HADITHI na Faki A Faki 0715 340572 , 0655 340572
SITASAHAU NILIVYOGEUZWA
PAKA 1
Kweli maisha ni safari
ndefu. Kama ilivyo safari ndefu yoyote ile, ina milima, mabonde, mbuga na
misitu. Na waswahili wana msemo usemao "Kabla hujafa hujaumbika".Leo
unaweza kujiona uko kamili lakini kesho au keshokutwa ukawa mlemavu wa aina
yoyote ile.
Lakini kama ulemavu unaweza kuwa jambo la kumshangaza mwanadamu, ingawa tumezoea kuwaona walemavu kila siku, inakuwaje pale binaadamu anapobadilika umbile lake na kuwa na umbo la mnyama, mnyama kabisa asiyeweza kusema chochote na mwenye miguu minne na mkia! Bila shaka hilo litakuwa ni la kushangaza zaidi lakini ndilo lililonitokea mimi. Amini usiamini niligeuka paka na niliiishi kama paka kwa siku kadhaa. Na hapo ndipo nilipojua adha wanazopata wanyama kutoka kwa binaadamu na pia ndipo nilipojua kuwa uchawi upo na laana zipo. Ilikuwa wapi na lini? sasa fumbua macho yako uanze kutiririka katika kisa hiki ambacho nina hakika hutakisahau maishani mwako. Jina langu ni Rajab Mgosingwa. Hilo jina Mgosingwa nilipachikwa na watu kwa sababu neno hilo linatumika katika kabila langu la Kizigua kumaanisha "Mtu mwanamume" kwa hiyo kwa vile nilikuwa mzigua na rafiki zangu wakanipachika jina hilo la Mgosingwa. Lakini mwenyewe nililikatisha na kujiita Mgosi ambalo nalo kwa kabila la Kibondei lina maana ileile ya mtu mwanaume. Wazigua na Wabondei ni jamii yenye asili moja. Nilizaliwa katika Kijiji cha Songe,Tarafa ya Kwekivu, Wilaya ya Handeni. Nilipofikia umri wa kwenda shule wazazi wangu walinipeleka shule kuanza darasa la kwanza. Nilisoma mpaka darasa la nne ambapo baba yangu mzazi alifariki. Na mimi sikuendelea tena na masomo. Nikaachia darasa la nne. Mara nyingi nilikuwa nikimsaidia mama yangu kazi za kilimo na mifugo kwani mimi nilikuwa mtoto wa pekee niliyezaliwa. Sikuwa na ndugu wa tumbo moja. Nilianmbiwa kwamba mama yangu aliharibu mimba (mimba zilitoka) mara tano kabla ya kuzaliwa mimi na nilipozaliwa nilikuwa ndiyo kitinda mimba. Pale katika mtaa niliokuwa naishi palikuwa na msichana mmoja akiitwa Chausiku. Nilisoma naye darasa moja. Mimi nilipoacha darasa la nne yeye aliendelea hadi darasa la saba. Tulianza uhusiano wa kitoto tangu tukiwa darasa la tatu. Tulivyofika darasa la nne ambalo mimi niliacha tuliahidiana kuwa tukimaliza masomo tutaoana. Pale kijijini kwetu ukifika darasa la saba ndiyo umesoma. Sekondari ilikuwa ni kama ndoto isiyotabirika. Kwa mwaka kijiji kinaweza kisitoe hata mwanafunzi mmoja kwenda Sekondari. Na kama kutatokea mmoja inakuwa ni kioja. Kijiji kizima kitajua. Katika miaka yangu minne niliyosoma katika shule ile ya msingi, sikumbuki kama kulikuwa na mwanafunzi aliyekwenda sekondari. Miaka miwili baada ya kuacha masomo Chausiku akawa mchumba wangu.Tulipendana sana. Wakati huo uhusiano wetu ulipata nguvu kwa sababu nilikuwa ninajua kutafuta pesa na nilikuwa nikimsaidia sana. Lakini uchumba huo ilikuwa nimsubiri amalize darasa la saba ndipo tuoane. Mwenyewe alishajua kuwa asingefaulu. Kwa bahati mbaya Chausiku alipokuwa darasa la sita mama yangu alifariki dunia. Nikawa sina mtu wa kuniongoza. Nikauzauza mifugo na nilipoona maisha yameanza kuwa magumu nikaondoka kwenda mjini Handeni kutafuta kazi. Nikamuahidi Chausiku kuwa endapo nitafanikiwa kupata kazi, mwakani nitarudi kuoana naye twende tukaishi Handeni kwani nilijua kipindi hicho yeye atakuwa amemaliza darasa la saba. Handeni nilifikizia kwa mjomba wangu aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni moja ya ulinzi. Nilimwambia kwamba nilikwenda kutafuta kazi akajitahidi kunisaidia. Baada ya kukaa kwa miezi miwili akawa amenifanyia mpango wa kazi ya ulinzi katika kampuni aliyokuwa anafanya yeye. Kwangu mimi ambaye sikupata mafunzo ya mgambo ilikuwa kazi ngumu na ya hatari lakini kutokana na shida nilijikaza kiume nikijua kwamba sikuwa na elimu na nisingeweza kupata kazi rahisi. Nilivyoonekana ni kijana na nina nguvu mara nyingi nilipangiwa kwenye malindo ya usiku. Silaha niliyopewa ni kirungu na sime, isitoshe hatukuwa tukipewa makoti ya kuzuia baridi. Kama ulihitaji koti ilikuwa ni juu yako mwenyewe kulinunua. Na pia kama watakuja majambazi wenye bunduki katika lindo lako wakati wewe una sime na kirungu pia ni juu yako mwenyewe kuokoa maisha yako. Kilichotakiwa pale uhakikishe eneo unalolinda liko salama hadi kunakucha. Siku za mwanzo mwanzo kabla sijalipwa mshahara wangu wa kwanza nilikuwa nikiteseka kwa baridi. Niliwahi kwenda na shuka nzito nikawa najifunika. Lakini mara nyingi ninapojifunika shuka na usingizi nao unakuwa jirani. Mjomba wangu alinishauri kwamba ukifika usiku wa manane nichome moto na vipande pande vya miti. Akaniambia nipendelee kuchoma majani ya mti wa mwarobaini kwani moshi wake unafukuza mbu. Tangu mjomba aliponiambia hivyo nikawa nawasha vipande vya miti ili kuota moto kisha nachoma majani ya muarobaini kwa ajili ya kufukuza mbu. Unapofika usiku mwingi ninaacha moto unawaka peke yake mimi mwenyewe ninapanda juu ya mti uliokuwa mbele ya ghala nililokuwa nikilinda na kujilaza kwenye matawi ya mti huo. Ule moshi wa muarobaini unaendelea kufuka na kufika juu ya ule mti hivyo mbu hupungua. Siku moja wakati nikiwa juu ya mti mvua ikanyesha, ule moto ukazimika. Mvua ilipokuwa inazidi nikaona nishuke kwenye ule mti kwani nilikuwa natota na sikuwa na koti. Wakati nataka kushuka nikaona gari aina ya Land Rover iliyokuja hadi mbele ya lile ghala ikasimama. Nilipoiona gari hiyo niliacha kushuka nikawa naitazama. Gari hiyo ilisimama mbele ya ghala hilo kwa kiasi cha dakika kumi hivi bila mtu yeyote kushuka. Nikapata wazo kwamba nishuke niende nikamuulize dereva wa gari hilo anataka nini, lakini wazo jingine likanikataza kwa kushuku kwamba wanaweza wakawa ni watu wabaya. Baadaye kidogo akashuka mtu mmoja akasimama kando ya gari na kuangalia kila upande kisha akaulia kwa sauti ya juu.
"Nani analinda hapa?........nani nalinda
hapa!"
Mimi sikujibu kitu. Nikaendelea kubaki kimya. Alipoona hapakuwa na jibu wala mtu yeyote anayetokea akasema.
"Tokeni"
Hapo hapo wakashuka watu watano kutoka katika gari hilo, mmoja alikuwa ameshika bunduki na wengine walikuwa na silaha za kijadi ikiwemo mitaimbo na koleo kubwa la kuvunjia makufuli. Hapo nikajua kuwa watu hao walikuwa majambazi. Baada ya kutoka kwenye gari walilizunguka lile ghala kisha watano wakaenda kwenye lango la ghala hilo na mmoja aliyekuwa na bunduki alisogea kwenye ule mti, akawa amesimama akiangalia huku na huku. Nikasikia kufuli moja likivunjwa kisha jingine na jingine tena. Makomeo ya chuma yaliyokuwa kwenye lango hilo yaling'olea kama mchezo. Wale jamaa walikuwa wanaume kweli kweli. Wakati huo mvua ilikuwa inaendelea kunyesha na watu hao walikuwa wanatota lakini hawakujali mvua. Mimi ndiyo nilikuwa nimetota chapa chapa lakini kutokana na lile tukio, kule kutota pia sikukujali. Nilikuwa nikifikiria jinsi ambavyo ningeweza kuokoa mali iliyopo kwenye ghala hilo isiibiwe. Tatizo lililokuwa hapo si idadi ya wale watu. Kwa vile nilikuwa na sime watu sita ningeweza kupambana nao, nilikuwa nikijiamini. Lakini ile bunduki ndiyo iliyonitisha. Usiku huo ndipo nilipogundua kwa vitendo matatizo ya kazi hizi za ulinzi wa usiku. Kwa vyovyote vile ilinipasa ninyamaze kimya na niwaache wavunje na kuchukua kila walichokuwa wanakitaka kwani nilijua nikijitia ubabe nitapoteza roho yangu. Lakini kama wataiba na kuondoka nini kitatokea? nikajiuliza na kujipatia jibu mwenyewe, kwamba atakayeshitakiwa ni mimi na kuhusishwa na wizi huo. Angalau majambazi hao wangenikamata na kunifunga ningekuwa na utetezi. Sasa nifanye nini? nikawa najiuliza lakini wale watu walishaingia kwenye ghala hilo.Baada ya nusu saa watakuwa wameshasafisha kila wanachokitaka na kuondoka kwa gari lao. Wao watafaidika kwa mali ya wizi, mimi ndiyo niingie kwenye matatizo. Haitawezekana! nikajiambia kijasiri. Nikashuka taratibu kwenye ule mti bila kusababisha sauti kusikika.
JE NINI KITATKEA? Hadithi
Itaendelea kesho. Usikose kufungua blogy hii mapema.
|
Sunday, April 24, 2016
HADITHI , SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA SEHEMU YA 1
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment