HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 17
ILIPOISHIA
“Unadhani lini utakuwa na
nafasi nzuri, siku ambayo si ya kazi?”
“Jumapili mchana nikitoka
kanisani”
“Nitakupata wapi?”
“Hapa hapa”
“Naomba unipatie namba yako
ya simu”
Maria hakuwa na uchoyo na
namba yake, akampa. Kweka naye akampa namba yake. Baada ya kumaliza chakula
Kweka alimpa Maria shilingi laki moja.
“Zitakusaidia kununulia vocha
ya simu”
“Asante
sana,
nashukuru”
Wakaagana. Siku ya jumapili
Maria alitimiza ahadi. Alipotoka kanisani alipanda teksi hadi mkahawa wa
Afrique. Alipofika akakutana na Kweka.
Siku ile ndio Kweka alimtolea
undani wake. Alimwambia wazi kuwa alikuwa akimuhitaji katika maisha yake. Kule
kutoa kauli ya kukubali tu, Kweka alimpeleka ‘shopping’ siku ile ile.
Alimfanyia shoping ya shilingi laki tano.
SASA ENDELEA
Kutoka hapo Kweka na Maria
wakawa wapenzi. Siku zote walikuwa wakikutana kwenye mahoteli tu. Maria aliwahi
kumfikisha nyumbani kwake mara kadhaa lakini Kweka hakumuonesha Maria alikuwa
anaishi wapi zaidi ya kumwambia kuwa alikuwa akiishi Masaki.
Mapenzi yalipowakolea
walifunga uchumba. Uchumba huo ulidumu kwa mwezi mmoja tu kabla ya Maria kupata
balaa la kukamatwa na kuwekwa ndani.
Kweka alikuwa ameshitakiwa
kwa kugushi nyaraka za wizara kwa ajili ya shughuli zake binafsi. Alipotolewa
kwa dhamana alimtuma Maria kulitafuta faili la kesi yake hapo mahakamani na
kuchomoa nyaraka muhimu za ushahidi ili kuharibu kesi.
Maria kwa sababu ya kutaka
mpenzi wake asifungwe alifanya hivyo. Uchunguzi ulipofanyika ilibainika kuwa
baadhi ya nyaraka za ushahidi hazikuwemo kwenye faili la Kweka. Shuku ikaenda
kwa Maria. Maria akashukiwa kuzichomoa nyaraka hizo.
Polisi walimkamata
akafunguliwa mashitaka. Wakati yeye akiendelea na kesi, Kweka alikuja kuachiwa
kutokana na kukosekana kwa ushahidi. Uamuzi huo ulikuja baada ya kesi yake
kuchukua muda mrefu.
Baada ya Kweka kuachiwa
hakushughulika tena na Maria. Alibadili namba yake ya simu. Maria akawa hampati
kwenye simu. Alikuwa akimtafuta ili amueleze kuwa kesi yake ilikuwa imekaa
vibaya na kwamba alihitaji pesa za kuweka wakili.
Maria alipogundua kuwa Kweka
alikuwa amemtosa, pengine akiamini kuwa angemtaja mahakamani aliamua kuachana
naye.
Ulikuwa ni wakati ule
anakutana na James ambaye alimwambia kuwa alikuwa na mchumba wake lakini mwisho
akamwambia hakuwa na mchumba bila kumfafanulia.
Mungu si Athumani, hakimu
aliyekuwa akisikiliza kesi ya Maria alimuachia huru kwa kukosekana kwa ushahidi
wa kutosha kwamba ni yeye aliyechomoa nyaraka hizo.
Siku chache baada ya Maria
kuachiwa huru Kweka alianza kumpigia Maria. Maria alipokea simu yake na
kumuuliza alikuwa akihitaji nini.
“Maria nilikuwa London, nimerudi jana”
Kweka alimwambia Maria kwenye simu.
“Kwenda zako, wewe ni tapeli
mkubwa. Sina hamu ya kukuona wala usinipigie simu”
“Maria unanijibu hivyo,
kumbuka tunatoka wapi?”
“Kwanini hukukumbuka wewe
wakati ule nakabiliwa na kesi. Leo unaona nimeachiwa ndio unanipigia simu. Wewe
mwanaume mbaya sana.
Ulinituma nikuchomolee nyaraka nikafanya hivyo ili kukusaidia wewe, halafu
ukaamua kunitosa!”
“Sijakutosa, nimekwambia
nilikuwa safari na safari yenyewe ilikuwa muhimu kwa maisha yetu. Nikubalie
mchumba wangu ili tuanze kupanga harusi yetu”
“Kwenda zako tapeli mkubwa.
Ulikuwa hapa hapa nchini, sema ulibadili namba yako kwa kujua ningefungwa, hata
utu huna. Ulishindwa kukumbuka kwamba wewe ndiye uliyeniponza!”
“Kwa hiyo umeamua kuvunja
uchumba wetu?
“Uchumba umeshavunjika muda
mrefu hivi sasa nina mchumba mwingine anaayenipenda na kunijali”
“Kumbuka kwamba nilikupa pesa
zangu nyingi”
“Na wewe kumbuka kwamba
ulinitumia sana
mpaka ukasababisha nipate kesi”
“Maria fikiria tena uamuzi
wako”
“Sifikirii na nimesha amua!”
Maria akakata simu.
Tangu siku ile Maria hakupokea
tena simu za Kweka.
Ndipo Kweka alipomtafuta
Simon Puto, muuaji wa kukodiwa. Simon alikuwa akiishi nchini Kenya ambako
alifanya mauaji mengi. Baada ya msako wa kumtafuta kupamba moto alirudi nchini.
Akiwa jijini Dar
alishirikiana na vikundi vingi vya ujambazi. Baada ya wenzake wengi kuishia
mikononi mwa polisi aliamua kujitenga na vikundi na kufanya kazi peke yake.
Yeye na Kweka walipeana ahadi
kwenye simu wakutane katika hoteli ya New Africa. Walipokutana ndipo Kweka
alipompa kazi ya kumpeleleza Maria ili kujua kama kweli alikuwa na mchumba
mwingine.
Ili kufanya upelelezi wake kwa ufanisi Kweka
alimpa Simon shilingi laki tano.
Simon akaanza kazi ya
upelelezi, akaja kugundua kuwa Maria alikuwa akishirikiana na kijana mmoja
aliyekuwa akiishi Msasani.
Kazi yake kubwa ilikuwa ni
kumuandama James kutoka nyumbani kwake hadi kazini kwake kila asubuhi.
Alikuwa akimsubiri, anapotoka
mchana aliendelea kumfuatilia hadi sehemu anayokwenda kula. Jioni alikuwa nyuma
yake hadi anafika nyumbani kwa Maria.
Ndipo siku moja alipomuibukia
James katika hoteli ambayo alikwenda kula chakula cha mchana, akamuuliza kama
alikuwa na uchumba na Maria. (Rejea sehemu ya tatu ya riwaya hii) James
akamjibu kuwa Maria alikuwa mchumba wake.
Akamuuliza pia walitarajia
kuoana lini swali ambalo lilimshitua James na kutaka kujua mtu huyo alikuwa
nani. Hatimaye Pascal aliondoka na kumuacha James akiwa na wasiwasi.
Jioni yake Pascal aliibukia
nyumbani kwa Maria ambako alijirushia picha za Maria kutoka kwenye simu ya
Maria. Picha hizo alimpelekea Dokta Kweka ili kumthibitishia kuwa Maria ana
mchumba.
Dokta Kweka alipopata uhakika
kwamba Maria alikuwa na mchumba na kwamba angeoana naye karibuni alimwambia
Simon Puto.
“Nataka unifanyie kazi moja
tu, nitakulipa kiasi chochote unachotaka”
“Kumbuka kwamba hii kazi ya
awali uliyonipa nimeikamilisha”
“Ndiyo, hii imekamilika.
Nataka kukupa kazi nyingine amabayo ni nzito kidogo”
“Kazi gani?”
“Nataka umuue Maria!”
“Kwanini?”
“Si juu yako kujua hilo kwa
sasa na halina umuhimu na wewe. Kilicho muhimu kwako ni kuniambia unataka kiasi
gani?”
Simon alipitisha muda kidogo
kabla ya kumuuliza.
“Unataka nimuue kwa lini?”
“Ukiweza hata leo. Sitaki
aishi. Si tu atanisononesha roho yangu bali pia amenitenda vibaya”
“Wewe unataka kunipa kiasi gani
kwa kazi hiyo?”
“Sijui. Niambie wewe unataka
kiasi gani?”
“Nipatie shilingi milioni
tano”
“Nitakupa nusu yake, ukimuua
Maria nakumalizia kiasi kilichobaki”
“Nipatie”
Dokta Kweka alifungua mkoba
wake ambao wakati wote amekuwa akitembea nao. Alitoa burungutu la noti,
akahesabu shilingi milioni mbili na laki tano akampa Simon.
“Umenipa kiasi gani?”
“Milioni mbili na nusu
taslim, zihesabu”
“Sihitaji kuzihesabu. Kama wewe umehakikisha ni kiasi hicho inatosha”
Simon alizitia kwenye mifuko
ya koti alilokuwa amevaa.
ITAENDELEA kesho hapaha pa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment