HADITHI na Faki A Faki, 0713 340572, 0655 340572
MWANAMKE ALIYENICHUNUKA 19 inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu cha Candle Education Centre Tanga.
ILIPOISHIA
Baada ya kuridhika kuwa kila kila kitu kiko sawa nilikaa kwenye kiti.
Muda si muda yule msichana aliingia tena akiwa ameshika kiredio kilichokuwa
kimewashwa.
Akakiweka juu ya meza na kuniambia.
“Redio hii na ya kukuchangamsha wakati wa usiku”
“Loh!. Nashukuru sana,
nitasikiliza taarifa za habari na miziki”
“Basi nipo ndani” akaniambia na kutoka.
Nilikaa ndani ya lile banda hadi giza
lilipoingia niliwasha taa kisha nikatoka kwenye ua na kuamza kurandaranda huku
na huko.
Ilipofika saa mbili usiku kuna msichana alitoka mle ndani akiwa
ameshika chano cha chakula. Hakuwa yule mwajiri wangu. Akaingia kwenye lile
banda na kukiweka kile chano juu ya meza kisha akatoka.
“Nimekuwekea chakula juu ya meza” akaniambia na kuingia ndani.
Kilichonishangaza ni kuwa mwajiri wangu aliniambia kuwa alikuwa anaishi
peke yake mle ndani. Yule msichana mwingine alitokea wapi?
Wakati nataka kuingia ndani ya lile banda nilisikia simu inaita.
Nikaingia haraka na kwenda kuipokea.
SASA ENDELEA
“Hellow…!”
“Ndiyo Alfred. Nimemtuma mtumishi akuletee chakula” Ilikuwa sauti ya
yule msichana aliyeniajiri kazi.
“Nimekiona. Asante sana” Na mimi nikamjibu
kwenye simu.
“Sawa. Endelea kula”
Akakata simu. Nilikitupia macho chakula hicho. Ilikuwa pilau ya kuku na
bilauli ya juisi. Pembeni mwa sahani kuliwekwa ndizi mbivu moja pamoja na
chungwa.
Yule mtumishi alirudi tena, safari hii akiwa na jagi la maji na bakuli.
Aliweka bakuli juu ya meza akaniambia.
“Nikunawishe mkono”
Nikakinga mikono yangu kwenye lile bakuli. Mtumishi huyo akanimiminia
maji. Niliosha mikono yangu nikamwambia.
“Basi”
Akaliweka jagi juu ya meza na kutoka.
Mtumishi alikwa mrembo na alikuwa ananukia manukato. Nilitamani angalau
angekuwa mke wangu.
Pilau ilikuwa tamu. Wakati ninakula nilijiambia fedha ndio kila kitu.
Msichana mrembo kama yule ameajiriwa utumishi
wa ndani kwa sababu ya fedha tu.
Nilipomaliza kula, msichana huyo alirudi tena kuondoa vyombo.
Mwajiri wangu akanipigia tena simu.
“Umeshakula?” akaniuliza.
“Nimekula, nimemaliza. Nashukuru, asante
sana”
“Umetosheka?”
“Nimetosheka sana”
“Sasa kuwa macho usiku huu”
“Usiwe na wasiwasi. Nitakuwa macho”
Simu ikakatwa.
Usiku ule ulikuwa wa faraja kwangu kwa sababu kwa mara ya kwanza tangu
nianze kazi ya ulinzi, nilifanya kazi
katika mazingira ya kuridhisha.
Kwanza ni kule kupata chakula cha jioni bure na bila
usumbufu na pia kukaa ndani ya banda mahali ambapo sitateseka kwa baridi.
Nilipochoka kukaa ndani ya lile banda nilitoka
nikazunguka katika ua wa ile nyumba kujichangamsha kabla ya kurudi tena ndani
ya banda hilo.
Ilipofika saa tisa yule msichana alitoka nje akaingia
ndani ya lile banda na kuzungumza na mimi hadi saa kumi na moja alfajiri aliporudi
ndani.
Mpaka kunakucha sikuona kama
nilipata shida yoyote. Nilifanya kazi pale kwa wiki nzima na taratibu nilianza
kupazoea.
Baada ya wiki kumalizika, wiki iliyoanza niliendelea kwenda
kazini kama kawaida.
Kulikuwa na siku ambayo nilikuta nyumba imepambwa kuliko kawaida. Na mle ndani kulikuwa na
shamrashamra. Sikuweza kujua mlikuwa na shughuli gani. Aliyenifungulia geti
alikuwa mtumishi wa mle ndani. Nikamuuliza kulikuwa na nini. Akaniambia
kulikuwa na sherehe.
“Sherehe ya nini?” nilimuuliza.
“Atakueleza dada mwenyewe”
“Dada mwenyewe yuko wapi?”
“Yuko ndani”
Mtumishi huyo akaondoka na kurudi ndani. Nikakaa ndani
ya lile banda hadi saa mbili usiku nilipoletewa chakula. Nilipomaliza kula
mtumishi alikuja kuondoa vyombo.
Nikaendelea kubaki ndani ya lile banda hadi saa nane
usiku, yule mtumishi alipokuja tena, akaniambia.
“Unaitwa ndani”
Nilishituka. Sikujua nilikuwa naitiwa nini. Na mle
ndani shamra shamra zilikuwa zikiendelea hadi muda huo.
Nikamfuata yule msichana aliyekuja kuniita, nikaingia
naye ndani. Nilikuta watu mbalimbali waliovalia maridadi wameketi wakinywa
vinywaji na kushereheka.
Msichana huyo alinichukua hadi kwenye chumba kimoja ambacho alinionesha
bafu na kuniambia.
“Unatakiwa uoge, ukimaliza unakuja hapa kwenye kabati”
Alinifungulia kabati lililokuwa mle ndani ya kile chumba na kunionesha
nguo zilizokuwemo ndani.
“Utachagua suti utakayoipenda, utavaa na shati jeupe na viatu vyeupe.
Halafu utagonga mlango, mimi nitaingia ili nikupeleke kwa dada”
Kwanza
nilisita, nikataka kumuuliza kulikoni lakini nikaona nitekeleze vile
nilivyoagizwa.
Nikaoga. Nilipomaliza nilichagua suti ya kijivu niliyoipenda. Nikaivaa
pamoja na shati jeupe na viatu vyeupe.
Nilipomaliza niligonga mlango. Hapo hapo yule mtumishi akaingia.
AITAENDELEA KESHO hapahapa Tangakumekuchablog
Kwa habari, matangzo wasiliana chumba cha Habari na Uenezi 0655 902929
|
Thursday, April 21, 2016
HADITHI MWANAMKE ALIENICHUNUKU SEHEMU 19
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment