HADITHI, SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA
SIMULIZI ZA FAKI A FAKI, 0655 340572
SITASAHAU NILIVYOGEUZWA
PAKA
Asubuhi nilipomuuliza,
Chausiku alikasirika akaja juu na kuniambia kuwa alikuwa ametoka barazani
kupunga upepo kwa sababu ya joto lililokuwemo ndani.
Nikamwaambia haikuwa
jambo zuri kutoka nje peke yake wakati wa usiku kwani anaweza kushambuliwa na
fisi wanaozunguka ovyo usiku kucha.
Chausiku akanyamaza
kimya.
Siku nyingine aliniaga
kuwa anakwenda kwa bibi yake mzaa mama yake aliyekuwa akikaa kijiji cha jirani.
Akaniambia atalala hukohuko na atarudi kesho yake.
Lakini akanionya kuwa
nisifungue chumba chake ambacho alikuwa akikitumia kama stoo yake. Baada ya
kile chumba tulichokuwa tunalala alikuwa na chumba kingine ambacho sikupata
kukiingia hata siku moja. Alikuwa akiingia yeye mwenyewe tu kuweka vitu vyake
pamoja na vyungu alivyokuwa anatengeza.
Siku ile alipoondoka
kwenda kumsalimia bibi yake, usiku wake nikaamua kuingia katika kile chumba
alichonikataza nisiingie.
Nilivizia watu wote
walikuwa wameshalala. Nikafungua mlango na kuingia huku nimeshika taa ya
kandili (Chemli) ili niweze kuona.
Hayo niliyoyakuta humo
chumbani sikuyatarajia kabisa. Yalikuwa ni maajabu yaliyonishitua sana!
SASA ENDELEA
Nilipoingia mle chumbani
nilishituka nilipomuona Chausiku ameketi kwenye kigoda kilichokuwa katikati ya
chumba hicho, ameelekea upande ule uliokuwa na mlango.
Alikuwa ametulia kimya
na amefumba macho kama aliyekuwa amelala.
"We Chausiku!"
nilimuita kwa kugutuka.
"Kelele!"
akaniambia kwa sauti tulivu bila kufumbua macho. "Si nilikuonya
usiingie katika chumba hiki?" akaniuliza.
"Nilikuwa natafuta
.....nilikuwa natafuta.....!"
"Toka!"
akaniambia kwa ukali akiwa bado amefumba macho yake vilevile.
Nikatoka huku
nikitetemeka kwa hofu. Nguvu ziliniishia kabisa mwilini.
Huyu mwanamke aliniaga
anakwenda kwa bibi yake tangu asubuhi. Kumbe amejifungia humu chumbani kwenye
giza na mbu, anafanya nini? nikawa najiuliza.
Nilirudi chumbani mwetu
nikaweka ile taa na kuketi kwenye kiti kutafakari. Baadaye
nilimuona akiingia mle chumbani huku akicheka.
"Nimekugundua sasa,
kwanza wewe si muaminifu na pili muoga" akaniambia huku akiketi kitandani.
"Kwanini unaniambia
hivyo?" nikamuuliza.
"Nilikuonya
usiingie katika kile chumba. Ulipoona nimeondoka ukaingia. Je ni uaminifu
huo?"
Nikanyamaza
kimya. Sikuwa na cha kumjibu.Ni kweli kuwa alinionya lakini nilivyoona
ameondoka nikaingia. kumbe na mwenyewe alikuwamo humo ndani.
"Halafu wewe ni
muoga sana" akaendelea kuniambia.
"Kumbe ulikuwa
unafanya nini mle chumbani?" nikamuuliza
"Nilitaka kukupima
wewe nione uaminifu wako kwangu na nione ujasiri wako. Sasa
nimeshakugundua"
Nikabaki kuguna tu.
Tukalala. Asubuhi
kulipokucha nikaenda zangu shambani kwangu. Ilipofika saa saba mchana mke wangu
akaja shamba kuniletea chakula.Ilikuwa ni kawaida yetu siku nikienda shamba mke
wangu kuniletea chakula.
Wakati ninakula
akaniambia kuwa mtoto wa jirani yetu mzee Juma amagongwa na nyoka na hali
yake si nzuri. Habari ile ikanishitua kwa sababu huyo mtoto alizoea
kucheza barazani mwa nyumba yetu na alikuwa mtoto mcheshi aliyependwa na kila
mtu.
"Amegongwa na
nyoka?" nikamuuliza mke wangu huku nikishangaa.
"Amegongwa kama saa
tano hivi"
"Wapi?"
"Huko nyumbani
kwao.Alikuwa akicheza na wenzake kwenye mti,kumbe palikuwa na nyoka
akamgonga"
"Nyoka wa rangi
gani?"
"Wenzake wanasema
ni nyoka wa rangi ya kijani"
"Nyoka wa kijani
wana sumu kali sana. Sasa wamempa dawa gani?"
"Babu yake anajua
dawa za nyoka, amemchanja akampaka dawa"
"Lakini umesema
hali yake si nzuri?"
"Walichelewa kumpa
dawa. Babu yake alikuwa shambani, mpaka anakwenda kuitwa, mtoto alikuwa
ameshalegea na mguu umevimba"
"Wangempeleka
hospitali Songe"
"Mh! watu wa hapa
wanaamini zaidi dawa zao za kiasili kuliko za hospitali"
''Lakini kama mtoto
amelegea kiasi hicho wangempeleka hospitali tu"
"Nitakwenda
kuwashauri wampeleke hospitali"
"Nikirudi
nitakwenda kumuangalia"
Nilipomaliza kula mke
wangu alichukua vyombo akarudi nyumbani.
Nilirudi kutoka shamba
majira ya saa kumi jioni. Sikuona dalili nzuri nyumbani kwa mzee Juma.Nilikuta
watu wamejazana barazani na huko ndani kulikuwa na sauti za watu wanaolia. Hapo
hapo nikajua nini kimetokea. Niliingia nyumbani mwetu nikaweka jembe. Mama
mmoja mkazi wa mle ndani akaniambia "Nyumba ya pili kumefiwa"
"Nani aliyekufa?"
nikamuuliza lakini tayari nilikwisha jua
"Ni Hamisi, mtoto
wa mzee Juma.Amegongwa na nyoka asubuhi, wamemchelewesha kumpeleka hospitali
hivi jioni amekufa"
"Na mke wangu yuko
hukohuko?"
"Tulikuwa naye
hukohuko kwenye msiba. Mimi nimerudi mara moja tu kumpikia mume wangu.Je
unataka nikuitie?"
"Hapana.Mimi pia
nitakwenda hukohuko.Mke wangu alikuja shambani kuniambia kuwa Hamisi amegongwa
na nyoka. Nikamwaambia kwanini baba yake hakumpeleka hospitali. Kumbe
wamemuacha mpaka amekufa"
"Babu yake alikuja
kumpa dawa lakini haikusaidia"
"Nyoka wa kijani
wana sumu kali sana"
Baada ya kuzungumza na
yule mama nikatoka kwenda kumpa pole mzee Juma na kumuuliza juu ya mipango ya
maziko.Akaniambia wamepanga kumzika mtoto wao kesho yake asubuhi.
Asubuhi mimi na mke
wangu tukaenda kwa jirani yetu kuhudhulia maziko.Muda ulipowadia jeneza
lilibebwa kuelekea eneo la makaburi ambalo halikuwa mbali sana.Tukamzika yule
mtoto kisha tukarudi
Siku ile tulishinda
nyumbani kwa mzee Juma kumfariji mwenzetu.Mke wangu alikuwa miongoni mwa akina mama
waliokuwa wakishughulika kupikia wageni kama ilivyo kawaida ya mahali
panapotokea msiba. Ilipofika usiku mimi na mke wangu tukarudi nyumbani kulala.
Nilikuja kushituka usiku
wa manane. Nikamuona mke wangu anashuka kitandani. Nikanyamaza kimya na
kujifanya kama nimelala.Akajifunga upande wa kaniki kisha akaniita mara tatu.
lakini sikumjibu kitu.
Akatoka mle chumbani.Alipotoka na mimi nikashuka kitandani, nikanyata hadi
mlangoni kumchungulia. Nikamuona ameingia katika kile chumba cha pili. Baadaye
kidogo akatoka, mimi nikarudi kitandani. Akaingia tena mle chumbani na
kunichungulia.Mkononi alikuwa ameshika kitu ambacho sikuweza kukiona vizuri kwa
sababu nilikuwa namwaangalia kwa kumuibaiba.
Nilitulia kimya pale
kitandani, nikasikia akifungua mlango wa nje.Nikainuka na kwenda
kumchungulia.Nikamuona anatoka na kuufunga mlango.Nilisubiri kwa dakika chache
kisha nikaenda kwenye mlango huo. Nikaufungua taratibu na
kumchungulia.Nikamuona anapotea kwenye kiza upande wa kushoto mwa nyumba yetu
ambako palikuwa na pori.
Yule msichana anakwenda
wapi usiku huu? nikajiuliza kwa mshangao bila kupata jibu. Nikatoka nje na
kuufunga mlango.Niliamua kumfuatilia ili nijue anakwenda wapi.
Kulikuwa na baridi
l;akini sikuisikia kwa sababu ya kutaharuki. Nilipoingia kwenye lile pori
nilimuona Chausiku ametokea upande wa pili wa pori hilo na kuendelea
kwenda.Nami niliendelea kumfuatilia taratibu huku nikijifichaficha kwenye miti
ili asinione.
Nikaendelea kumfuatilia
hadi kwenye eneo la makaburi mahali ambako kwa usiku ule palikuwa panatisha
kweli kweli na isingekuwa rahisi kwa mtu yeyote mwenye akili zake timamu kufika
mahali hapo wakati ule usiku akiwa peke yake tena bila taa na akionekana hana
wasiwasi.
Mh! Makubwa! Haya huyo
msichana anakwenda wapi usiku huo? Hebu endelea kufuatilia hadithi hii ya kusisimua katika blogy hii hapo kesho.
No comments:
Post a Comment