Monday, April 25, 2016

HADITHI, SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA SEHEMU YA 2

HADITHI na Faki A Faki , 0655 340572, 0713 340572
SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA 2
ILIPOISHIA
Wakati huo mvua ilikuwa inaendelea kunyesha na watu hao walikuwa wanatota lakini hawakujali mvua. Mimi ndiyo nilikuwa nimetota chapa chapa lakini kutokana na lile tukio, kule kutota pia sikukujali. Nilikuwa nikifikiria jinsi ambavyo ningeweza kuokoa mali iliyopo kwenye ghala hilo isiibiwe. Tatizo lililokuwa hapo si idadi ya wale watu. Kwa vile nilikuwa na sime watu sita ningeweza kupambana nao, nilikuwa nikijiamini. Lakini ile bunduki ndiyo iliyonitisha.

Usiku huo ndipo nilipogundua kwa vitendo matatizo ya kazi hizi za ulinzi wa usiku. Kwa vyovyote vile ilinipasa ninyamaze kimya na niwaache wavunje na kuchukua kila walichokuwa wanakitaka kwani nilijua nikijitia ubabe nitapoteza roho yangu.

Lakini kama wataiba na kuondoka nini kitatokea? nikajiuliza na kujipatia jibu mwenyewe, kwamba atakayeshitakiwa ni mimi na kuhusishwa na wizi huo. Angalau majambazi hao wangenikamata na kunifunga ningekuwa na utetezi.

Sasa nifanye nini? nikawa najiuliza lakini wale watu walishaingia kwenye ghala hilo.Baada ya nusu saa watakuwa wameshasafisha kila wanachokitaka na kuondoka kwa gari lao. Wao watafaidika kwa mali ya wizi, mimi ndiyo niingie kwenye matatizo.

Haitawezekana! nikajiambia kijasiri. Nikashuka taratibu kwenye ule mti bila kusababisha sauti kusikika.
SASA ENDELEA
Yule mtu aliyesimama kando ya mti akiwa na bunduki alikuwa amenipa mgongo na bunduki aliishika kwa mkono mmoja akiwa ameielekeza chini. Mara kwa mara alikuwa akifuta maji ya mvua kwenye uso wake ili aweze kuona vizuri.

Nilipofika chini ya mti huo nilichomoa sime yangu nikaipunga na kuanza kumnyatia mtu huyo kwa nyuma. Kutoka shina la mti na mahala aliposimama yeye kulikuwa ni hatua tano. Nikapiga hatua ya kwanza...ya pili...ya tatu...ya nne. Sikutaka kumfikia karibu kabisa. Nikainua sime juu kisha nikaishusha kwenye kiganja cha mkono wake ulioshika bunduki.
 Nukta mbili baadaye kiganja na bunduki vikawa chini. Mtu huyo aliruka na kugeuka nyuma akiwa ameushika mkono wake nilioukata. Nikamkabili na kuipunga sime kwa mara ya pili, nikamchanja kwenye bega. Akageuka na kwenda mbio huku akipiga kelele. Nikainama na kuchukua ile bunduki.

Wenzake waliposikia kelele walitoka haraka kwenye ghala na kumulika tochi. Walimuona mwenzao akikimbilia kwenye gari lao huku damu inamtoka. Wakaniona na mimi nimeshika ile bunduki nikiwaelekezea. Watu hao wakashangaa. Nikafyatua risasi kwenye lango la ghala. Jambazi mmoja alianguka palepale, wenzake wengine walitoka mbio kukimbilia kwenye gari.

Sikutaka kufyatua risasi nyingene kwa sababu sikujua bunduki ile ilikuwa na risasi ngapi kwani haikuwa aina ya bunduki za kijeshi zinazokaa risasi nyingi.Ilikuwa bunduki ya kiraia ambayo aghalabu hukaa risasi mbili tu.

Hivyo niliona nikifyatua risasi ya pili na kama bunduki yenyewe ilikuwa na risasi hizohizo mbili nitakuwa nimejimaliza mwenyewe.Majambazi hao kwa kujua kuwa nimemaliza risasi zilizokuwemo wanaweza kunivamia kwa hasira na kunikatakata kwa mapanga na kupata nafasi ya kuendelea na ujambazi wao.Kufa kwa mwenzao mmoja niliyempiga risasi na kumkata mwenzao mwingine kwa sime kusingewazuia wasiendelee na uporaji huo.

Majambazi hao walijipakia kwenye gari lao haraka haraka na kuliondoa kwa kasi.

Mvua iliyokuwa inanyesha nayo ikaacha.Kwa nukta kadhaa nilisimama nikiliangalia gari hilo lilivyokuwa linakwenda mbio bila kuamini kuwa niliweza kuwasambaratisha majambazi hao waliotaka kuniharibia kitumbua changu.

Sikuweza kuamini kuwa nilikuwa nimewashinda. Na ndani ya moyo wangu sikuona fahari juu ya ushindi huo kwani nilifikiria mengi. Kwanza nilifikiria kwamba nimeshaua na nimeshamkata mmoja wao kiganja cha mkono. Kitendo cha kuua mtu na kumkata mtu kiungo cha mwili vilinitia hofu kwa vile katika maisha yangu sikutarajia kuwa ningekuja kutenda vitendo kama hivyo.

Lakini hili linaweza kuonekana si jambo la msingi sana kunitia hofu. Pengine jambo la msingi ni kufikiria kwamba wale majambazi wanaweza kurudi tena wakiwa na bunduki nyingine kwa ajili ya kulipa kisasi.

Wazo hilo ndilo hasa lililonitia hofu. Hata hivyo nilijikaza kiume nikaenda pale alipoanguka yule mtu niliyempiga risasi nikamuangalia na kuona alikuwa ameshakufa, risasi niliyoifyatua ilikuwa imempiga kifuani. Koti alilokuwa amevaa lilikuwa limetapakaa damu.

Nikarudi tena kwenye ule mti nikauegemea na kusimama hapohapo huku macho yangu yakitazama kwa kila upande.Nikajiambia nikiona gari linakuja nitakimbia na kwenda kujificha mahali penye giza .

Laiti kama kituo cha polisi kingekuwa karibu na hapo ningekimbia mara moja na kuwaita polisi lakini kituo kilikuwa mbali na hapo. Vilevile hapakuwa na mlinzi wenzangu aliyekuwa karibu.

Nikaendelea kusimama kwa muda mrefu.Nilipochoka nilikaa chini kwenye tope. Muda ulizidi kwenda mpaka nikaona kumekucha. Ghala ninalolilinda linalindwa usiku na mchana.Wakati mimi ninalinda usiku kuna mwenzangu mwingine anayenipokea zamu saa kumi na mbili asubuhi lakini anachelewa kufika. Badala ya saa kumi na mbili anaweza kuja saa moja au saa moja na nusu.

Siku ile ilikuwa ni bahati, aliwahi kuja.Kwanza alishangaa kunikuta nimeshika bunduki kisha akaona lango la ghala limevunjwa na kuna maiti iliyolala katikati ya lango hilo huku damu ikiwa imesambaa chini.

“Mgosi vipi tena?” mlinzi mwenzangu aliyekuwa akiitwa Mbwana aliniuliza akiwa ameshituka  “Naona umeshika bunduki na ghala limevunjwa na kuna maiti hapa!”

“Jamaa wamekuja kuvunja usiku”

“Halafu ikawaje?”
Nikamueleza na kumuonyesha kile kiganja cha mkono wa jambazi nilichokikata kwa sime.

“Kumbe palipita patashika!”

“Ni patashika kubwa.Hivi nilikuwa ninakusubiri ili nikimbie ofisini kutoa taarifa halafu tukatoe taarifa polisi”

“Yaani mimi ndiyo nibaki na hii maiti?”

“Ndiyo baki nayo” nikamwaambia na kuchapuka kuondoka katika eneo hilo .

Nilifika katika ofisi yetu iliyopo katikati ya mji wa Handeni. Afisa wetu alikuwa tayari ameshafika. Nikamueleza kilichotokea. Akaniambia. 

“Hebu twende”

Tukaondoka tena kurudi katika eneo la tukio.Baada ya afisa wetu kujionea mwenyewe hali ilivyokuwa akaniambia,

“Twende polisi haraka”

Tukaenda kituo cha polisi huku njia nzima akinimwagia sifa kwa kuokoa mali zilizokuwemo kwenye lile ghala.

Tulipowapa taarifa polisi, polisi watatuwakatupakia kwenye gari na kwenda nao katika eneo la tukio.Hapo nilihojiwa maswali na nikajibu kila nilichoulizwa.Baada ya hapo polisi hao waliichukua ile maiti na ile bunduki ya majambazi pamoja na kile kiganja. Wakaniambia nirudi nyumbani lakini saa tatu nifike kituo cha polisi kuandika maelezo.

Polisi hao wakaondoka na ile maiti.Afisa wetu akaniruhusu niende nyumbani kubadili nguo kwani zilikuwa zimetota na kujaa tope.Nikarudi nyumbani.Nilimueleza mjomba kilichotokea.Akanipa moyo kwa kuniambia.

“Hayo ni matukio ya kawaida katika kazi zetu lakini umefanya kitendo cha kijasiri”

Ilipofika saa tatu nikawa kituo cha polisi.Nilikuwa nimeshaoga na kubadili nguo isipokuwa si kunywa chai kwa sababu ya wasiwasi.

Nikiwa kituo cha polisi niliingizwa katika ofisi ya afisa upelelezi ambaye alichukua maelezo yangu.Baada ya kumaliza kuchukua maelezo yangu alinipongeza kutokana na ujasiri wangu.

Tukio hilo la ujambazi lilisababisha nipande cheo kazini kwangu.Nikavalishwa v mbili begani. Pia ukawa ndiyo mwanzo kwa walinzi wa usiku wanaolinda sehemu nyeti kupewa bunduki. Kwa vile mimi nilikuwa sijapata mafunzo ya kutumia bunduki nilipewa lindo jingine la mchana kwa wiki nzima huku nikipewa mafunzo ya jinsi ya kutumia bunduki na kulenga shabaha.

Je nini kitatokea? Endelea kufuatilia hadithi hii ya kusisimua katika blog hii kila siku bila kukosa.

No comments:

Post a Comment