HADITHI hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, Candle ni kituo bora cha kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu, Candle wako na hosteli na kutoa usafiri kwa gari lao, Candle inapokea wanafunzi na wafanyakazi wanaojiendeleza kielimu. Candle wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 777246
MWANAMKE ALIYENICHUNUKA
14 na Faki . A . Faki
ILIPOISHIA
“Aliwahi kunieleza”
“Je ulikubali kwa hiyari yako?”
“Hapana, sikukubali”
“Alikuwa anakutisha?”
Hapo nikanyamaza. Sikutaka kusema ukweli kuwa alikuwa ananitishia
maisha.
Yule mama alitambua mawazo yangu, akaniambia.
“Sema usifiche”
“Ndiyo alikuwa ananitisha” nikamwambia.
Banuna akanitazama kwa uso wa tadhaa.
“Alfred sema ukweli, nimekutisha mimi? Si tumekubaliana tuoane,
uliniambia kuwa umenipenda?” Banuna akaniambia lakini sauti yake haikuwa na
nguvu kwa vile maneno aliyosema yalikuwa ya uongo.
SASA ENDELEA
Sikumjibu chochote. Nilikuwa nimeinamisha kichwa changu chini. Sikutaka
kutazamana na macho yake.
Mama mtu akakasirika.
“Banuna, wewe muongo. Umekuja kunidanganya hapa!”
Banuna akamjibu kwa kiarabu. Pengine hakutaka nisikie uongo wake. Lakini
mama yake aliendelea kuchachamaa. Wakawa wanajibizana kwa kiarabu.
Mwisho Banuna alinyanyuka kwa hasira. Sikujua aliambiwa nini. Mama yake
naye akanyanyuka. Banuna alitamka neno lililomuudhi yule mama, akampiga kibao
Banuna.
“Ondoka hapa fedhuli mkubwa!” Mwanamke huyo wa kijini alimwambia Banuna
kwa ukali kisha
akaongeza.
“Mrudishe kijana wa watu kule ulikomchukua. Mrudishe sasa hivi halafu
ukome kumfuatafuata tena!”
Banuna alipopigwa kibao aliondoka huku maneno yakimtoka mdomoni.
“Sitamuacha hata ukunipiga. Nimeshampenda. Nitaendelea naye hivyo
hivyo!” akamjibu mama yake na kutokomea kwenye pazia.
Yule mama alikuwa akumfuata nyuma huku
akijibishana naye kwa kiarabu. Na yeye aliingia kwenye pazia hilo hilo.
Sauti zao za kujibizana zikawa zinasikika kwa ndani. Baadaye kukawa kimya.
Nikajikuta nimeachwa peke yangu mahali hapo. Kwa mara ya kwanza
nilianza kusikia uoga hasa vile ambavyo mwenyeji wangu aliyeambiwa anirudishe,
amenikimbia kwa hasira.
Nilijua kuwa nilikuwa nimemuudhi kwa kumkana mbele ya mama yake ambaye
ingawa alikuwa jini, alikuwa muadilifu sana.
Alipoambiwa na Banuna kuwa anataka kuoana na mimi, alitaka uthibitisho
kutoka kwangu. Nilipopinga jambo hilo
aliamua kumuonya Banuna asinifuate tena, lakini Banuna alikuwa kisoi.
Niliendelea kukaa pale kwa muda kidogo kabla ya kumuona jini mwingine
mwanaume aliyenifuata na kuniambia.
“Mama ameniambia nikurudishe kwako kwa usalama, sasa inuka twende”
Niliponyanyuka akaniambia.
“ Nifuate”
Nikamfuata. Tulipita katika njia ileile tuliyopita na Banuna mpaka
tukatokea ile sehemu yenye kiza. Jini huyo hakuniambia nimshike bega, hivyo
ikanibidi niwe karibu naye sana
ili tusipoteane. Tukaenda mpaka tukatokea kule juu ya mnara.
Yule jini akachutama na kuniambia.
“Kaa kwenye mabega yangu”
Nikakaa. Akanibeba na kuniambia nifumbe macho, nikafumba macho. Vile
ananyanyuka tu, nikahisi tunaibuka juu ya bahari!
Nilifumbua macho yangu bila kuambiwa. Ilikuwa miujiza mikubwa ambayo
sikupata kuiona maishani mwangu.
Yule jini alinipeleka hadi ufukweni mwa bahari, akachutama na kuniambia
nishuke. Nikashuka.
Niliposhuka alichora msitari kwenye tope, akaniambia.
“Fumba macho yako halafu vuka msitari huu. Ukishavuka fumbua macho
yako”
Nikaenda nyuma ya ule msitari, nikafumba macho yangu na kuinua hatua
kuvuka ule msitari. Nilipofumba na nilifumbua macho na kujikuta nipo mbele ya
mlango wa nyumba ninayoishi Makorora.
Niliangalia kila upande ili kujiridhisha kuwa kweli nilikuwa nyumbani
ninakoishi. Nikaona ni kweli. Macho yangu hayakunidanganya.
Ilikuwa bado usiku. Na kitu kingine cha ajabu ni kuwa nguo zangu
zilikuwa kavu kabisa. Nilisimama kwa muda mbele ya huo mlango nikifikiria kati
ya kubisha mlango niingie ndani, au nirudi kwa Juma.
Kwa vile ilikuwa usiku, kubisha mlango ilikuwa ni vyema zaidi ila nilipata shaka kuwa naweza kuingia chumbani
mwangu na kukutana na Banuna mwenye hasira.
Wazo hilo
lilinifanya niamue kwenda kwa Juma. Ilikuwa ni hatari usiku ule kutembea nikiwa
peke yangu lakini nilijikaza kiume. Nikatembea haraka haraka kuelekea mtaa wa pili.
Mwili ulikuwa unanisisimka kila nilipokumbuka nilivyopelekwa ujinini.
Sasa niligundua kuwa Banuna alipokuja kunichukua, sikuwa na akili yangu.
Nilikuwa kama niko kwenye ndoto. Lakini kwa muda ule niliorudishwa nilijiona
niko sawa.
Niseme ukweli kama ningekuwa na akili
yangu timamu wakati Banuna anakuja kunichukua, nisingekubali. Tungebishana sana na ningekimbia. Na
yeye kwa kujua hilo
ndio maana alinizuga akili.
Nilipofika nyumbani kwa Juma nilijaribu kufungua mlango, kwa vile
nilipoondoka na Banuna hatukuufunga. Lakini nikaukuta umefungwa.
Nikaenda kwenye dirisha la chumba cha Juma, nikamgongea huku nikimuita.
“Juma! Juma!”
Mara moja Juma alizinduka na kuuliza.
“Wewe nani?”
“Mimi Alfred”
“Alfred?” Juma alionekana kushituka, akauliza. “Alfred si yumo humu
ndani?”
“Ni mimi. Nilikuwa nimetoka, wewe ukiwa umelala”
Mara nikaona taa inawashwa.
“Alfred ulitoka saa ngapi, mbona mlango umefungwa kwa ndani?” Sauti ya
Juma ikauliza kutoka ndani.
“Nifungulie, nitakueleza”
Baada ya ukimya wa dakika mbili hivi, Juma akafungua mlango wa nje.
“Ulitokaje humu ndani?”
“Tuingie ndani nikueleza”
Tukaingia ukumbini. Juma akaufunga mlango wa nje kisha tukaingia
chumbani. Mimi nilikaa kwenye kiti, Juma akakaa kwenye kitanda.
ITAENDELEA KESHO. Usikose na kujua nini Afred atamueleza Juma na je, Banuna hatatokea ? uhondo huu ni hapahapa Tangakumekuchablog
|
Friday, April 15, 2016
HADITHI , MWANAMKE ALIENICHUNUKU SEHEMU YA (14 )
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment