Thursday, April 28, 2016

HADITHI SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA SEHEMU YA 4

HADITHI

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI, 0713 340572

SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA 4 inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, Candle ni mabingwa wa kufaulisha wanafunzi wanaorisiti mitihani yao na wafanyakazi maofisini, Candle wapo Tanga mkabala na bank ya CRDB simu 0715 772746

ILIPOISHIA

Kawaida yetu ni kuwa ninaporudi kutoka kazini huniuliza kuwa aniwekee chakula au maji ya kuoga. Lakini siku ile hakuniuliza chochote. Ikabidi nimwaambie mwenyewe. 

"Nimwekee chakula"

"Sikupika" akanijibu haraka.

"Hukupika kwa nini?"

"Si nilikwenda harusini?"

"Ukenda harusini ndiyo hupiki?"

"Ah! nimechoka bwana, nimerudi sasa hivi!"

"Sasa kama wewe umekula harusini mimi nikale wapi?"

"Lakini si umeniruhusu mwenyewe niende?"

"Hilo sio swali langu. Nimekuuliza kama hukupika mimi nikale wapi?"

"Lakini uliniruhusu mwenyewe!"

"Kwamba usipike?"

"Niende harusini"
"Lakini sikukuambia nenda harusini lakini usipike. Kama umesharudi huko harusini kwanini hukupika?"

Nilipomuuliza hivyo alikunja uso akaguna. Jambo hilo liliniudhi nikakasirika.

SASA ENDELEA

Alipoondoka kitandani ili aende akapike nikamzuia.

"Basi endelea kulala......unakwenda wapi.....wewe si unajifanya jeuri!"

Lakini hakunisikia akatoka kwenda uani. Ilimchukua saa nzima kutayarisha ugali kwa mboga ya mrenda na perege wa kuchoma. Aliponiwekea kwenye meza nikaisukuma sahani ya ugali ikaanguka chini na kuvunjika.

"Unamuwekea nani?....kwenda zako!" nikamwaambia kwa ukali  "Si nilikwambia basi, sitaki chakula?"

"Sasa ndiyo uisukumie chini sahani ya ugali?" akaniuliza naye akinionesha kukasirika.

"Tena ushike adabu yako, nitakupiga sasa hivi!" nikamwaambia kwa sauti ya ghadhabu huku nikinyanyuka kwenye kiti.

Mke wangu alipoona nimehamaki hakusema tena.Aliinama akauokota ule ugali ulioanguka pamoja na vipande vya sahani akatoka navyo uani. Na mimi nikatoka kwenda mtaa wa pili ambako kulikuwa na baraza ya kahawa. Nikakaa na kuzungumza na wenzangu.

Ilipofika saa mbili usiku nilikwenda kula kwa mamalishe kisha nikarudi nyumbani.Kwa vile nilikuwa nimekasirika sikuzungumza na mke wangu.Nilikwenda bafu kuoga kisha nikarudi kulala.

Asubuhi kulipokucha nilioga nikavaa nguo zangu za kazini.Sikusemeshana lolote na mke wangu.Nilimuachia pesa yake ya matumizi mezani kisha nikatoka.

Nilivyotoka kumbe na yeye alitoka kwenda katika kijiji kimoja kilichokuwa jirani. Alikwenda kumchukua  dada yake aje atupatanishe.

Siku ile nilirudi usiku kutoka kazini. Kilichonifanya nichelewe kurudi ni kwamba mwenzangu aliyetakiwa kuja kunitoa katika lindo alipata dharura akachelewa. Isitoshe nilipotoka katika lindo nilipitia kwa mamalishe nikala chakula ndio nikarudi nyumbani.

Nilipofika nilimkuta mke wangu na dada yake Mkiwa. Tukaulizana hali. Akaniambia alikuwa arudi kijijini kwao jioni ile lakini kwa vile nilichelewa kurudi ilimbidi anisubiri.

Baada ya kuoga mke wangu aliniwekea chakula lakini sikukila. Sikukila kwa sababu kwanza nilikuwa nimeshakula na pili zile chuki za jana yake nilikuwa bado ninazo.

Msekwa alipoona sikukila kile chakula alitoka chumbani na kwenda kumuambia dada yake.Mara nikawaona wanaingia chumbani.

"Shemeji mbona hutaki kula?" Mkiwa akaniuliza

"Sitaki tu" nikamjibu.
"Si kawaida mtu kuwekewa chakula na mke wake akakataa bila
sababu,lazima ipo sababu.Mke wako ameniambia tangu jana umekataa chakula na hamzungumzi"

"Ni kweli lakini yeye atakueleza ni kwa kwanini nimekataa chakula na kwanini hatuzungumzi"

Mkiwa akamgeukia mdogo wake

"Msekwa hebu eleza kumetokea nini?"

Msekwa akaeleza yaliyotokea jana yake lakini hakuyaeleza sawasawa.Maelezo yake yalikuwa ni ya kunipa mimi lawama.

"Hebu sema ukweli mbele ya dada yako, niliporudi kazini nilikukuta wapi?" nikamuuliza

"Ulinikuta nimelala" akajibu

"Nilipokuuliza kuhusu chakula ulinijibu nini?"

"Chakula nilichelewa kupika kwa sababu nilienda harusini na nilikuaga"

"Ulichelewa kupika au uliniambia hukupika?"

"Si nilipika chakula ukakimwaga wewe!"

Hatua yake ya kugeuza geuza maneno ikaniudhi tena.

Nikamgeukia dada yake na kumueleza ukweli ulivyokuwa.Dada yake akaona mke wangu alikuwa na makosa.Kule kwetu wanaume ni watu wanaoheshimiwa sana.Ili kutusuluhisha Mkiwa akamgombesha sana mdogo wake na mwisho akamwaambia asingependa asikiye tena kuwa ameudia kosa kama hilo.

Msekwa akamjibu kuwa hatarudia.

"Sasa muombe msamaha mume wako" Mkiwa aliyeonekana kuwa mkali akamwaambia mdogo wake.

Mke wangu akaniangalia kisha akainamisha kichwa chini na kuniambia 

"Nakuomba unisamehe mume wangu"

Hapo nikahisi moyo wangu unakunjuka na kinyongo nilichokuwa nacho kinaondoka.

"Nimekusamehe" nikamwaambia kwa sauti tulivu.

"Basi naomba ule hicho chakula" akaniambia.

"Nimeshakula chakula huko nilikotoka lakini kwa vile umeniomba nitakula tena"

Nikaosha mkono na kula kile chakula.

Ugomvi wangu na mke wangu ukaishia hapo.

Asubuhi kulipokucha Mkiwa akaniambia anasubiri ikifika saa nne ataondoka arudi kijijini kwao, nikamjibu vyema.Wakati huo nilikuwa ninajindaa kutoka niende kazini.Baada ya kumaliza kuvaa sare zangu niliwaaga mke wangu na dada yake, nikatoka.Lakini nikakumbuka kuwa nilitoka bila kumuachia mke wangu pesa za matumizi na mke wangu naye alisahau kuniuliza.Nilikuwa nimeshafika mbali nikaamua kurudi na kuingia chumbani mwangu.

Lakini nilipoingia humo chumbani, sikuamini macho yangu. Nilijifuta uso nikatizama tena.Mke wangu alikuwa amelala chini huku damu zikimtoka kifuani.Kisu chenye mpini wa nchi tano kilikuwa kimezama kifuani kwake. Wakati namuangalia ndio alikuwa anavuta pumzi za mwisho na kukata roho.Kwa kweli nilishituka sana.Nikajiuliza je nilikuwa naota? lakini akili yangu iliniambia haikuwa ndoto.Nilichokiona kilikuwa kweli.Mke wangu amechomwa kisu na kuuawa mara tu nilipotoka.

Nikainama pale alipolala ili nimuangalie vizuri na kuyasadikisha macho yangu kama alikuwa ni yeye kweli.

Mara nikasikia mlango unafunguliwa nyuma yangu, Mkiwa akaingia.Alikuwa anatoka kuoga.

"Samahani nilijua umeshatoka" akaniambia halafu akamuona Msekwa aliyekuwa amelala chini. Mimi nikanyanyuka na kumgeukia yeye.

"Kitu gani kimetokea hapa?" nikamuuliza.

"Ha! shemeji umempiga kisu mke wako?" Mkiwa akang'aka na kuongeza "Mimi nilijua ule ugomvi umekwisha kumbe umemuwekea kisasi mwenzako!"

Vile nilivyomgeukia alidhani nilitaka kumkamata, akakurupuka na kutoka mbio huku akipiga kelele.

"Jamani mdogo wangu ameuliwa na mume wake....."

"Mimi siye niliyemuua,nimerudi sasa hivi na kumkuta ameshachomwa kisu.Sijui ni nani aliyefanya ushenzi ule" nikasema huku nikiwa ninamfuata Mkiwa aliyekuwa amekimbilia uani.

Wanawake waliokuwa uani pamoja na mama mwenye nyumba wakatushangaa.

"Jamani kuna nini, mbona mnatushitua?" mama mwenye nyumba aliuliza kwa hofu.

"Msekwa ameuliwa,amepigwa kisu kifuani na shemeji.Nendeni chumbani mwao mumuone!" Mkiwa akasema huku akilia

"Sikumpiga kisu shemeji, hebu nielewe.Mimi nilikuja na kumkuta ameshapigwa kisu. Mbona unataka kunitia katika hatia?" nikamwaambia kwa ukali kidogo.

"Ni wewe shemeji, ndiye uliyekuwa naye huko chumbani.Ni chuki za jana hizo"

Wanawake wote waliokuwa uwani wakaenda ukumbini, wakaingia chumbani mwangu.Mimi nilikuwa nikiendelea kueleza kile nilichokishuhudia.Kila aliyeingia mle chumbani alitoka mbio huku akipiga kelele.

Wanawake wengine walikimbilia uani wengine walikimbilia nje.Mama mwenye nyumba alinifuata na kunishika mkono na kuniuliza "Kwanini umefanya kitendo kama kile mwanangu?"

"Sikumpiga kisu mimi mama"

"Ni wewe, shemeji yako amekuona.Unakataa nini" mama mwenye nyumba akanikata kauli.

Balaa hilo! Je nini kitatokea? Ili kupata jibu endelea kuitembelea blog yako kila siku bila kukosa.
Kwa habari, matukio michezo na burudai ni hapahapa Tangakumekuchablog


1 comment:

  1. Huu ni lazima ushuhudia usomaji na kila mtu, nipo hapa kuruhusu ulimwengu wote kujua kuhusu mtu aliyeokoa uhusiano wangu na mtu huyu mkuu anaitwa Dr IZOYA. Hakika alifanya kazi nzuri kwangu kwa kumrudisha mpenzi wangu wa zamani ambaye aliniacha na kuahidi kamwe kurudi kwangu tena. Kwa hili, nimekuja kutambua kuwa kutoa maelezo ya Dk IZOYA kwa ulimwengu utafanya mengi mazuri kwa wale walio na nyumba zilizovunja au uhusiano kwa ajili yake ili kukusaidia kurekebisha uhusiano huo uliovunjika au ndoa yako. Unaweza kumfikia kupitia barua pepe yake: drizayaomosolution@gmail.com. Kuwasiliana naye na kuona jinsi tatizo lako litatatuliwa ndani ya 24hours. Pia mtaalamu katika mambo yafuatayo ...
    (1) Unataka kurudi nyuma yako.
    (2) Unataka kukuzwa katika ofisi yako.
    (3) Unataka wanaume / wanawake kukufuate.
    (4) Unataka mtoto.
    (5) Wewe ni mjasiriamali na unataka kushinda mikataba
    (6) Unataka mume wako awe wako milele
    (7) Unahitaji msaada wa kiroho.
    (8) Umeshambuliwa na unataka kupona fedha zilizopotea.
    (9) Weka talaka
    (10) Kualika kwa mila ya fedha
    (11) Chagua uchaguzi

    ReplyDelete