HADITHI hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, Candle ni mabingwa wa kufaulisha wanafunzi wanaorisiti mitihani yao na wanaojiendeleza kielimu makazini, Candle wako na hostel na wako na gari maalumu la kuwapelea wanafunzi shule, Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
MWANAMKE ALIYENICHUNUKA
18
ILIPOISHIA
Saa kumi na moja jioni!. Kwanini isiwe mchana? Muda ulioutaja ni wa
kujiandaa kuja kuanza kazi”
“Na ndio muda huo ninaotaka uje ili tuondoke pamoja”
“Kama mwenyewe unataka hivyo sawa,
nitakuja hiyo saa kumi na moja”
Nikashuka kwenye gari.
“Ushinde salama” akaniambia wakati anaondoka.
Jioni ile nilishughulika kuandika ile barua ya kuacha kazi, nikaitia
kwenye bahasha na kusubiri asubuhi niiwasilishe ofisini kwetu.
Hatua ile ya kupata mwajiri mpya ambaye ameniahidi kuwa ataniongezea
mshahara, kwa kweli kilinifariji. Niliwaza kwamba endapo nitapata mshahara wa
kutosha, nitanunua fanicha za chumbani mwangu na kuondoa zile zilizokuwemo
ambazo zilikuwa zimepitwa na wakati na zilikuwa zimechakaa.
Niliendelea kujiambia baada ya kununua fanicha zingine ikiwemo tv na
deki yake, nitatafuta msichana mzuri wa kumuoa ili nifungue ukurasa mpya wa maisha
yangu.
SASA ENDELEA
Asubuhi kulipokucha nilienda kazini bila kuvaa sare yangu. Nilipofika
nilitoa ile barua kwa bosi wangu. Akaifungua na kuisoma mbele yangu.
Alipomaliza kuisoma alishangaa na kuniangalia.
“Umeamua kuacha kazi?” akaniuliza.
“Ndiyo” nikamjibu.
“Kwanini umeamua kuacha kazi ghafla, kuna tatizo lolote?”
“Hakuna tatizo lolote. Kaka yangu ameniita Dar es Salaam. Anataka nikaishi kule.
Atanitafutia kazi mahali pengine” nikamdanganya..
“Sawa, lakini kwa sheria za kikazi itabidi usamehe mshahara wako”
“Ninajua”
“Sawa. Tunakutakia kila la heri huko Dar es Salaam unakokwenda”
“Asante
bosi wangu”
Nikaondoka pale ofisini na kurudi nyumbani. Nilipofika nyumbani
niligundua tatizo moja kwamba nisingeweza kuzitumia tena zile sare za kampuni
niliyoacha kazi na hivyo ingebidi yule msichana aninunulie sare zingine
atakazopenda nivae..
Ilipofika saa kumi na moja jioni nikawa nimeketi barazani mwa nyumba
niliyokuwa naishi kumsubiri mwajiri wangu mpya.
Muda wa saa kumi na moja na robo hivi, niliiona gari yake ikitokea.
Punde tu ikasimama kando ya baraza ya nyumba yetu. Nikanyanyuka na kuifuata.
Moja kwa moja nilifungua mlango wa upande wa pili wa dereva na kujipakia.
“Habari za tangu jana?” Msichana huyo akawahi kunisalimia huku
akitabasamu kwa haiba ya kipekee kabisa.
“Nzuri, sijui zako?” nikamjibu.
“Mimi mzima. Vipi?”
“Ndiyo umekuja kunichukua?” nikamuuliza.
“Kwani umeshaacha kazi kule kwa mwanzo?”
“Tayari nimeshaacha. Nilikuwa nakusubiri wewe tu”
“Asante sana. Sasa tunaweza
kwenda?”
“Ndiyo, isipokuwa…”
“Isipokuwa nini tena Alfred?”
“Ni suala la sare za kazi. Siwezi kutumia sare ya kampuni ya zamani”
“Oh sawa. Nitakununulia”
Msichana alitia gea na kuiondoa gari.
“Sikuchukua chakula cha jioni wala chupa ya chai”. Nikamwambia wakati
gari ikichanganya mwendo.
“Usijali. Nitakupatia kila kitu”.
Baada ya hapo tukawa kimya hadi tulipofika nyumbani kwake. Aliingiza
gari ndani ya geti akaisimamisha karibu na banda la mlinzi.
“Sasa shuka uingie kwenye banda lako” akaniambia.
Wakati nafungua mlango aliniuliza.
“Umekula mchana?”
“Nimekula lakini nitahitaji chakula cha usiku”
“Hakuna tatizo”
Nikafungua mlango na kushuka, nikaingia kwenye lile banda. Msichana
aliingiza gari kwenye banda la gari. Akashuka na kufungua nyumba yake.
Aliingia ndani na baada ya muda kidogo alitoka akiwa ameshika jaketi,
sime na tochi. Akaingia katika lile banda na kunipa vile vitu.
“Hili jaketi utavaa usiku na hii sime pamoja na hii tochi utatumia kwa
ulinzi”
“Asante sana”
Nilivipokea na kuviweka juu ya meza.
“Labda kuna kitu utahitaji?”
“Kwa sasa sihitaji kitu”
“Kama utakuwa na tatizo lolote nipigie
simu”
Akaniandikia namba yake kwenye karatasi na kuniwekea juu ya meza kisha
akatoka.
Alipotoka nililijaribu lile jaketi na kuona lilikuwa sawa. Nikashika
ile sime na kuiangalia kisha nikairudisha juu ya meza. Nikaichukua ile tochi na
kujaribu kuiwasha. Ilipowaka niliizima nikaiweka juu ya meza.
Baada ya kuridhika kuwa kila kila kitu kiko sawa nilikaa kwenye kiti.
Muda si muda yule msichana aliingia tena akiwa ameshika kiredio kilichokuwa
kimewashwa.
Akakiweka juu ya meza na kuniambia.
“Redio hii na ya kukuchangamsha wakati wa usiku”
“Loh!. Nashukuru sana,
nitasikiliza taarifa za habari na miziki”
“Basi nipo ndani” akaniambia na kutoka.
Nilikaa ndani ya lile banda hadi giza
lilipoingia niliwasha taa kisha nikatoka kwenye ua na kuamza kurandaranda huku
na huko.
Ilipofika saa mbili usiku kuna msichana alitoka mle ndani akiwa
ameshika chano cha chakula. Hakuwa yule mwajiri wangu. Akaingia kwenye lile
banda na kukiweka kile chano juu ya meza kisha akatoka.
“Nimekuwekea chakula juu ya meza” akaniambia na kuingia ndani.
Kilichonishangaza ni kuwa mwajiri wangu aliniambia kuwa alikuwa anaishi
peke yake mle ndani. Yule msichana mwingine alitokea wapi?
Wakati nataka kuingia ndani ya lile banda nilisikia simu inaita.
Nikaingia haraka na kwenda kuipokea.
ITAENDELEA KESHO
Kwa matangazo wasiliana na chumba cha habari na uenezi 0655 902929
|
Tuesday, April 19, 2016
HADITHI MWANAMKE ALIENICHUNUKU SEHEMU YA 18
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment