HADITHI
SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572, 0713 340572
SITASAHAU NILIVYOGEUZWA
PAKA 5
ILIPOISHIA JANA
Wanawake waliokuwa uani
pamoja na mama mwenye nyumba wakatushangaa.
"Jamani kuna nini,
mbona mnatushitua?" mama mwenye nyumba aliuliza kwa hofu.
"Msekwa
ameuliwa,amepigwa kisu kifuani na shemeji.Nendeni chumbani mwao mumuone!"
Mkiwa akasema huku akilia
"Sikumpiga kisu
shemeji, hebu nielewe.Mimi nilikuja na kumkuta ameshapigwa kisu. Mbona unataka
kunitia katika hatia?" nikamwaambia kwa ukali kidogo.
"Ni wewe shemeji,
ndiye uliyekuwa naye huko chumbani.Ni chuki za jana hizo"
Wanawake wote waliokuwa
uwani wakaenda ukumbini, wakaingia chumbani mwangu.Mimi nilikuwa nikiendelea
kueleza kile nilichokishuhudia.Kila aliyeingia mle chumbani alitoka mbio huku
akipiga kelele.
Wanawake wengine
walikimbilia uani wengine walikimbilia nje.Mama mwenye nyumba alinifuata na
kunishika mkono na kuniuliza "Kwanini umefanya kitendo kama kile
mwanangu?"
"Sikumpiga kisu
mimi mama"
"Ni wewe, shemeji
yako amekuona.Unakataa nini" mama mwenye nyumba akanikata kauli.
SASA ENDELE
"Siye
mimi.....mbona hamnielewi jamani.....?" kila nilipotaka kueleza
nilizingirwa na vilio vya wanawake hao.Wengine wakinilaani na wengine
wakiniapiza.
"Baba unaweza
kufanya kitendo kama kile kwa mke wako?" mwanamke mmoja aliniuliza akiwa
amenitolea macho.
"Ha! ni ukatili wa
hali ya juu!. Unamchoma kisu mwenzako kwa jambo la kipuuzi tu?" mwanamke
mwingine akajisemea peke yake.
Huo ulikuwa ni ushahidi
wa kutosha kunitia kwenye hatia hata kama sikuwa mimi niliyeua.Nikaona
usalama wangu ulikuwa hatarini.
Nilihofia pia kuwa
kelele za wanawake hao zingeweza kuwavuta majirani na nyumba ikajaa watu. Penye
wengi huzaa mengi, ningeweza kushikwa na watu wenye hasira nikapigwa na kuuawa
wakati sikutenda kosa lolote na sijamjua aliyetenda kosa hilo.
Nikaona niondoke.
Kuondoka kwenyewe pia nilitumia udanganyifu wa kujifanya ninakwenda polisi
kutoa taarifa. Hapo ndipo nilipofanikiwa kutoka salama. Lakini sikwenda polisi.
Nilikwenda katika kituo cha mabasi cha Handeni,nikapanda basi la kijijini kwetu
Songe
Lakini ni kwanini
sikwenda polisi?.Sikwenda polisi kwa sababu nilijua kuwa wangenikamata mimi na
huo ndio ungekuwa mwisho wa maisha yangu.
Ningefunguliwa kesi ya
kuua kwa kukusudia.Wale wanawake wote wangeitwa wakatoa ushahidi wakati mimi
sikuwa na shahidi hata mmoja. Uongo wa wengi si ukweli wa mtu mmoja. Ningenyongwa
tu.
Baada ya kujipakia
kwenye basi hilo haukupita muda mrefu basi likaondoka. Nikaenda kijijini
kwetu Songe. Mji wa Handeni nikaukimbia. Sikujua tena kilichotokea nyuma
yangu.
Nilipofika Songe
nilijificha kwenye mashamba hadi usiku, ndipo nikatoka na kutembea kwa miguu
hadi kijiji kingine ambako Chausiku alikuwa anaishi kwenye chumba chake
mwenyewe.
Mpaka nilipokuja
kuigundua nyumba aliyokuwa anaishi ilipita kazi.Lakini kwa kifupi nilipoipata
nyumba yake ilikuwa saa tatu usiku.
Ilikuwa ni nyumba kubwa
iliyojengwa kwa tofali.Yeye alikuwa amepangisha chumba.
Chausiku aliponiona
alifurahi sana akanikaribisha chumbani kwake kwa
bashasha.Tukazungumza. Nikamdanganya kuwa nimeamua kuacha kazi na kurudi
kijijini kwetu kujishughulisha na kilimo.
Nilidhani angeniuliza
kwanini nimeacha kazi. Lakini swali lake lilikuwa. "Na mke wako
umemuachia nani?"
"Nimeachana naye
ili nije nikuoe wewe mchumba wangu wa zamani"
Chausiku akafurahi
sana. "Kumbe bado ulikuwa unanipenda?"
"Nakupenda
sana.Yule msichana nilikuwa nimemuoa kwa bahati mbaya tu lakini chaguo langu
lilikuwa ni wewe"
"Sasa ngoja basi
nikuwekee maji ukaoge halafu nikupikie chakula"
"Nitakushukuru
sana"
Huo ndio uzuri niliouona
kwa wanawake wa vijijini.Hawakuulizi umekuja na nini au una kiasi gani cha
pesa.Wao wanafurahia mume tu.
Baada ya muda kidogo
Chausiku alirudi chumbani na kuniambia "Maji tayari"
Chausiku akanipa khanga
yake ili nivue nguo.Kule kijijini kwetu taulo hazikuwa zikitumika sana.Pengine
ni kwasababu ya ukata. Chausiku akanisindikiza hadi uani ambako alinitambulisha
kwa wapangaji wenzake kuwa ni mchumba wake ninayetokea Handeni. Akatoa maelezo
marefu ya tangu tulivyoanzana tukiwa shule.Wenyeji wangu wakanifurahia na
kunikaribisha.
Niliporudi kutoka kuoga
sikukaa sana Chausiku akaniletea ugali kwa perege. Nikala hadi nikashiba.
Huo ukawa mwanzo wa
maisha yangu katika kijiji hicho. Siku za kwanza kwanza nilikuwa
najifichaficha.Baada ya juma moja Chausiku alipata habari kuwa kuna polisi
waliokwenda Songe kuniulizia lakini wakaambiwa niliondoka kijijini hapo miaka
mitatu iliyopita na sijaonekana tena.
Mke wangu akaja
kuniambia. Mimi nikamwaambia kwamba polisi walikuja kuniulizia kutokana na kesi
ya ujambazi.Nikamhadithia kile kisa cha jambazi niliyemkata mkono na mwingine
kumpiga risasi. Chausiku akaamini kuwa hao polisi walikuwa wananitafuta kwa
sababu hiyo.
Ilipofika wiki ya pili
nikaandaa mipango ya harusi. Harusi za vijijini hazina gharama kubwa,hivyo
mipango yangu ilikwenda vizuri japokuwa sikuwa na fedha za kutosha.Wiki ya tatu
yake nikaoana na Chausiku na kuendelea kuishi katika nyumba ileile.
Nilikuwa
nikijishughulisha na kilimo na mke wangu alikuwa akiendelea na kazi yake ya
ufinyanzi wa vyungu ambavyo alikuwa akivipeleka Handeni kuviuza kila wiki.
Hivyo maisha yalikuwa yanatuendea vizuri. Chakula tulikuwa nacho cha kutosha na
pesa za kutumia hazikuwa zikitupiga chenga.
Baada ya kupita mwaka
mmoja angalau nikajiona niko huru. Ule wasiwasi wa kukamatwa ukaanza kunitoka.
Nikahisi lile tukio la kuawa kwa mke wangu wa kwanza limeanza kusahauliwa na
polisi.
Katika maisha yetu na
Chausiku kulijitokeza kitu ambacho kilinitia wasiwasi. Mara nyingi ninapoamka
usingizini wakati wa usiku Chausiku alikuwa hayupo kitandani. Lakini ninapolala
tena baadaye ninakuja kuta nimelala naye.
Niliwahi kumuuliza
anakwenda wapi.Siku za kwanza alinijibu kuwa labda ninaota. Lakini siku zingine
aliniambia anakwenda maliwatoni kujisaidia.
Kuna siku moja ambayo
nimeamka na kukuta nimelala peke yangu. Nikatoka hadi uani kumfuatilia lakini
sikumuona,nikarudi chumbani.
Asubuhi nilipomuuliza,
Chausiku alikasirika akaja juu na kuniambia kuwa alikuwa ametoka barazani
kupunga upepo kwa sababu ya joto lililokuwemo ndani.
Nikamwaambia haikuwa
jambo zuri kutoka nje peke yake wakati wa usiku kwani anaweza kushambuliwa na
fisi wanaozunguka ovyo usiku kucha.
Chausiku akanyamaza
kimya.
Siku nyingine aliniaga
kuwa anakwenda kwa bibi yake mzaa mama yake aliyekuwa akikaa kijiji cha jirani.
Akaniambia atalala hukohuko na atarudi kesho yake.
Lakini akanionya kuwa
nisifungue chumba chake ambacho alikuwa akikitumia kama stoo yake. Baada ya
kile chumba tulichokuwa tunalala alikuwa na chumba kingine ambacho sikupata
kukiingia hata siku moja. Alikuwa akiingia yeye mwenyewe tu kuweka vitu vyake
pamoja na vyungu alivyokuwa anatengeza.
Siku ile alipoondoka
kwenda kumsalimia bibi yake, usiku wake nikaamua kuingia katika kile chumba
alichonikataza nisiingie.
Nilivizia watu wote
walikuwa wameshalala. Nikafungua mlango na kuingia huku nimeshika taa ya
kandili (Chemli) ili niweze kuona.
Hayo niliyoyakuta humo
chumbani sikuyatarajia kabisa. Yalikuwa ni maajabu yaliyonishitua sana!
Je kijana huyo ameona
nini? Hakikisha hupitwi na uhondo. Usikose kufungua blog hii hapo kesho ili
ujue kilichotokea.
No comments:
Post a Comment