bunduki nilipewa lindo jingine
la mchana kwa wiki nzima huku nikipewa mafunzo ya jinsi ya kutumia bunduki na
kulenga shabaha.
SASA ENDELEA
Baada ya wiki moja
nikawa tayari ninajua kutumia bunduki.Nikarudishwa kwenye lindo langu lilelile la
usiku.
Nimekieleza kisa hicho
kwa sababu kilikuwa chanzo cha mimi kufahamiana na msichana mmoja anayeitwa
Msekwa. Nilikutana na msichana huyo sokoni. Sote tulikuwa tunachagua nazi. Msichana
huyo wa Kiruvu akanisalimia kwa kutabasamu kisha akaniambia.
“Ninakufahamu”
“Tulikutana wapi
vile….?” Nikamuuliza huku nikijaribu kuvuta kumbukumbu.
“Ninakufahamu
tu”akaniambia
Nikawa sikumuelewa. Alipoona
ameniacha njia panda akaniambia.
“Wewe si ndiye
uliyemkata jambazi mmoja kiganja cha mkono ukachukua bunduki yake.....?”
hakumaliza sentensi yake akacheka kisha akaondoka. Nikabaki nimesimama
nikimuangalia.
Kitu ambacho sikukijua
ni kwamba habari zangu zilizungumzwa sana pale Handeni jinsi
nilivyowasambaratisha wale majambazi.Wakati nikipita kwenye mitaa watu walikuwa
akinisema na kuninyooshea kidole.Yule msichana alikisikia kisa changu na
kuniona nilikuwa kijana shujaa. Kwa kweli alinipenda.
Siku nyingine nilikuja
kukutana naye wakati ninaenda kazini. Akanisalimia na ndipo nilipogeuka na
kumuona.Tukaulizana hali. Akanieleza anapoishi kisha tukaachana. Kutoka siku
ile tukawa tunakutana mara kwa mara na kuzungumza. Bila kutegemea tukaja kuwa
marafiki na mwisho akawa mchumba wangu.Nikaja kuoana naye.
Tayari nilikuwa
nimepangisha chumba changu kwenye nyumba ya mzee mmoja iliyokuwa jirani na
mahakama ya mwanzo.Nikaendelea na maisha nikiwa na mke wangu ambaye tulipendana
sana. Miaka mitatu ikapita.
Siku moja wakati naenda
kazini mchana,nilisikia sauti ya msichana akiniita nyuma yangu.
“Rajabu….Rajabu….” nikageuka nyuma na kumuona Chausiku yule mchumba wangu wa
kwanza ambaye tulipanga kuoana nikipata kazi lakini nilipopata kazi nikamsahau
na kuoana na msichana mwingine.
“Oh! Chausiku ni wewe?
Sikukujua, samahani”
“Najua hukunijua.Habari
za siku?”
“Nzuri, za Songe au
hukai Songe siku hizi?”
“Niko Songe nakusubiri
wewe uje unioe, naona kimya tu”
Nikajidai kucheka.
“Mbona mimi nilishaoa”
“Kumbe ulishaoa?”
akaniuliza kwa sauti ya fadhaa.
“Nilishaoa mwenzako”
“Sasa kwanini hukuja
kuniambia kama umebadili mawazo?”
“Kwa hilo nakuomba
unisamehe.Najua nilikosea”
“Basi nimeshakusamehe.Ndoa
ni riziki, kama haikupangwa haiwezi kuwa. Sasa unafanya kazi wapi?”
“Ninafanya kazi ya
ulinzi. Si unaniona nilivyovaa?”
“Unafanya wapi?”
Nikamuelekeza zilipokuwa
ofisi zetu.
“Sasa wewe utakuja lini
Songe?”
“Nikipata likizo mwaka
huu nitakuja kuwatembelea”
“Sawa, basi mimi huwa
ninakuja mara kwa mara kuuza
vyungu. Nikimaliza kuuza
ninapanda gari ninarudi”
“Basi ukija nitembelee
ofisini kwetu. Si umesha pajua?”
“Nimeshapajua”
Baada ya hapo tukaagana.
Akaenda zake na mimi nikaenda kazini kwangu.
Kumbe kile kitendo cha
kumwambia nitembelee ofisini kwetu kilikuwa kosa.Baada ya wiki mbili wakati
nimerudi nyumbani jioni kutoka kazini,nikasikia mtu anabisha mlango wa chumba
changu.Mke wangu alikuwa uani.Nilipofungua mlango nikamuona mfanyakazi mwenzangu
amefuatana na Chausiku.Nikashituka.
"Karibuni"
nikawaambia huku nikitoa tabasamu la uongo kuficha mshangao wangu.
"Ahsante"
mfanyakazi mwenzangu ndiye aliyejibu na kuongeza "Huyu msichana
alikuja ofisini kukuulizia.Anasema anatoka Songe,alikuja kuuza bidhaa zake hapa
mjini lakini amechelewa gari.Ametuambia wewe ni kaka yake"
"Ndiyo, tunatoka
kijiji kimoja" nikasema na kumtazama Chausiku.
"Kumbe leo ulikuja
na umechelewa gari?" nikamuuliza.
"Gari limewahi
kuondoka na sina pa kulala ndiyo nikaja kukuulizia kazini kwako ili unipe
msaada wa mahali pa kulala hadi kesho asubuhi nirudi kijijini" Chausiku
akasema kwa ufasaha na kujiamini kama vile alijua mimi nina chumba cha wageni
wakati chumba changu kilikuwa kimoja tu.
Kadhalika sikuufurahia
ugeni wake nyumbani kwangu kwa sababu ya vile nilivyomuacha kwenye mataa na
kuoa mke mwingine.Sikutaka kabisa wakutane na mke wangu lakini ndiyo alikuwa
ameshaletwa nyumbani. Sikuwa na la kufanya zaidi ya kumkaribisha.
"Basi mimi ninarudi
kazini" mfanyakazi mwenzangu aliniambia.
Nikaagana naye akaenda
zake.
Mke wangu aliposikia
sauti za watu akaja haraka kwenye mlango, akamuangalia yule msichana.
Nikamtambulisha kuwa ni binti
wa shangazi yangu anayeishi Songe kisha nikamueleza tatizo lililomleta kwangu
jioni ile.
Mke wangu Msekwa kwa
kudhani ni wifi yake alimkaribisha chumbani.Wakazungumza sna kwa furaha na
vicheko.Jua likawa limekuchwa. Nikamfuata mama mwenye nyumba na kumuomba
amruhusu mgeni wangu alale chumbani kwa binti yake kwa siku moja.
Mama mwenye nyumba
akanikubalia.Jioni ile tulipika wali kwa sababu ya mgeni.Wenyewe tulikuwa
tupike ugali.Baada ya kula tulikaa nje tukazungumza mpaka saa nne usiku
tulipoingia ndani kulala.
Asubuhi kulipokucha
Chausiku aliondoka mapema sana ili kuwahi gari la saa moja.Nilishukuru kwamba
katika kukaa kwake pale nyumbani mke wangu hakumgundua kwamba alikuwa mchumba
wangu wa kwanza.
Baada ya wiki mbili
ulitokea ugomvi kati yangu na mke wangu. Kisa cha ugomvi huo ni mke wangu
kuchelewa kupika. Siku hiyo nilirudi kutoka kazini saa kumi na moja jioni. Kwa
kawaida ninakuwa sili mchana siku nikiwa kazini. Ni mpaka jioni ninaporudi mke
wangu anakuwa ameniwekea chakula cha mchana.
Siku hiyo sikukuta
chakula na njaa ilikuwa inaniuma. Nilimkuta mke wangu amelala.
Nikamuuliza "Vipi?"
Akanijibu kuwa alikuwa
amechoka baada ya kurudi kutoka katika harusi ya jirani yetu.
Kawaida yetu ni kuwa
ninaporudi kutoka kazini huniuliza kuwa aniwekee chakula au maji ya kuoga.
Lakini siku ile hakuniuliza chochote. Ikabidi nimwaambie mwenyewe.
"Nimwekee
chakula"
"Sikupika"
akanijibu haraka.
"Hukupika kwa
nini?"
"Si nilikwenda
harusini?"
"Ukenda harusini
ndiyo hupiki?"
"Ah! nimechoka
bwana, nimerudi sasa hivi!"
"Sasa kama wewe
umekula harusini mimi nikale wapi?"
"Lakini si
umeniruhusu mwenyewe niende?"
"Hilo sio swali
langu. Nimekuuliza kama hukupika mimi nikale wapi?"
"Lakini uliniruhusu
mwenyewe!"
"Kwamba
usipike?"
"Niende harusini"
"Lakini sikukuambia
nenda harusini lakini usipike. Kama umesharudi huko harusini kwanini
hukupika?"
Nilipomuuliza hivyo
alikunja uso akaguna. Jambo hilo liliniudhi nikakasirika.
Je nini kilifuatia baada
ya hapo? Hebu endelea kufuatilia hadithi hii katika blog yako maarufu ya Tangakumekuchablog.
No comments:
Post a Comment