Tangakumekuchablog
Tanga, WAPENZI
na washabiki wa soka Tanga wameingiwa na
kiwewe cha kuzipoteza timu zao tatu kushiriki ligi kuu Tanzania Bara msimu ujao
na kuwataka viongozi wa Mkoa kuungana kutoa msukumo kwa makocha na viongozi ili
kushinda michezo iliyoko mbele yao.
Wakizungumza na Mwanaspoti kwa
nyakati tofauti leo, Kamishna wa Chama Cha NCCR Magezi Tanga, Ramadhani
Manyeko, alisema tatizo liko kwa viongozi kwani wachezaji wamekuwa wakionyesha
kandanda safi uwanjani.
Alisema wachezaji wamekuwa
wakionyesha mchezo mzuri uwanjani na wamekuwa wakijituma lakini wamekuwa
wakikatishwa tama baada ya kukosa ushirikiano hivyo kutaka kipindi hiki cha
lala salama kushikamana na kuwa kitu kimoja.
“Ni jambo ambalo huwezi kuamini timu
tatu kutoka mkoa mmoja zinachungulia tanuri, hapa kwetu kuna namna na sisi
wapenzi wa soka tunawashushia viongozi wetu” alisema Manyeko na kuongeza
“Timu kama Coastal imeifunga Simba na kutoa upinzani mkubwa kwa Yanga, hapa
utasema timu ni mbovu, hebu tuutafute muarubaini kabla kipenga cha kuisha msimu
wa ligi” alisema
Alisema endapo timu zote tatu
zitateremka daraja soka la Tanga litakufa na ni ndoto kurudi ligi kuu kwa miaka
ya karibuni na wachezaji wengi wataibukia timu za nje ya Mkoa huo.
Kwa upande wake shabiki wa mpira
mkazi wa Mikanjuni Tanga, Habib Swaleh, aliwataka viongozi wa Serikali na Mkoa
kuzipa ushirikiano timu zote tatu, Coastal Union, African Sports na Mgambo ili
ziweze kunusurika na janga la kushuka daraja.
Alisema itakuwa aibu uwanja wa
Mkwakwani kuchukuliwa na timu za nje na kuufanya uwanja wa nyumbani ilhali zipo
timu tatu ambazo zimekuwa zikionyesha upinzani kwa timu shiriki za ligi kuu
Tanzania Bara.
Alisema ili kuweza kuzinusuru timu
na soka la Tanga ni wajibu wa viongozi wa mpira na viongozi wa Serikali kukaa
chini na kutafakari namna ya kuzinusuru timu hizo kutumbukia janga la kushuka
daraja.
“Tuko na uwanja mzuri ambao ni wa
pili nchini kwa uzuri na ubora lakini tunashuhudia tukiuwacha uote nyasi ili
kupata majani ya kulisha ng’ombe na mbuzi” alisema Swaleh
Alisema kama viongozi wako na
dhamira ya kweli timu za Tanga timu mbili zinaweza kubaki ligi kuu msimu ujao
hivyo wakazi wa Tanga macho yao yako kwa viongozi wa soka na Serikali.
Mwisho
No comments:
Post a Comment