HADITHI na Faki A Faki 0655 340572, 0713 340572
MWANAMKE ALIYENICHUNUKA 15
ILIPOISHIA
Mara nikaona taa inawashwa.
“Alfred ulitoka saa ngapi, mbona mlango umefungwa kwa ndani?” Sauti ya
Juma ikauliza kutoka ndani.
“Nifungulie, nitakueleza”
Baada ya ukimya wa dakika mbili hivi, Juma akafungua mlango wa nje.
“Ulitokaje humu ndani?”
“Tuingie ndani nikueleza”
Tukaingia ukumbini. Juma akaufunga mlango wa nje kisha tukaingia
chumbani. Mimi nilikaa kwenye kiti, Juma akakaa kwenye kitanda.
SASA ENDELEA
“Juma utashangaa nikikueleza kuwa Banuna alikuja kunichukua huu usiku
na kunipeleka kwao ujinini chini ya bahari!” nikamwambia Juma.
“Unasema kweli Alfred?”
“Huwezi kuamini Juma lakini hivi ninavyokwambia ninatoka ujinini”
“Alikuja kukuchukua saa ngapi?”
“Sijui ilikuwa saa ngapi lakini alinipeleka baharini, tukazama chini ya
bahari na kukuta mji wao”
“Acha bwana!. Mji uko chini ya bahari!”
Hapo nikamueleza Juma jinsi nilivyoondoka na Banuna, tulivyozama chini
ya bahari na kutokea katika mji wa majini. Pia nilimuelezea yale yaliyotokea
wakati tulipokuwa ndani ya jumba la majini hao lenye mnara mrefu.
“Mama yake amekataa msioane?” Juma akaniuliza baada ya kumueleza kisa
kizima.
“Amekataa. Nafikiri yule mama alitaka nikubali mwenyewe na sio
kulazimishwa kama anavyotaka Banuna”
“Sasa itakuwaje, kwa maana kesho ndio napata
mshahara ambao tumepanga nikupe uende Zanzibar?”
“Banuna alipokatazwa asinifuate, alisema kwa kiburi kuwa atanifuata.
Sasa sijui itakuwaje!”
“Kama mama yake amemkataza, unadhani
anaweza kuendelea kukufuata kweli?”
“Amesema ataendelea”
“Labda amesema kwa hasira tu”
“Siwezi kujua. Na hata alipoambiwa anirudishe huku alikataa.
Nimerudishwa na jini mwingine”
“Sasa unaweza kwenda Zanzibar
kesho lakini Banuna akawa hana shughuli na wewe tena. Hapo ni sawa na kuharibu
pesa bure. Au unaweza usiende lakini keshokutwa ukaona amekufuata”
“Hapo ndipo penye utata”
“Sasa tusubirishe kwanza tuangalie. Kama
atakutokea tena utakwenda”
“Sawa”
Nikaendelea kuzungumza na Juma hadi asubuhi kwani hatukulala tena.
Kutoka siku ile ulipita mwezi mzima sikumuona Banuna. Hapo nikapata
uhakika kuwa Banuna alishaamua kuachana na mimi kwa sababu haikuwa kawaida yake
kupitisha hata wiki moja bila kunitokea.
Ile hofu niliyokuwa nayo ya kupata vitisho vya Banuna, sasa
ikaniondoka. Nikaamua kurudi chumbani kwangu.
Maisha sasa yakawa ya utulivu na ya amani. Siku moja nilipata barua ya
kuitwa katika kampuni moja ya ulinzi ambako nilikuwa nimeomba kazi. Nikaenda.
Nilifanyiwa usaili na baadaye niliambiwa niende kesho yake kuanza kazi.
Siku iliyofuata nilipokwenda niliajiriwa kazi ya ulinzi. Nilipewa sare
za kampuni nikavaa a kupelekwa kwenye duka la muasia mmoja kuanza kazi ya
ulinzi wa duka hilo.
Nilikuwa naingia kazini saa mbili asubuhi na kutoka saa kumi jioni.
Nikishakunywa chai asubuhi ndiyo nashinda hadi saa kumi jioni ninapotoka na
kurudi nyumbani. Kuanzia saa kumi anaingia mlinzi mwingine ambaye anaendelea
hadi asubuhi ya siku ya pili.
Zamu hizo zilikuwa zinabadilika kwa wiki. Anayeingia mchana
anabadilishiwa zamu na kuingia usiku.
Katika juma lile la kwanza nilikuwa nimepangiwa zamu ya mchana. Hii
ilikuwa nzuri kwani iliniwezesha kulala nyumbani kuliko zamu ya usiku ambapo
unalazimika kukesha macho usiku kucha.
Siku tatu baada ya kuanza kazi yangu alikuja msichana mmoja wa kiarabu
pale dukani. Akanunua vitu vingi. Alipokuwa anatoka nikamsaidia boksi moja na
kumpelekea kwenye gari lake. Akanishukuru kisha akanipa shilingi elfu ishirini kama bahashishi yangu.
Kwanza
sikuelewa pesa hizo alizonipa zilikuwa za nini. Nikawa nimeduwaa na kumuangalia
ili aniambie pesa hizo zilikuwa za nini.
“Ni zako. Nimekupa kwa msaada wako” akaniambia huku akifungua mlango wa
gari hilo na
kujipakia.
Kwa kweli nilimshangaa msichana huyo kwa kunipa pesa zote hizo kwa
msaada mdogo tu. Hata hivyo nilishukuru na kuzitia mfukoni. Msichana huyo
akaliwasha gari na kuondoka.
Nikarudi kwenye kiti changu kilichokuwa kando ya mlango wa duka hilo, nikaendelea na kazi
yangu. Kabla ya wiki ile kumalizika yule msichana alikuja tena pale dukani. Kwa
bahati mbaya vitu alivyotaka kununua havikuwepo. Alipotoka akanipa tena
shilingi elfu ishirini kisha akaenda kwenye gari lake na
kuondoka.
Siku nyingine tena wakati niko katika zamu ya mchana, msichana huyo
akaja tena Nakumbuka ilikuwa saa kumi wakati nabadilishana zanu na mlinzi
mwenzangu. Msichana huyo hakushuka kwenye gari. Alisubiri mpaka wakati naondoka
akanifuata na gari na kusimama karibu yangu. Na mimi nikasimama.
Msichana huyo alitoa kichwa kwenye dirisha la gari na kuniambia.
“Kijana hujambo?”
“Sijambo. Habari yako?”
“Nzuri. Unarudi nyumbani?”
“Ndiyo,ninarudi nyumbani”
“Ingia garini nikupeleke. Nina mazungumzo na wewe!”
“Una mazungumzo na mimi?” nilimuuliza kama
vile sikumsikia vizuri.
“Mbona umeshituka?”
“Hapana, sikushituka”
“Basi ingia garini”
Nikafungua mlango wa upande wa pili wa dereva na kujipakia. Msichana
akalindoa gari.
ITAENDELEA KESSHO hapaha Tangakumekuchablog
|
Saturday, April 16, 2016
HADITHI, MWANAMKE ALIENICHUNUKU SEHEMU YA ( 15)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment