HADITHI na Faki A Faki, 0555340572, 0713 340572
MWANAMKE ALIYENICHUNUKA 21
ILIPOISHIA
Tuliporudi chumbani msichana huyo akaniambia.
“Mimi napenda sana
kusimulia hadithi. Ngoja nikusimulie hadithi moja”
Nikamwamia “Nisimulie”
“Zamani kulikuwa na msichana mmoja mrembo ambaye alimpenda sana kijana mmoja ambaye
naye alikuwa mzuri. Msichana huyo alitamani sana kijana huyo awe mume wake lakini ikawa
vigumu kwa wawili hao kuoana”
“Kwanini ilikuwa vigumu, huyo kijana hakumpenda huyo msichana?”
nikamuuliza.
“Lahasha mume wangu. Ilikuwa vigumu kuoana kwao kwa sababu yule kijana
alikuwa binaadamu lakini yule msichana alitoka katika kizazi cha kijini”
“Enhe!. Halafu ikawaje?” nikamuuliza baada ya kuona hadithi yake
inafanana na kile kisa kilichonotokea mimi.
“Yule kijana alipogundua yule msichana ni jini alianza kumkimbia lakini
msichana huyo hakukata tamaa, aliendelelea kumfuatilia kijana huyo na kumrai na
kumueleza jinsi alivyokuwa anampenda”
Hadithi ile ilianza kunishangaza. Nikawa makini kuisikiliza ili nijue
mwisho wake.
SASA ITAENDELEA
“Basi kuna siku msichana yule wa kijini alimchukua kijana yule kwa hila
na kwenda kumuonesha mama yake huko kwao ujinini, Mama yake alipomuona kijana
huyo alimuuliza kama amekubali kuoana na binti
yake. Kijana kwa sababu ya hofu yake alijibu hakukubali. Basi mama mtu
alikasirika na akamkataza mwanawe aache kumfuta kijana yule kwa sababu hamtaki”
Wakati mke wangu anaendelea kunisimulia hadithi ile nilikuwa
nimemtumbulia macho kumsikliza. Akaendelea.
“Basi yule msichana kwa vile alikuwa amempenda sana kijana yule alifanya mpango mwingine
ambao ulifanikisha dhamiri yake ya kuoana na msichana yule. Na hadithi yangu
imeishia hapo”
“Kumbe baadaye walikuja kuoana?” nikamuuliza.
“Ndiyo, walioana”
“Huyo kijana hakuwa na uoga tena na huyo jini?”
“Hakuwa na uoga tena”
“Hicho kisa kinafanana na kisa kilichonitokea mimi, lakini mimi
sikuoana naye”
“Alah! Wewe pia kilikutokea kisa kama
hicho?”
“Kilinitokea”
“Sasa kwanini hamkuoana?”
“Nisingeweza
kuishi na jini”
“Mbona umeoana naye?”
“Hapana , sikuoana naye. Alinipeleka kwao nikamkataa, sikumuona tena”
Mke wangu huyo akatabasamu.
“Mmeoana bwana na ndiye mke uliyenaye na unampenda sana”
“Mimi sina mke mwingine zaidi yako’
“Basi huyo jini nitakuwa mimi!”
Aliponiambia hivyo nilishituka.
“Mke wangu acha utani, wewe siye yule. Kwanza hamlingani kabisa”
“Unajuaje kama nimejibadili ili usinitambue?”
“Unataka uniambie wewe ni Banuna mwana wa Ziraili?”
“Naam!”
“Siamini mpaka nikuone katika sura ileile”
“Nihakikishie kama utaendelea kunipenda iwapo nitakuwa kwenye sura
yangu”
“Nakuhakikishia kuwa nitaendelea kukupenda kwa maana tumeshaoana”
“Asante.
Sasa fumba macho yako”
Nikafumba macho yangu. Muda ule ule akaniambia.
“Fumbua sasa”
Nikafumbua macho na kumtazama. Nilishituka sana nilipoona sura yake ilikuwa imebadilika
na kuwa ya Banuna.!
“Kumbe kweli wewe ni Banuna mwana wa Ziraili!” nikamwambia.
“Umeamini sasa?” akaniuliza huku akitabasamu.
Alipoona nimeshikwa na mshangao, alinikumbatia haraka na kunibana
kwenye kifua chake. Nilisikia faraja sana.
“Nakupenda mume wangu, niambie kama na
wewe unanipenda” akaniambia.
Nikajikuta nikimwambia.
“Na mimi nakupenda pia”
“Asante
mume wangu. Nakuahidi kuwa nitakuenzi na nitakupa utajiri usioutarajia maishani
mwako”
“Nitafurahi”
Naam. Miaka sita sasa imepita tangu tukio hilo la ajabu linitokee. Nataka niwambie kuwa
nimekuwa tajiri kama msichana huyo wa kijini
alivyoniahidi.
Si tajiri wa pesa tu bali tajiri wa miradi. Nina miradi mbali mbali ya
kiuchumi iliyonifanya niishimike mjini. Unaponiona huwezi kunidhania kuwa miaka
sita iliyopita nilikuwa korokoroni niliyekuwa nikilinda maghala.
Tena nikiwa muajiriwa wa makampuni ya ulinzi ambaye mshahara wangu
haukufika hata shilingi laki moja!
Raslimali iliyokuwamo chumbani
mwangu wakati huo kilikuwa kitanda cha bei rahisi na kimeza kilichochochakaa.
Nashukuru kwamba Banuna alikuwa ameniwezesha!
Mke wangu huyo nilikuwa ninaendelea kuishi naye hadi ninaposimulia kisa
hiki. Ananipenda na mimi nampenda.
Kwa kweli tunapendana mapenzi ya dhati na ya kweli. Amenionesha mahaba
ya kijini ambayo sijapata kuyaona maishani mwangu.
Katika kipindi nilichoishi naye Banuna ameshapata ujauzito mara mbili
lakini watoto alikwenda kuwazalia kwao. Mtoto wetu wa kwanza alikuwa mwanamke
wa pili alikuwa mwanaume.
Mara moja moja anawaleta pale nyumbani niwaone wanangu halafu
anawarudisha kwao. Ameniambia watoto hao hatuwezi kuishi nao pale nyumbani
wakiwa wadogo kwa sababu ni majini.
Licha ya unyenyekevu alionao Banuna, ni mkali na ana wivu wa
kupindukia.
MWISHO, Kila siku asubuhi na mapema Tangakumekuchablog inakuletea hadithi tamu na ya kusisimua, fuatilia simulizi hii hapa hapa Tangakumekuchablog
|
Friday, April 22, 2016
HADITHI, MWANAMKE ALIENICHUNUKU SEHEMU YA 21
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment