HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 18
ILIPOISHIA
“Ni kweli alinituma nimuue
Maria. Sikujua ni kwanini alitaka Maria afe lakini mbali na hilo bila shaka
alijua kuwa nitakamatwa na alishapanga kumchukua mke wangu. Mtu yule ni mshenzi
sana”
“Nataka uende ukamuue!” James
alirudia kumwambia kwa mkazo.
“Ameniweka katika wakati
mgumu hivi sasa. Miezi sita niliyokaa ndani nimepoteza kila kitu, nyumba, mke
na pesa…”
“Kwa tatizo la pesa
nitakusaidia. Unahitaji kiasi gani cha kuanzia maisha?”
“Kama milioni moja hivi”
“Nitakupatia laki tano,
ukimuua huyo mtu aliyekutuma umuue Maria, nitakumalizia laki tano hapo hapo”
“Utanipatia sasa hivi?”
“Kama tumekubaliana
nitakupatia”
“Bado nitkuwa na tatizo la
usafiri”
“Nitakukodia gari”
“Sawa. Nipatie hizo pesa na
usafiri. Nitakwenda kumuua”
“Unadhani utaweza kumpata kwa
leo?”
“Kwa leo si rahisi, nipe siku
tatu”
“Sawa. Sasa twende kwenye ATM
nikatoe pesa”
James akanyanyuka. Simon naye
akainuka. Walitoka nje wakajipakia kwenye gari la James na kuondoka.
“Ulifahamianaje na Dokta
Kweka?” James alimuuliza Simon wakati gari likiwa kwenye mwendo.
“Alinitafuta”
SASA ENDELEA
“Umesema hujui ni kwanini
alitaka Maria afe?”
“Sijui”
“Nilikuja kugundua kuwa Maria
alikuwa mchumba wake. Maria akavunja uchumba baada ya kukutana na mimi. Hicho
ndicho kilichomtia uchungu”
Simon akamkubalia kwa kichwa.
“Sikuona sababu ya wewe
kunyongwa, yeye abaki akiwa mzima. Bali niliona sababu ya wewe kubaki mzima ili
umuue yeye” James akamwambia Simon.
“Ulifanya uamuzi wa busara
sana. Kwa sababu yeye ni jeuri nitamuua na nitamchukua mke wangu. Bila kumuua
sitaweza kumpata”
Walikwenda katika ATM, James
akatoa shilingi laki nne. Alirudi kwenye gari akampa Simon pesa hizo.
“Hizo ni shilingi laki nne”
alimwambia huku akiliondoa gari. Akaongeza.
“Shilingi laki tatu ni zile
tulizozungumza na shilingi laki moja ni ya kukodi gari”
“Sawa” Simon alimkubalia na
kuzitia pesa hizo mifukoni.
“Sasa nikupeleke wapi?”
“Kaniache mjini ili niweze
kukodi gari”
“Tutawasiliana vipi?”
“Sina simu”
“twende nikakununulie moja”
Walikwenda Kariakoo. James
alisimamisha gari kwenye duka moja la simu. Akashuka na Simon. Waliingia kwenye
duka hilo James akanunua simu moja ya bei rahisi na kumpa Simon.
Alimuandikia namba yake ya
simu na kumpa.
“Namba yangu ni hiyo.
Ukinunua laini utanipigia” alimwambia.
“Usijali”
Wakaachana hapo hapo.
Simon alikwenda kuazima gari
la jambazi mwenzake. Aliliomba kwa siku tatu na akampa ile shilingi laki moja.
Alikwemda kujaza mafuta mwenyewe.
Breki yake ya kwanza ilikuwa
nyumbani kwake Temeke. Alitaka aanze uchnguzi ili ajue kama kweli mke wake
hakuwepo. Alipobisha mlango wa nyumba hiyo aliyetoka alikuwa mwanamke mwingine.
“Karibu” aliambiwa huku
mwenyeji wake akimtazama machoni.
“Namuulizia Vicky”
“Humu ndani hakuna mtu
anayeitwa Vicky” alijibiwa.
“Alikuwepo labda kama
amehama”
“Inawezekana ni mpangaji wa
zamani kwani sisi tumeingia katika nyumba hii kama miezi minne iliyopita”
“Sawa, basi asante sana”
Simon alipoondoka hapo aliona
akatafute gesti ya kupangisha chumba atakacholala siku ile na kisha aanze
kumtafuta Dokta Kweka.
Alipata chumba katika gesti
moja iliyokuwa Kimara. Hapo hapo alinunua laini na kuchaji simu aliyonunuliwa.
Wakati simu inapata chaji alikwenda kwenye mkahawa mmoja ulio jirani kupata
chakula. Wakati anakula mawazo yalikuwa yametanda kwenye kichwa chake.
Alijiambia kuwa Dokta Hiza
alikuwa amemtenda kosa baya sana kumchukua mke wake na hivyo atakapokutana naye
hatakuwa na sababu yoyote ya kumlaumu wala kubishana naye.
“Nitamlipua hapo hapo!”
alijiambia kwa hasira.
Baada ya kumaliza kula
alirudi gesti akaichukua simu na kupiga namba za mke wake. Simu yake iliita
kisha ikapokelewa.
“Halo Vicky!”
“Wewe nani?” Sauti
aliyoitambua kuwa ni ya Vicky ikamuuliza.
“Mimi Simon, nimetoka jela
leo. Uko wapi?”
“Ndoa yetu ilishavunjwa na
Padre baada ya wewe kukabiliwa na kesi ya mauaji. Hivi sasa mimi si mke wako
tena. Naomba usinipigie simu”
Simon sasa aliamni kuwa Vicky
alikuwa amechukuliwa na Dokta Kweka.
“Padre gani aliyevunja ndoa
yetu wakati mimi nipo? Ni nani huyo aliyekupa wazo la kwenda kwa Padre?” Simon
akamuuliza.
Hapo hapo Simon alisikia
sauti ya Dokta Kweka kwenye simu ikimuuliza.
“Wewe nani?”
“Mimi Simon, ninahitaji
kuonana na wewe”
“Sikutambui. Tafadhali acha
kufuatilia maisha ya watu”
Simu ikakatwa. Simon alipiga
tena lakini simu haikupokelewa.
Sasa alikuwa ameugundua
ushenzi wa Dokta Kweka.
“kitendo chake
hakitasameheka!” alijiambia kwa hasira.
Alikumbuka kwamba mke wake
hakuwa amefika mahakamani tangu aliposomewa mashitaka ya mauaji. Akajimbia
kutofika kwake kunatokana na kurubuniwa na Dokta Kweka.
“Kama alikwenda kweli kwa
Padre kuvunja ndoa yetu alipelekwa na Kweka ili ahalalishe ufuska wake” Simon
alijiambia.
“Sasa sina haja tena ya
kungoja kuhakikisha, nimeshahakikisha na kuthibitisha kuwa Kweka ni mpenda
wanawake na amemchukua mke wangu” Simon aliendelea kujiambia.
Alihakikisha kuwa kilichobaki
kwa upande wake ni kitu kimoja tu, kumuonesha Kweka kuwa yeye Simon alikuwa
mshenzi zaidi. Na hilo atalijua Kweka akiwa ahera.
Simon alijilaza kitandani
akaendelea kuwaza hadi saa kumi jioni. Alikwenda kuoga na kuvaa tena nguo
zilezile alizotoka nazo jela. Wakati wote alikuwa akimlaani Dokta Kweka.
Alipomaliza kuvaa alitoka
akajipakia kwenye gari na kuelekea nyumbani kwa James. Alipofika alishuka
kwenye gari akabisha mlango. Mlango ulifunguliwa na James aliyekuwa amejifunga
taulo kunoni.
“Karibu Simon, nimefarijika
kukuona tena” James alimwambia.
Simon alipita ndani.
“Karibu ukae” James
alimwambia huku akifunga mlango.
Simon akakaa. James naye
alikaa kando yake.
“Nimegundua kuwa maneno
uliyoniambia ni ya kweli” Simon akamwambia James.
“Umegunduaje?”
“Nilimpigia simu Vicky
akaniambia ameshavinja ndoa yangu kwa Padre hivyo mimi si mume wake tena”
“Nilikueleza hivyo baada ya
kufanya utafiti wa kina”
“Halafu hapo hapo Dokta Kweka
alichukua simu kutoka kwa Vicky
akaniambia hanitambui na nisifuatilie maisha yao”
“Umechukua hatua ya maana
kusadikisha maneno yangu. Huo ndio ukweli wenyewe”
“Sasa kuna kitu kimoja…”
“Kitu gani?”
“Nataka unipe pesa ya kukodi
bastola, kwa sasa sina bastola”
“Kiasi gani?”
“Kukodi kwa siku moja ni
shilingi elfu themanini, nitaihitaji kwa siku tatu”
“Kwa hiyo itakuwa laki mbili
na arobaini”
“Ndiyo, laki mbili na
arobaini”
“Utazihitaji sasa hivi?’
“Ikiwezekana”
“Subiri”
James alinyanyuka akaingia
chumbani kwake. Baada ya muda kidogo alitoka akiwa na shilingi laki mbili na
arobaini mkononi.
“Chukua”
Alimpa Simon ambaye
alizipokea na kuzitia kwenye mfuko wa koti lake.
“Utahitaji kitu kingine?”
James alimuuliza huku akiketi.
“Nikihitaji nitakwambia”
“Unapafahamu anapoishi huyu
mtu”
ITAENDELEA.
No comments:
Post a Comment