HADITHI na Faki A Faki 0655 340572
MWANAMKE Alienichunuka inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, Candle ni mabingwa wa kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu, Candle wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
ILIPISHIA
Nikamfuata yule msichana aliyekuja kuniita, nikaingia
naye ndani. Nilikuta watu mbalimbali waliovalia maridadi wameketi wakinywa
vinywaji na kushereheka.
Msichana huyo alinichukua hadi kwenye chumba kimoja ambacho alinionesha
bafu na kuniambia.
“Unatakiwa uoge, ukimaliza unakuja hapa kwenye kabati”
Alinifungulia kabati lililokuwa mle ndani ya kile chumba na kunionesha
nguo zilizokuwemo ndani.
“Utachagua suti utakayoipenda, utavaa na shati jeupe na viatu vyeupe.
Halafu utagonga mlango, mimi nitaingia ili nikupeleke kwa dada”
Kwanza
nilisita, nikataka kumuuliza kulikoni lakini nikaona nitekeleze vile
nilivyoagizwa.
Nikaoga. Nilipomaliza nilichagua suti ya kijivu niliyoipenda. Nikaivaa
pamoja na shati jeupe na viatu vyeupe.
Nilipomaliza niligonga mlango. Hapo hapo yule mtumishi akaingia.
SASA ENDELEA
“Umependeza. Sasa twende” akaniambia.
Nikaenda naye katika chumba kingine ambacho kilikuwa kimepambwa.
Nilimkuta yule msichana mwajiri wangu naye amepambwa. Alikuwa amekaa kwenye
kitanda huku wasichana wanne wakiwa wamesimama karibu yake kama
walinzi.
Niliogopa hata kuingia mle chumbani lakini yule msichana mwajiri wangu
aliponiona aliniambia.
“Ingia”
Nikaingia. Akanitazama kwa makini kisha akaniambia.
“Alfred umependeza leo!”
“Asante,
hata na wewe umependeza”
“Sogea karibu yangu’
Nikamsogelea. Alikuwa ananukia uturi (manukato).
“Inama nikuambie”
Nikainama.
Akaniambia kwenye sikio langu “ Samahani sikuwahi kukwambia, shughuli
hii ni yako wewe. Nilitaka kukushitukizia”
“Mh!. Unasema shughuili hii ni yangu mimi?” nikamuuliza baada ya
kutomuelewa.
“Ndiyo, ni yako wewe. Leo tutafunga ndoa usiku huu na hutakuwa mlinzi
wangu tena bali utakuwa bwana wa nyumba hii”
“Umesema utafunga ndoa na mimi usiku huu?” nilimuuliza kwa mshituko
uliochanganyika na kiwewe.
“Ndiyo, ni kwa sababu nilikupenda tangu nilipokuona ukilinda pale
dukani. Nikapanga uwe mume wangu”
Wakati akiniambia hivyo alikuwa anatabasamu huku akiniangalia kwa jicho
la huba.
Nilishindwa kujizuia na mimi nikamwambia.
“Kama ni kweli unayoniambia nitafufurahi kama
utakuwa mke wangu”
“Sasa ninamuita sheikh nimpe idhini atuozeshe”
Msichana akamtuma yule mtumishi amuite sheikh. Sheikh alipofika
msichana huyo akamwambia.
“Nimekuita kukupa idhini uniozeshe na Alfred na tangu sasa atakuwa
anaitwa Abubakar, jina ambalo nimemchagulia mimi”
“Nataka na idhini ya mzazi wako wa kiume” Sheikh akamwambia.
“Atakupa idhini huko huko”
“Twende bwana!” Yule sheikh akaniambia.
Nikatoka na yule sheikh nikiwa siamini yale yaliyokuwa yanatokea.
Tulikwenda sebuleni ambako watu mbalimbali walikuwa wamekaa. Katikati
ya sebule palitandikwa zulia dogo na palikuwa na watu wanne waliokuwa wamekaa
hapo. Wote wanne walikuwa wamevaa kanzu nyeupe na vilemba kama
waarabu.
Sheikh niliyekuwa nimefuatana naye alinishika mkono na kuniambia.
“Kaa hapa”
Alinionesha pale walipokuwa wamekaa watu wanne. Nikakaa na yeye akakaa
mbele yangu. Mtu aliyekuwa ameketi upande wake wa kulia alikuwa mzee aliyekuwa
na ndevu nyingi nyeupe.
Nikasikia akimwambia.
“Wewe ndiye walii (baba) wa bi harusi. Nataka idhini yako ili
nimuozeshe binti yako kwa Abubakar”
Ninakupa idhini” Yule mzee akamwambia kwa sauti ndogo.
Sheikh huyo akanishika mkono na kunifungisha ndoa ambayo sikuitarajia.
Baada ya kufungishwa ndoa nilipelekwa katika chumba alichokuwemo yule
msichana. Nikaambiwa nimpe mkono, nikampa mkono.
“Karibu kwenye nyumba yako mume wangu” Msichana huyo akaniambia kwa
furaha na kwa sauti ya unyenyekevu iliyotoka kwenye moyo wake. Hapo vigelegele
na chereko vilisikika nyumba nzima.
Mke wangu huyo akaniambia nikae kwenye kitanda karibu yake. Nikakaa.
Baadaye kidogo tuliletewa vyakula na vinywaji. Mke wangu akanikaribisha, tukala
pamoja. Hata hivyo mimi sikula sana
kutokana na kihoro kilichonipata ingawa chakula kilikuwa kitamu.
Baada ya kumaliza kula tuliachwa peke yetu. Msichana huyo akaniambia.
“Sasa tulale mume wangu. Hapa ni
kwako”
Tukalala hadi asubuhi.
Wakati huo wa asubuhi nyumba
ilikuwa kimya. Sikuona mtu yeyote humo ndani zaidi ya mke wangu na watumishi
wake wawili.
Wakati tunakunywa chai nilimuuliza.
“Wale watu wa jana usiku wamekwenda wapi?”
“Walienda zao usiku ule ule. Walikuja kwa ajili ya harusi yetu”
Tuliporudi chumbani msichana huyo akaniambia.
“Mimi napenda sana
kusimulia hadithi. Ngoja nikusimulie hadithi moja”
Nikamwamia “Nisimulie”
“Zamani kulikuwa na msichana mmoja mrembo ambaye alimpenda sana kijana mmoja ambaye
naye alikuwa mzuri. Msichana huyo alitamani sana kijana huyo awe mume wake lakini ikawa
vigumu kwa wawili hao kuoana”
“Kwanini ilikuwa vigumu, huyo kijana hakumpenda huyo msichana?”
nikamuuliza.
“Lahasha mume wangu. Ilikuwa vigumu kuoana kwao kwa sababu yule kijana
alikuwa binaadamu lakini yule msichana alitoka katika kizazi cha kijini”
“Enhe!. Halafu ikawaje?” nikamuuliza baada ya kuona hadithi yake
inafanana na kile kisa kilichonotokea mimi.
“Yule kijana alipogundua yule msichana ni jini alianza kumkimbia lakini
msichana huyo hakukata tamaa, aliendelelea kumfuatilia kijana huyo na kumrai na
kumueleza jinsi alivyokuwa anampenda”
Hadithi ile ilianza kunishangaza. Nikawa makini kuisikiliza ili nijue
mwisho wake.
ITAENDELEA KESHO hapahapa Tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment