HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 24
ILIPOISHIA
Inspekta Temba akagutuka.
“Ulimuona wakati gani na
alikuwa wapi?”
“Wakati nashuka kwenye teksi
nilimuona”
“Ulimuona wapi?”
“Nilimuona akitoka kwenye
mlango wa hoteli”
“Halafu akaenda wapi?”
“Sikumpatiliza tena, mimi
nilijifanya kama sikumuona nikaingia hoteli.
Na ndio nikaenda kumkuta Kweka ameuawa kule chumbani”
“Yeye alikuona?”
“Nina hakika kuwa aliniona”
“Alikusemesha chochote?”
“Hakunisemesha”
“Je aliwahi kukwambia au
kumwambia marehemu kuwa atafanya kitu?’
“Hakuwahi kuniambia wala
kumwambia marehemu kuwa atafanya kitu lakini nina shaka naye”
“Ungetuambia tangu jana
tungelikwisha mkamata. Anaweza kuwa mtuhumiwa namba mbili. Anapatikana wapi?”
“Kwa sasa sijui anapatikana
wapi?”
“Unadhani tutampataje”
“Hapo siwezi kujua”
“Una namba yake ya simu?”
SASA ENDELEA
“Ndiyo ninayo, aliwahi
kunipigia”
“Alikupigia kukueleza nini?”
Alipotoka jela alinipigia
kuniuliza niko wapi, ndipo nilipomjibu kuwa nimeolewa na mwanaume mwingine”
“Akakwambia nini?”
“Alisikitika tu”
“Sasa tupe namba yake”
“Simu yangu mnayo nyinyi,
nilinyang’anywa tangu jana”
“Sawa. Tutakupatia utupe
namba yake”
Temba alimuagiza yule polisi
mwanamke akalete simu ya Vicky. Polisi huyo
alikwenda kuichukua simu ya Vicky na kumpa Temba.
“Mpe mwenyewe” Temba
alimwambia.
Vicky alipopewa simu
aliiwasha. Baada ya sekunde chache akaisoma namba ya Simon.
“Sasa sikiliza, ninataka
umpigie umwambie mkutane sehemu muda huu ili akija tuweze kumkamata”
“Nimwambie tukutane sehemu
gani”
“Wewe unafikiri wapi anaweza
kuja haraka”
“Kwa hapa kwenye kituo
hataweza kuja”
“Si hapa. Sehemu nyingine
yoyote hata kama ni kwenye hoteli. Tunaweza
kwenda kumsubiri”
Vicky akampigia Simon.
“Utamwambia mkutane wapi?”
Temba akamuuliza huku simu inaita.
Kabla ya Vicky kujibu simu
ilikwishapokelewa.
“Hallo…Simon nahitaji
kukuona” Vick akasema kwenye simu.
“Uko wapi?” Sauti ya Simon
ikasikika.
“Niko hapa New Africa Hotel”
“Nisubiri hapo hapo, ninakuja”
“Sawa”
“Twende New Africa
Hotel, anakuja” Vicky akamwambia Temba.
Simon alikuwa ndio amemaliza
kuvaa akiwa kwenye chumba cha gesti aliyokuwa amepangisha chumba tangu
alipoachiwa na mahakama kutokana na kesi ya mauaji iliyokuwa inamkabili.
Katika hisia zake aliamini
kuwa Vicky hakuwa tena na pa kushika baada Dokta Kweka kuuawa. Hivyo alikuwa
anamuita ili wazungumzie tofauti zao.
Pia Simon alijua kuwa Vicky
alishaachiwa na polisi baada ya kukamatwa jana yake katika hoteli ya Suzy
ambako Dokta Kweka alikuwa ameuawa
Hisia kwamba Vicky alitaka
kurudisha uhusiano wao na ndio sababu amempigia simu, ilimfariji Simon kutokana
na ukweli
kwamba bado alikuwa akimpenda. Hivyo aliharakisha kuvaa akatoka na kujipakia
kwenye gari alilokuwa amelikodi kwa kazi ya kumuua Dokta Kweka.
Aliificha bastola yake chini
ya siti aliyokuwa amekaa kwani kazi yake ilikuwa imekwisha. Alikuwa akisubiri
apewe pesa na James airudishe alikoikodi.
Akaliwasha gari hilo na kuliendesha hadi New Africa Hotel akiwa
na tamaa ya kumpata Vicky. Wakati huo Vicky alikuwa ameketi kwenye ukumbi wa nje wa New Africa
akiwa katika meza ya peke yake akinywa soda aliyonunuliwa na Inspekta Temba.
Katika meza ya jirani yake
kulikuwa na makachero watatu ambao walikuwa wakizungumza.
Inpekta Temba mwenyewe
alikuwa akisubiri kwenye gari lililokuwa jirani na hoteli hiyo maarufu.
Wakati Vick akiendelea kunywa
soda simu yake ikaita. Alipoitazama aliona namba ya Simon. Akaipokea.
“Hallo Simon…vipi?”
“Umekaa
sehemu gani?”
“Niko kwenye ukumbi wa nje wa hoteli, ukiingia tu
utaniona”
“Okey, ninakuja”
“Kwani umeshafika”
“Nimeshafika”
“Sawa. Ukiingia tu kwenye huu
ukumbi
wa nje utaniona” Vicky alimwambia Simon na kukata simu.
Simon alikuwa amelisimamisha
gari kwenye eneo la kuegesha la hoteli akafungua mlango na kushuka. Alitembea
hadi kwenye mlango wa kuingilia ambapo alitupa macho kwenye ukumbi huo na
kumuona Vicky aliyekuwa ameketi katika meza ya peke yake.
Aliingia na kutembea hadi
kwenye meza hiyo akavuta kiti na kuketi.
“Hujambo mke wangu” Simon akamsalimia
Vicky kwa tabasamu.
“Sijambo. Na wewe hujambo?”
“Mimi sijambo. Tatizo langu
lilikuwa kwa upande wako kwani bado naamini wewe ni mke wangu”
Vicky aligeuza uso
akawatazama makachero waliokuwa wameketi kwenye meza ya karibu kisha akaurudisha uso wake kwa Simon.
“Na mimi pia ninaamini hivyo,
ndio maana nimekuita tuzungumzie hilo”
Ghafla Simon akajikuta
amezungukwa na makachero. Kachero mmoja alimuonesha kitambulisho chake na
kumwambia.
“Sisi ni askari wa upelelezi,
tunakuhitaji kituo cha polisi!”
Simon akashituka na kuwatazama makachero hao.
“Kuna nini tena?” akawauliza.
“Utaelezwa, usiwe na
wasiwasi” Kachero mmoja akamwambia.
Simon akamtazama Vicky.
“Wewe ndio umepanga njama
hizi?’ akamuuliza.
Vicky akabetua mabega yake
bila kusema chochote.
Simon akainuliwa kwenye kiti.
“Kuwa mstaarabu, jaribu
kutekeleza kile unachoambiwa” Kachero mmoja alimwambia Simon.
Baada ya kumtupia jicho kali
Vicky Simon aliongoza njia. Alitolewa nje ya hoteli na kupakiwa kwenye gari la
polisi ambalo ndani yake alikuwemo Inspekta Temba.
Vicky naye alipakiwa kwenye
gari hilo hilo,
wakaondoka.
Walipofika kituo cha polisi,
Vicky na Simon walitenganishwa. Vicky alirudishwa mahabusi, Simon akapelekwa
ofisini kwa Inspekta Temba.
Simon hakuwekwa kwenye kiti,
alikaa chini.
“Msichana uliyekuwa ukiongea naye
pale hoteli mnafahamiana vizuri?” Temba akamuuliza.
“Ndiyo tunafahamiana vizuri”
“Unaweza kunieleza uhusiano
wenu ulivyo?”
“Yule ni mke wangu”
“Ni mke wako hadi hivi sasa?”
“Tulikuwa tumetengana
kidogo…”
“Kwa vipi?”
“Niliwahi kupata matatizo
kidogo ya kipolisi nikashitakiwa kwa kuhisiwa kuwa nilifanya mauaji ya msichana mmoja lakini mahakama
ikaona sikuwa na hatia ikaniachia huru. Sasa niliporudi uraiani Vicky akaniambia kuwa alidhani
ningenyongwa hivyo ndoa yetu alishaivunja kwa Padre”
“Unamfahamu mtu anayeitwa
Kweka?”
Simon alishituka alipoulizwa
swali hilo.
Mshituko wake ulionekana waziwazi.
Akajiambia akijibu kuwa
hamfahamu atajiingiza katika matatizo kwani hakujua Vicky aliwaeleza nini
polisi.
“Namfahamu” akajibu baada ya kusita
kidogo.
“Tueleze unavyomfahamu?”
“Ni rafiki yangu”
“Ni kweli kwamba alimuoa mke
wako baada ya wewe kuwekwa ndani kutokana na kesi iliyokuwa inakukabili?’
Simon aligundua kuwa hilo swali lilikuwa la
mtego.
“Vicky aliwahi kunieleza kuwa
aliolewa na mtu mwingine lakini nilimwambia kuwa hakupaswa kuolewa”
“Alikwambia aliolewa na
nani?”
ITAENDELEA kesho hapahapa usikose
No comments:
Post a Comment